BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MAHAKAMA YA RUFANI YAFUNGA MVUTANO WA UMRI WA LULU.


MAHAKAMA ya Rufani imefunga mjadala wa utata wa umri wa msanii wa fani ya filamu nchini, Elizabeth Michael  maarufu kama Lulu anayekabiliwa na kesi ya mauaji, baada ya kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu.

Sambamba na uamuzi huo wa kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu, pia Mahakama ya Rufaa imeamuru jalada la kesi hiyo lirejeshwe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili kuendelea na mwenendo wa kesi ya msingi.

Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akituhumiwa kumuua msanii mwenzake, Steven Kanumba. 


Anadaiwa kutenda kosa hilo April 7, 2012 nyumbani kwa marehemu, Sinza jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, umri wake ulizua mvutano mkali baina ya upande wa mashtaka katika kesi hiyo [Jamhuri], na  jopo la mawakili wanaomtetea, mvutano ambao ulianzia Mahakama ya Kisutu na kuendelea hadi Mahakama ya Rufani, huku kesi ya msingi ikiwa bado haijaanza kusikilizwa.

Juni 11, 2012  Mahakama Kuu ilikubali kufanya uchunguzi wa umri halali wa mshtakiwa huyo, kufuatia maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na jopo la mawakili wanaomtetea mshtakiwa huyo.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda, akisaidiana na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro, waliwasilisha maombi Mahakama ya Rufani wakiiomba Mahakama ya Rufani ifanye marejeo ya uamuzi huo wa Mahakama Kuu  kama ulikuwa ni sahihi.



Jana jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani likiongozwa na January Msoffe [Mwenyekiti wa jopo], akisaidiana na Jaji Bernard Luanda na Jaji Edward Rutakangwa, lilizima mvutano na badala yake likaamuru kuendelea kwa kesi ya msingi.

Katika uamuzi wake uliosomwa jana na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Zahra Maruma, jopo hilo kwanza lilisema kuwa maombi ya marejeo ya uamuzi wa mahakama kuu yaliyowasilishwa na Jamhuri yalikuwa ni batili.

Lilibainisha kuwa kifungu cha 4 (2) cha Sheria ya Mahakama ya Rufani, ambacho Jamhuri ilikitumia kuwasilisha maombi hayo ya marejeo si sahihi kwa kuwa kifungu hicho kinatumika pale tu panapokuwa na rufaa katika mahakama hiyo ya Rufaa.

“Kwa kuwa hakuna rufaa yoyote katika mahakama hii, basi kifungu hicho hakikuwa sahihi kutumika kuwasilisha maombi haya ya mnarejeo.”, lilisema jopo hilo katika uamuzi wake huo.

Kwa mujibu wa jopo hilo, kifungu sahihi kilichostahili kutumika ni Kifungu cha 4 (3), ambacho ndicho kinachoeleza Mamlaka ya Mahakama ya Rufani kufanya marejeo ya uamuzi wa Mahakama Kuu kujiridhisha  na usahihi wake.

Pia Jopo hilo lilisema kuwa maombi hayo ya Jamhuri ya marejeo hayakuwa sahihi kwa kuwa hayakueleza sababu za kuomba marejeo hayo, kinyume na Kanuni ya 48 (1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani za mwaka  2009.

“Kwa kushindwa kutoa kifungu sahihi na kutokubainisha sababu za marejeo haya, kunayafanya maombi haya yasiwe halali mbele ya mahakama hii, ” lilisema jopo hilo katika uamuzi wake huo.

Hata hivyo licha ya maombi hayo ya marejeo ya Jamhuri kuwa batili, pia Jopo hilo lilisema kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu kuchukua  jukumu la kufanya uchunguzi wa umri wa mshtakiwa 

huyo haukuwa sahihi.



Kwanza  jopo hilo lilikubaliana na hoja za upande wa Jamhuri kuwa maombi ya uchunguzi wa umri wa mshtakiwa huyo yaliyowasilishwa Mahakama Kuu na mawakili wake  hayakuwa halali kwa kuwa yaliwasilishwa isivyo sahihi kisheria.

Hivyo Jopo hilo la majaji lilisema kuwa, Mahakama  Kuu haikupaswa kuendelea nayo zaidi ya kuyatupilia mbali, na likaongeza kuwa hata vifungu vya sheria ambavyo Mahakama Kuu ilivitumia kuchukua  jukumu hilo haviipi mamlaka hayo.

Jopo hilo lilibainisha kuwa, kile ambacho Mahakama Kuu ilipaswa kukifanya ni kurejesha jalada la kesi hiyo katika Mahakama ya Kisutu na kutoa maelekezo kwa mahakama hiyo, na si yenyewe [Mahakama Kuu] kuchukua jukumu hilo.

