MADAI YA RUSHWA YATAWALA, MALISA, SHIGELLA, BASHE, NYALANDU WATUHUMIWA, MAKONDA ATOA KAULI NZITO.
Mjumbe
wa
Kamati Kuu ya CCM, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Sheni akimpongeza,
Khamis Sadifa Juma baada ya kutangazwa kuwa Mwenyekiti Mpya wa Umoja wa
Vijana wa CCM UVCCM, mjini Dodoma baada ya kumalizika kwa kazi ya
kuhesabu kura.
Neville Meena, Dodoma.
MATOKEO
ya uchaguzi wa Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM)
yametangazwa jana huku kukiwa na harakati za kuyapinga kwa madai ya
ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.
Kati ya mambo
yaliyotajwa kupindisha taratibu za uchaguzi huo uliofanyika juzi ni kile
kilichoelezwa kuwa ni kutawaliwa na vitendo vya rushwa.
Baada
ya Msimamizi wa uchaguzi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi kutangaza matokeo, baadhi ya
vijana waliyapinga na kuanza kukusanya saini 340 ili kuyapinga.
Katika
kuonyesha kutoridhishwa na mchakato mzima wa uchaguzi, baadhi ya
wajumbe walibeba mabango yenye ujumbe wa kutokubaliana na matokeo, mbele
ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali
Mohamed Shein baada ya kumaliza kufunga mkutano huo.
Moja
ya bango hilo lilikuwa na maneno: “Jumuiya si ya Lowassa na wafuasi
wake (Benno, Bashe, Zungu, Zabein…..) hivyo jumuiya itakuwa na kambi
mbili ya kwanza jukwaani na kambi ya mezani.”
Bango jingine lilisomeka: “Jumuiya imara hujengwa na uchaguzi wa haki na siyo rushwa za Bashe, Benno na Zungu.”
Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ni miongoni mwa makada wa CCM wanaotajwa
kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kambi yake imekuwa
ikitajwa kuwa na ushawishi mkubwa katika uchaguzi wa ndani wa CCM.
Kwa
tafsiri ya mabango hayo, Benno (Malisa) alikuwa Kaimu Mwenyekiti wa
UVCCM aliyemaliza muda wake, Bashe (Hussein) naye alikuwa ni Mjumbe wa
Baraza Kuu la jumuiya hiyo ambaye amemaliza muda wake.
Maofisa
usalama na walinzi wa jumuiya hiyo ambao walikuwa wakijaribu
kuwanyang’anya vijana hao mabango walishindwa, hivyo kulazimika kusubiri
dakika kama tano hivi hadi msafara wa Dk Shein ulipoondoka walipowatoa
nje ya eneo la ukumbi wa mkutano.
Tukio hilo lilizua
tafrani baada ya walinzi hao kuwanyanyua juujuu vijana wawili kati ya
sita waliokuwa na mabango, huku wengine wakionekana kutaka kuwapiga
lakini polisi waliingilia kati na kuwatoa nje.
Baadaye
polisi waliondoka na vijana watatu katika tukio ambalo lilikuwa
likifuatiliwa kwa karibu na baadhi ya wagombea ambao walishindwa katika
nafasi mbalimbali za uongozi wa UVCCM.
Mjumbewa
Kamati Kuu ya CCM, ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed
Shein, (Kulia), akishuhudia wakati Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa
Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, (CCM), aliyemaliza muda wake, Benno
Malisa, (Wapili kushoto), akimpongeza mwenyekiti mpya wa jumuiya hiyo
aliyechaguliwa kwenye mkutano mkuu uliofanyika jana Jumanne mjini
Dodoma, Khamis Sadifa Juma.
Vijana walalama.
Mapema
jana asubuhi, kundi la vijana kutoka mikoa mbalimbali walikutana na
waandishi wa habari na kulalamika kwamba rushwa ilitawala huku
wakiwatuhumu viongozi wa UVCCM na baadhi ya makada wa chama hicho kwa
kuhusika na vitendo hivyo.
Waliotajwa ni pamoja Malisa, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela, Bashe na mtoto wa Lowassa, Fredy.
“Kama
Rais Jakaya Kikwete kweli yuko makini na kauli zake ni za dhati, basi
atengue matokeo ya uchaguzi huu maana kanuni zimekiukwa na kusema kweli
rushwa ilitawala.
