DK EMMANUEL NCHIMBI.
SIKU moja baada ya kamati iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya
Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, kutoa ripoti ya uchunguzi wa mauaji ya
mwanahabari, Daudi Mwangosi, huku ikikwama kuweka bayana kiini cha kifo
hicho kutokana na kesi inayoendelea mahakamani, wasomi, wanaharakati,
wanasiasa na wananchi wamepinga hatua hiyo.
Baadhi ya waliozungumza na gazeti hili waliiponda ripoti hiyo ya
Kamati ya Dk. Nchimbi wakidai imeidhalilisha serikali na kuonesha
mkanganyiko uliopo wa kujaribu kuwalinda polisi wanaotuhumiwa kuhusika
na mauaji ya raia.
Wadau hao pia walilisifu Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la
Wahariri (TEF) kutoka ripoti yao iliyojaa kila aina ya ukweli kuwa
Mwangosi aliuawa na polisi kama picha za video na mnato zilizopigwa siku
ya tukio zinavyojieleza wazi.
Wakati kamati ya Dk. Nchimbi katika uchunguzi wake ikidai kuwa nguvu
iliyotumiwa na Jeshi la Polisi kutawanya wafuasi wa CHADEMA haikuwa
sababu ya kifo cha mwanahabari huyo, wadau hao wameiponda wakisema ni
aibu na kwamba hata wajumbe wake walionesha bayana kuwa walikuwa na aibu
ya kuisoma.
Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azavery
Lwaitama, alisema kuwa ripoti hizo mbili ni nzuri kwani kwa mtu mwenye
akili zake timamu anaweza kuona jinsi serikali ya Tanzania ilivyofika
mbali katika mambo ya ajabu.
“Waziri Nchimbi ni bora asingeitoa ripoti hiyo maana inajichanganya
kwa sababu haina maelezo ya kutosha kuhusu kile alichoahidi mapema kuwa
hatua zingechukuliwa baada ya kamati hiyo kumaliza uchunguzi wake,”
alisema.
Alisema ripoti hiyo ni ya kijinga maana inaishia kauli tata za
viongozi wasio na hatia badala ya kutaja bayana kuwa kiini cha mauaji
hayo ni kuwazuia waandishi wa habari wasiwe wanaripoti mikutano ya
CHADEMA na kuwadhibiti CHADEMA wenyewe.
Dk. Lwaitama alibainisha kuwa baada ya Waziri Nchimbi kupokea ripoti
zote mbili, ni bora angekaa kimya na kuchukua hatua zaidi ya kuunda
kamati nyingine ya kuwachunguza polisi.
“Polisi wameumbuka, maana hawakujua kama kuna picha zilikuwa zinapigwa
na ripoti zote zimethibitisha ukweli kuwa lengo lilikuwa ni kuwazuia
waandishi ili kuficha kile ambacho kingetokea kwa CHADEMA pale Nyololo,”
alisisitiza.
Alishauri kuwa Waziri Nchimbi angejijengea heshima kubwa kama
angejiegemeza kwenye ripoti ya MCT, lakini katika kulinda vigogo wa
polisi wasiumbuliwe ndiyo maana ikaandaliwa ripoti ya kuwasafisha.
“Kama si Mwangosi basi angeuawa Dk. Slaa maana hata TBC1 walishaanza
kupotosha kuwa alikuwepo eneo la tukio ili kuhalalisha mambo ya ajabu
ambayo polisi wangeyafanya. Sasa baada ya kuona mlengwa hayupo
wakamgeukia Mwangosi wakielewa kabisa amerekodi mipango yao yote,”
alisema.
Dk. Lwaitama alifafanua kuwa kabla ya Mwangosi kuuawa, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, alinukuliwa akimwambia kuwa
ana kiherehere na askari mwingine akamwambia atakufa.
Alisema picha zinawaonesha watu saba wakimpiga Mwangosi na kisha
kuuawa, lakini mahakamani kafikishwa mmoja tena anafichwa sura na kwamba
Kamanda Kamuhanda bado hajaguswa wakati alishuhudia mpango mzima wa
mauaji.
“Kuhangaika na ripoti ya Nchimbi ni kujipotezea muda, walifanya hivyo
ili baadaye watoe sababu za kijinga za kupigwa na kitu chenye ncha kali,
lakini picha zikawaumbua. Kama hawakuwa tayari kuyasema yaliyomo
wangekaa na ripoti yao,” alisema.
Naye mwanaharakati Deus Kibamba, aliliambia gazeti hili kuwa ameisoma
ripoti ya MCT, lakini ya Waziri Nchimbi hakuhangaika nayo kwani
waliipinga tangu mwanzo wakijua si halali kisheria.
Alisema kuwa Waziri Nchimbi alikuwa mtuhumiwa katika tukio hilo, na
hivyo hakuwa na mamlaka kisheria kuunda kamati hiyo na kuongeza kuwa
wajumbe wa kamati hiyo licha ya kuheshimika sana kwenye jamii, lakini
kwa ripoti hiyo wamejitia doa kubwa.
“Watu wanakubali uteuzi kwenye tume na kamati hizo bila kuhoji maana
wanatafuta maslahi kifedha. Kisheria Nchimbi hakupaswa kuunda kamati
hiyo na hata MCT wao waliiunda kamati ya kimaadili si kisheria ndiyo
maana tunaisifu ya kwao.
Tulishasema tunahitaji tume ya kimahakama
kuchunguza matukio haya wakatupinga,” alisema.
Alisema kuwa Jeshi la Polisi walikwishaonesha kupishana kwa kauli
kutokana na tukio hilo, kwamba Waziri Nchimbi alisema hawatamshtaki mtu
hadi kamati imalize kazi, lakini wakati ikiendelea askari mmoja
alifikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Mtatiro Julius, alisema
kuwa Nchimbi aliunda kamati ya kuendelea kujilinda yeye, serikali na
CCM kwani kusema polisi hawakutumia nguvu kumuua Mwangosi si kweli.
“Mimi ukiachilia ripoti hizo nimetazama video ya mauaji hayo na
inaonesha wazi kabisa kuwa polisi walimuua Mwangosi kwa makusudi kwa
kutumia nguvu nyingi ambazo hazikuwa na sababu,” alisema.
Aliongeza kuwa ripoti ya Kamati ya Nchimbi ni ya kupikwa, kuwalinda
polisi kwani hata kumshtaki askari mmoja ni mkakati wa kukwepa wengine
wasijekutajwa wakawajibishwa.
Naye Katibu Mkuu wa chama kipya cha ADC, Limbu Kadawi, alisema kwa
ujumla ripoti hiyo ni aibu kwa taifa na Nchimbi mwenyewe, kwamba hata
Jaji Ihema wakati anaisoma alikuwa akiona aibu.
Alisema wakati umefika kwa wananchi kujifunza kukasirika wanapoletewa mambo ya kijinga na aibu kama hayo.
Kidawi alifafanua kuwa, hata waandishi walianza kugawanyika mapema
tangu tukio hilo kutokea kwani katika maandamano yao pale Jangwani,
baadhi walionekana kujikomba kwa Waziri Nchimbi wakati ndiye alikuwa
akilaaniwa kwa askari wake kuua.
“Mauji ya Mwangosi yalikuwa wazi wala hayakuhitaji kamati hiyo
kuchunguza maana askari wote walioonekana kwenye picha pamoja na kamanda
wao Kamuhanda walipaswa kuwa wamekamatwa na kushtakiwa.
0 comments:
Post a Comment