“Kutokana na sababu hizo tulizozieleza hapo juu, tunatupilia mbali uamuzi wa Mahakama Kuu, na tunaamuru Jalada  la kesi hii lirejeshwe katika Mahakama ya Kisutu ili kuendelea na mwenendo wa kesi ya msingi.”, lilihitimisha jopo hilo katika uamuzi wake.

Licha ya kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu na kuamuru jalada la kesi lirejeshwe katika Mahakama ya Mkazi Kisutu kuendelea na mwenendo wa kesi ya msingi, jopo hilo halikusema chochote kuhusu utata wa umri wa mshtakiwa huyo wala kuelekeza namna ya kuutatua.

Hata hivyo wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo ya marejeo, Septemba 17, mwaka huu, jopo hilo lilionyesha kushangazwa na mvutano huo huku likihoji sababu na matokeo ya mvutano huo.

Jopo hilo lilibainisha kuwa kwa hoja hiyo ingeweza kuangaliwa katika hatua ya usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo (PH) katika Mahakama Kuu ambayo ndiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo  Wakili wa Serikali Mwandamizi (SSA), Faraja Nchimbi aliyekuwa akisaidiana na Wakili Shadrack, alidai kuwa Mahakama Kuu ilikosea katika kutoa uamuzi huo kwa kuwa maombi ya uchunguzi wa umri wa mshtakiwa yaliwasilishwa mahakamani hapo isivyo halali kisheria.

Alidai kuwa hilo limethibitishwa na Jaji mwenyewe, Dk Fauz Twaib  katika uamuzi wake ambapo amekiri kuwa hayakuwasilishwa kihalali mbele yake na kwamba kwa hali hiyo yalipaswa kutupiliwa  mbali.

Wakili Nchimbi alidai kuwa hoja yao nyingine ni kwamba Mahakama Kuu ilikosea katika kutafsiri kifungu cha 44 (1) cha Sheria ya Mahakimu.

Alidai kuwa jaji hakupaswa kusahihisha mwenyewe uamuzi wa Mahakama ya Kisutu bali alipaswa kutoa maelekezo tu ili kosa hilo lisijirudie na siyo kushughulikia yenyewe.

Kwa upande wake mmoja wa mawakili wa utetezi, Peter Kibatala  alidai kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu ulikuwa sahihi na kwamba  lengo la  uchunguzi wa umri halali wa mshtakiwa huyo  lilikuwa ni kulinda maslahi yake kama  mtoto ambayo ni pamoja na aina ya adhabu.

Alidai kuwa hawakuwa na namna nyingine ya kuwasilisha ushahidi wa umri halali wa mshtakiwa huyo na kwamba ilibidi kuwe na namna ya kuweza kuliweka hilo kwenye rekodi (kumbukumbu).

Naye Kiongozi wa Jopo la mawakili wa mshtakiwa, Kennedy Fungamtama  alidai kuwa upande wa mashtaka ulipaswa ukate rufaa na si kuwasilisha maombi ya marejeo.

Kesi hiyo itatajwa katika Mahakama ya Kisutu, Oktoba 8, mwaka huu.

Umri wa mshtakiwa huyo umezua utata baada ya mawakili wanaomtetea  kuomba kesi yake isikilizwe katika Mahakama ya Watoto (Juvenile Court) wakidai kuwa bado ni mtoto.

Mei 7, 2012, mawakili hao waliiomba mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iruhusu kesi hiyo isikilizwa katika Mahakama ya Watoto wakidai kuwa mshtakiwa huyo ni mtoto kwa kuwa  ana umri wa miaka 17 na si 18 kama hati ya mashtaka inavyoonyesha.



Hata hivyo Mahakama hiyo iliyakataa maombi hayo baada ya kupingwa na Wakili Kaganda,  ambaye aliomba wapewe muda zaidi kwa kuwa bado upelelezi ulikuwa ukiendelea na kwamba upelelezi huo unahusisha  suala la umri.

Wakili Kaganda aliongeza kuwa hata jina la mshtakiwa katika cheti cha kuzaliwa kilichotajwa na mawakili wake linasomeka kama  Diana Elizabeth wakati mahakamani mshtakiwa anatambulika kama Elizabeth.

Katika uamuzi wake, Hakimu Mkazi Agustina Mmbando alisema  kwa kuwa kesi hiyo ni ya mauaji na upelelezi haujakamilika, mahakama hiyo haiwezi kuamua hoja yoyote, badala yake aliutaka upande wa utetezi kuwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: