WAASI nchini Syria wanaendelea na mapambano kuiteka kambi ya kijeshi ya
Wadi al-Daif iliyoko karibu na njia kuu ya kutoka kaskazini kuelekea
kusini ambayo ni muhimu kwa waasi hao kudhibiti kabisaa sehemu ya
kaskazini.
Kwa muda wa wiki mbili waasi wameizingira na kuishambulia kambi ya Wadi
al-Daif lililoko mashariki mwa mji wa Maaret al-Numan. Wanasema ukali wa
mashambulizi kutoka kwa vikosi vya serikali unaonyesha ni kwa kiasi
gani kituo hicho ni muhimu kwa mkakati wa kijeshi wa rais Bashar
al-Assad.
Kama kambi hiyo itaangukia mikononi mwa waasi ambao tayari
wanadhibiti mpaka wa kaskazini kuelekea Uturuki, Assad atakuwa
anategemea njia moja tu kutoka bandari ya Latakia katika bahari ya
Mediterranean kwa ajili ya kusafirisha mahitaji muhimu kwa vikosi
vinavyopambana kuurudisha mji muhimu wa Aleppo, ambao ndiyo mkubwa zaidi
nchini Syria.
Raia wa Syria wakitafuta miili ya watu katika vifusi vya jengo lililoharibiwa katika mashambulizi ya ndege za jeshi la Syria.
Afisa wa zamani wa jeshi la Syria aliyejiunga na waasi, Luteni Kanali
Khaled Hamood alisema mapambano ya sasa yalianza siku 11 zilizopita
ambapo walienda kama kundi dogo kuikomboa kambi hiyo lakini
walishangazwa na upinzani ulioonyeshwa na vikosi vya serikali. Aliongeza
kuwa jeshi linapigana kufa na kupona na hawajali kama wanapoteza maelfu
ya wanajeshi ili kuendeleza udhibiti wa kituo hicho.
Mji wa Maaret
al-Numan tayari umeshatekwa na wapinzani hao wa rais Assad, na hivyo
kukata njia kuu ya Aleppo. Lakini bila udhibiti wa kituo hicho cha
karibu cha kijeshi, udhibiti wao wa barabara hiyo hautakuwa na maana.
Hamood alisema anaamini kundi la wanajeshi wapatao 500 wanailinda kambi
ya Wadi al-Daif iliyoko karibu mita 500 kutoka barabara kuu ya kutoka
Damascus kwenda Aleppo, wakisaidiwa na mashambulizi ya angani ambayo
Assad anayatumia dhidi ya waasi na wakaazi wa Maarat al-Numan.
Kambi
hiyo pia inaweza kuwa kituo muhimu cha ugavi wa mafuta ikiaminika kuwa
na lita milioni 5 za mafuta ya taa katika maghala matano chini ya ardhi.
Wanaharakati wanaompinga rais Bashar al-Assad wamesema raia 40 waliuawa
katika mashambulizi ya angani Alhamis iliyopita, katika moja ya
makabiliano makali zaidi ya mgogoro huo.
Wanajeshi wa Jeshi Huru la Syria, FSA wakiwa katika wilaya ya Salaheddin mjini Aleppo.
Baada ya kuzidiwa katika nchi kavu, jeshi la Syria sasa linawapatia
mahitaji wanajeshi waliyoko katika kambi ya Wadi al-Deif kutokea angani
likiangusha mikate na vyakula vingine kutoka katika helikopta.
Lakini
jitihada zake za kuwaongezea vifaa vya kijeshi zimekumbana na upinzani
mkali kutoka kwa waasi waliyoizingira kambi hiyo.
Juhudi za mwisho siku ya Jumapili ziliishia kwa vifaru vinne kuharibiwa
na kuwalaazimu wanajeshi waliobakia kurudi nyuma.
Hamood alisema kama
watafanikiwa kuichukua kambi hiyo, watazidisha juhudi za kuzuia njia ya
kutoka Latakia kwenda Aleppo, ambayo ni njia kuu ya pili ya ugavi kwa
vikosi vya Assad kwenda kaskazini kupitia mji wa Jisr al-Shughour.
Wanasema hii itasaidia kuukomboa kabisaa upande wa kaskazini na
kuelekeza nguvu upande wa kusini mwa Syria.

0 comments:
Post a Comment