KWA mara nyengine tena Rais Barack Obama ametajwa kumbwaga Mitt Romney
katika mdahalo wa televisheni, ambao licha ya mada yake kuu kuwa siasa,
masuala muhimu kwa wapiga kura, yaani uchumi na ajira, yalitawala
mjadala.
Safari hii, wachambuzi wanasema kwamba mpira ulikuwa unachezwa uwanjani
kwa Rais Obama - siasa za kimataifa - na hivyo alitumia vizuri ujuzi
wake kwenye eneo hilo kuponda kile kinachoonekana kama uelewa mdogo wa
Romney linapohusika suala la siasa za nje.
"Gavana Romney, nimefurahi kwamba unatambua kwamba al-Qaida ni tishio
kwa sababu miezi michache iliyopita ulipoulizwa ni kipi kitisho kikubwa
duniani kwa Marekani, ulisema Urusi, ilhali Vita Baridi vilimalizika
tangu miaka 20 iliyopita.
Linapokuja suala la sera za nje, unaonekana
kurudisha siasa za miaka ya 1980, kama vile ambavyo una sera za kijamii
za mwaka 1950 na za kiuchumi za mwaka 1920.
Unasema hupendelei kuigiza
kilichotokea Iraq, lakini wiki chache zilizopita ulisema unafikiria
tuongeze wanajeshi zaidi nchini Iraq." Obama alimdhihaki Romney.
Pakiwa pamebakia wiki mbili tu kabla ya Siku ya Uchaguzi, Romney
aliutumia mdahalo wa jana kushadidia hoja yake kwamba Obama ameufuja
uchumi wa Marekani.
"Ili tuweze kuendeleza misingi hiyo ya amani, tunahitajika kuwa na
nguvu, na hilo linaanza na uchumi imara hapa kwetu, na bahati mbaya
uchumi si imara kiasi hicho.
Pale rais wa Iraq- samahani- rais wa Iran,
Ahmedinejad, anaposema kwamba deni letu linatufanya tusiwe tena taifa
kubwa, hilo ni jambo la kutisha.
Mkuu wa zamani wa jeshi, Admirali
Mullen, alisema kwamba deni letu ndicho kitisho kikubwa cha usalama wa
taifa. Tumeudhoofisha uchumi wetu." Alisema Romney.
Mchuano mkali
Wagombea urais wa Marekani wakiwakumbatia wake zao baada ya mdahalo wa tatu kati yao.
Wakiwa wanachuana vikali, hakuna hata mmoja kati yao aliyeweza
kumtoa mwenzake nje ya ulingo haraka, wakati wakilumbana kuhusiana na
masuala ya Israel, Iran, Urusi, na ukubwa wa jeshi la Marekani, katika
mdahalo huo uliofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Lynn, Boca Raton.
Matokeo ya uchunguzi wa maoni yaliyotangazwa baada ya mdahalo huo,
yamemuonesha Obama akiongoza, ingawa asilimia 60 ya waliotuma maoni yao
kwenye kituo cha CNN, walisema Gavana Romney ana uwezo wa kuwa amiri
jeshi mkuu wa majeshi, akitimiza jukumu lililowekwa na wasaidizi wake.
CNN imempa Obama asilimia 8 mbele ya Romney.
Kura ya maoni ya kituo cha CBS inaonesha kuwa asilimia 53 ya watu
wanaamini kuwa Obama alishinda mdahalo wa jana, ikilinganishwa na
asilimia 23 ya Romney, huku asilimia 24 wakisema wametoka suluhu.
Kwa kuwa siasa za nje ni kipaumbele cha chini katika kampeni iliyojikita
kwenye uchumi, bado si wazi ikiwa mdahalo huu utakuwa na athari gani
kwenye kinyang'anyiro hicho cha urais.
Wachangiaji maoni kupitia kituo
cha CNN, walionekana kugawika juu ya suala ikiwa mdahalo huo
ungeliathiri kura zao hapo tarehe 6 Novemba.
Hata hivyo, picha hii ya Boca Raton ilikuwa ni moja ya nafasi za mwisho
mwisho kabisa kwa wagombea wote wawili kuwanasihi mamilioni ya wapiga
kura waliokuwa wakiifuatilia kupitia televisheni zao, na ambapo Obama
ametajwa kujidhihirisha mtundu zaidi ya Romney.

0 comments:
Post a Comment