Atumie nafasi yake kurejesha hadhi ya chama, huu
uchaguzi ni batili,” alisema Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kutoka
Morogoro, Augustine Matefu.
Walidai kuwa Bashe ndiye
aliyekuwa mratibu wa uingizaji wa fedha katika eneo la mkutano ambazo
zilitumika kugawanywa kwa wajumbe na kwamba Malisa na Shigela waligawa
Sh1 milioni kwa viongozi wa mikoa kama hatua ya kumpigia kampeni mmoja
wa wagombea walioshinda.
Kada mwingine, Livamba Adinan
Selemani alisema: “Vijana kweli tumempuuza Rais, kweli mtu ambaye hana
hela hawezi kupata uongozi UVCCM, kwa maana nyingine nchi yetu inakwenda
pabaya. Watu wachache wenye fedha wanaweza kuamua kufanya wanachotaka,
hivyo ndivyo uchaguzi wetu wa vijana ulivyokuwa.”
Mjumbe
mwingine, Kichanta Selemani alisema malalamiko ya viongozi wa UVCCM
kuwapendelea baadhi ya wagombea yalifikishwa kwa Lukuvi lakini hakuna
hatua zilizochukuliwa.
Wakati makada hao wa CCM
wakizungumza na waandishi wa habari, lilitokea kundi jingine la makada
wa chama hicho ambao walianza kuzozana na wenzao wakisema kuwa
malalamiko yao yanatokana na kushindwa na kwamba walitaka kutumia:
“Viongozi wa ngazi za juu za CCM” kuwachagulia vijana viongozi.
Kundi
hilo la pili lilidai kuwa katika uchaguzi huo kundi hilo la kwanza
ndilo lililohonga fedha na kumtaja Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,
Lazaro Nyalandu kwamba alikuwa akiwashawishi wajumbe kwa fedha kumchagua
mmoja wa wagombea.
Akizungumzia tuhuma hizo, Nyalandu
alisema kupitia ujumbe wa simu yake ya mkononi:
“Mimi siyo mjumbe wala
mgombea na wala sihusiki kwa lolote.
Nilikwenda ukumbini na waziri
mwenzangu na baadaye tukaondoka pamoja. Hao ni waongo wakubwa na wazushi
wachache wanaonunua haki.”
Hakuna mtu yeyote
niliyeongea naye wala kutoa hela yoyote kwa sababu zozote zile na
tulikuwa ukumbini baadaye nje wote pamoja (na waziri). Shame to them who
lie (aibu kwao wanaosema uongo) na wataje majina yao tuyasikie.”
Alimtaja
Waziri aliyekuwa naye kuwa ni Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles
Tzeba kwa lengo la kuwasalimia vijana ambao walikuwa wakiendelea na
mkutano wa uchaguzi.
Watuhumiwa wanena
Kwa
nyakati tofauti, wakijibu tuhuma hizo watuhumiwa wote walikanusha
kuhusika kutoa rushwa na kuwataka wanaolalamika kupeleka ushahidi wao
Takukuru na kufikisha malalamiko hayo katika vikao vya ulinzi na maadili
vya CCM.
Shigela kwa upande wake, akizungumza na
waandishi wa habari alisema kinachotokea sasa kuhusu tuhuma hizo
kilitarajiwa kwani ni kawaida watu wanaposhindwa katika uchaguzi kutoa
malalamiko hata kama hawana ushahidi wa tuhuma husika.
Shigela
alikanusha yeye na Malisa kutoa fedha kwa viongozi wa mikoa akisema kwa
nafasi yake asingeweza kupata fursa ya kufanya hivyo kwani alikuwa
mratibu mkuu wa uchaguzi kuhakikisha kila jambo linakwenda sawa.
“Kama
kuna watu hawakuridhika kuna taratibu za chama inabidi zifuatwe, kwa
mujibu wa taratibu zetu kuna siku 14 za malalamiko na hizo mtu anaweza
kuzitumia kuandika malalamiko yake na yapelekwe kwa viongozi wahusika
ili wachuke hatua,” alisema Shigela na kuongeza:
“Vinginevyo
taratibu za chama haziruhusu kutoa au kupokea rushwa kwa namna yeyote,
kwa hiyo kama mtu anadhani ana uwezo aitumikie jumuiya popote pale alipo
kwa sababu wote hatuwezi kuwa viongozi kwa pamoja.”
