RAIS wa Kenya Mwai Kibaki, amekataa kuidhinisha
mipango ya wabunge wa taifa hilo kujipatia kitita kikubwa cha pesa kama
marupurupu ya kuhudumu kama wabunge.
Wabunge hao walipanga kujilipa dola alfu mia moja na kumi kila mmoja kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Lakini bwana Kibaki amesema kuwa hatua hiyo inakiuka katiba na
haiwezi kutekelezwa wakati ambapo walimu pamoja na madaktari nchini
Kenya wamekuwa wakigoma kudai nyongeza ya mishahara.
Waandamanaji waliojawa na ghadhabu nchini Kenya
walijitokeza hapo jana kulaani hatua ya wabunge hao kutaka kujilipa
mamilioni ya pesa kama pesa za ziada wakati bunge litakapofunga vikao
vyake kwa maandalizi ya uchaguzi mwaka ujao.
Waliwataja wabunge hao kama fisi wenye ulafi.
Wabunge wa Kenya ni baadhi ya wale wanaopokea
mishahara mikubwa sana barani Afrika , wakipokea takriban dola elfu
10,000 kama mshahara kila mwezi.
Malipo hayo ya ziada ya dola 110,000 kwa kila
mmoja walitaka yalipwe wakati watakapofunga vikao vyao kwa maandalizi
ya uchaguzi mkuu mwaka 2013.
Wadadisi wanasema kuwa wananchi wangetozwa kodi zaidi ili kugharamia malipo hayo ya dola milioni 23.
Hatua hii imewakasirisha watu wengi, hasa
ikizingatiwa kuwa inakuja baada tu ya migomo katika sekta ya umma ambapo
madaktari, walimu na hata wahadhiri wa vyuo vikuu walisusia kazi
wakidai nyongeza ya mishahara.
Mswaada huo ulipitishwa siku ya Alhamisi ikiwa sehemu ya mabadiliko yaliyofanyiwa mswaada wa fedha bungeni.
Mnamo mwezi Septemba, shule za umma zilifungwa
kwa wiki tatu wakati walimu walipogoma wakidai nyongeza ya mishahara na
huku madaktari nao wakitaka mazingira bora ya kazi.
0 comments:
Post a Comment