POLISI nchini Kenya hivi sasa ipo katika msako mkali kufuatia
tukio la mauaji ya watu wanne na wengine kadhaa kujeruhiwa kwenye
mashambulizi yaliyofanywa na watu wasiofahamika katika mkutano wa
kisiasa mjini Mombasa.
Mkutano huo ulitarajiwa kuhutubiwa na waziri ustawi wa uvuvi wa nchi
hiyo, Amason Kingi, ambaye alinusurika. Hii ni mara ya pili kwa
mashambulizi kama hayo kufanyika ndani ya wiki moja katika eneo hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Agrey Adoli, ameiambia DW kwamba
majeruhi wamepelekwa hospitali na wanaendelea vizuri.
Kamanda Adoli
amesema kwamba polisi haikuwa na taarifa kuhusu kufanyika kwa mkutano
huo, na ndio sababu washambuliaji waliweza kuuvamia na kufanya
mashambulizi hayo.
Miongoni mwa waliojeruhiwa ni aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya rufaa
nchini Kenya Stewart Madazayo ambaye ametangaza kuwania kiti cha useneta
wa jimbo la Kilifi, kwenye uchaguzi mkuu Ujao hapo mwakani.
Namna mashambulizi yalivyofanyika
Kijiji cha Chamwanamuma kikiwa kimechomwa kabisa kwa washambuliaji.
Mashambulizi hayo yalitokea wakati viongozi hao wa siasa walipofika
katika uwanja wa shule ya Mtumondoni iliyoko Mtwapa nje kidogo tu ya Mji
wa Mombasa, wakati kundi la vijana wenye mapanga walipokwenda moja
moja hadi kwenye jukwaa wakitaka kuukatiza mkutano huo.
Mlinzi wa Waziri Kingi alikuwa wa kwanza kushambuliwa alipojaribu kutoa
bastola yake, na kupata majeraha mengine ya panga kichwani. Hata hivyo,
mlinzi huyo alifariki dunia muda mfupi tu baada ya kufika hospitalini.
Mgombeaji wa kiti cha useneta katika jimbo la Kilifi, Jaji Madzayo,
ambaye ndio alikuwa jukwaani kuhutubia umati, alikatwa kwa panga
kichwani na kuzimia na anaendelea kupata matibabu hospitalini.
Hata hivyo, umati uliokusanyika kuwasikiliza viongozi hao waliwazingira
washambuliaji hao na kuwaua watatu miongoni mwao.
Mkuu wa Polisi wa
wilaya ya Kilifi, Climent Wangai, anasema kuwa bado hakuna mshukiwa
aliyekamatwa au kundi lolote kudai kuhusika na mashambulizi hayo.
Mapigano katika mtaa wa mabanda wa Mathare nchini Kenya mwaka 2008.
Mashambulizi hayo yanatokea siku nne tu baada ya mashambulizi
mengine kama hayo kufanyika katika eneo la Ganze ambako watu 15 waliuawa
baada ya kundi la majambazi wanaodaiwa walikuwa wakila kiapo kwa lengo
la kutekeleza mashambulizi kuuawa na wanakijiji.
Wakati wa mkasa huo, polisi walidai kukamata bendera ya kundi
linalojiita FEDERESA, ambalo linadai kuwa limeunda serikali yake iliyo
na baraza la mawaziri 17.
Kundi la Mombasa Republican Council (MRC) ambalo ni vuguvugu
linalopigania ukombozi wa mkoa wa Pwani, na ambalo linanyooshewa kidole
kuhusika na mashambulizi ya aina hii, limepinga vikali kuhusika na visa
hivi huku likiishtumu serikali "kwa njama ya kutaka kulitia lawamani",
kwa mujibu wa msemaji wa kundi hilo, Mohammed Mraja.
Katika siku za hivi punde visa vya mashambulizi yanayofanywa na watu
wasiojulikana vinaongezeka katika eneo la mkoa wa Pwani, kwa kiwango cha
kutia hofu.
0 comments:
Post a Comment