Kwa
upande wake, Malisa alisema: “Nimefanya kazi yangu na kutekeleza wajibu
wangu kwa ukamilifu, kama kuna jambo lolote ambalo linahusu UVCCM, basi
kamuulizeni mwenyekiti wa jumuiya maana yupo.”
Bashe
alikanusha kuhusika na vitendo vya rushwa na kuwataka wanaotoa madai
hayo, kama wana ushahidi waupeleke Takukuru au kufikisha suala hilo
katika vikao vya chama hicho.
“Waambieni kwamba
wasilete siasa za shule za sekondari UVCCM, maana kama wangeshinda ni
dhahiri kwamba wasingelalamika.
Ninawapa ushauri wa bure, kwanza kama
wana ushahidi wa madai hayo kwamba mimi Hussein nimetoa rushwa, basi
wapeleke ushahidi wao Takukuru lakini pia ndani ya chama tunayo Kamati
ya Maadili na Usalama wapeleke malalamiko yao huko ili yafanyiwe kazi.”
Alisema hawezi kujihusisha na rushwa kwani hata Rais Kikwete katika hotuba ya ufunguzi alikemea vitendo hivyo.
Fredy
akizungumza kwa simu alisema:
“Tuhuma hizo siyo za kweli kwani mimi
licha ya kwamba nilipata barua ya mwaliko wa kuhudhuria mkutano huo
sikuenda Dodoma kutokana na kubanwa na kazi.
“Kwanza
mimi si mjumbe wa mkutano mkuu japokuwa ni Katibu wa Uhamasishaji wa
Mkoa wa Arusha. Nilipata mwaliko lakini sikuweza kufika huko (Dodoma)
nimetingwa na kazi nyingi,” alisema.
Matokeo ya uchaguzi
Lukuvi alimtangaza Mbunge wa Donge, Sadifa Juma Khamisi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM baada ya kupata kura 483.
Sadifa
alimshinda Rashid Simai Msaraka aliyepata kura 263, wakati mgombea
mwingine Lulu Msham Abdallah licha ya kujitoa katika kinyang’anyiro
hicho muda mfupi kabla ya kura kupigwa, alipata kura nane.
Katika
nafasi ya Makamu Mwenyekiti Mboni Muhita alishinda katika duru ya pili
baada ya kupata kura 489 na kumshinda, Paul Makonda aliyepata kura 241.
Katika
duru ya kwanza, Mboni alikuwa amepata kura 361 na Makonda kura 206,
huku mgombea mwingine Ally Salum Hapi akipata kura 179.
Uchaguzi huo
ulirudiwa baada ya wagombea wote kutofikisha nusu ya kura kama kanuni
zinavyotaka.
“Sheria kushindwa kwa heshima kuliko kushinda kwa fedheha.”
Makonda
aliyekuwa akizungumza kwa hisia jukwaani alisema ikiwa UVCCM wanataka
kujenga taasisi yenye nguvu na inayoaminika, lazima wahakikishe
wanajiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vinaua demokrasia.
“Uchaguzi
tulioufanya hatukumchagua Sadifa wala Mboni, bali tumechagua uongozi wa
aina ya jumuiya tunayoitaka, sasa tutarajie jumuiya hiyo…. kama
sikueleweka historia itakuja kutuambia maana ya maneno haya,” alisema
Makonda na kuongeza:
“Kama kuna mtoto wa maskini,
mtoto wa mkulima kama mimi amechagua au kupiga kura yake kwa sababu ya
rushwa, basi ajue amepanda mbegu maishani mwake.”
Baada
ya Makonda kutoa kauli hizo alishuka jukwaani na kwenda moja kwa moja
nje ya ukumbi ambako baadhi ya wapambe wake walimfuata na kuanza kulia
machozi.
Baadhi yao walisikika wakisema kwamba UVCCM
wameisaliti demokrasia kutokana na nguvu ya fedha. Hata hivyo, Makonda
alikuwa akiwafariji kwa kuwaambia wasife moyo.

0 comments:
Post a Comment