Kiungo wa Azam, Himid Mao (kushoto) akijaribu kumtoka beki wa JKT Oljoro, Omar David katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliozikutanisha timu hizo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi. Azam ilishinda 1-0.Picha na Michael Matemanga.
AZAM wameiporomosha Simba hadi nafasi ya tatu baada ya kuichapa Oljoro JKT bao 1-0 huku Azam pia ikiwafungia wachezaji wake Deogratius Munishi na mabeki Said Morad na Erasto Nyoni.
Wawakilishi hao wa Kombe la Shirikisho Afrika mwakani, Azam sasa wamepanda hadi nafasi ya pili wakiwa na pointi 24, moja zaidi ya Simba (23), wakiachwa na vinara Yanga (26) kwa pointi mbili.
Mabingwa wa mwaka 1988, Coastal Union wameisogelea Simba wakiwa na pointi 22 baada ya kuichapa Polisi Morogoro kwa bao 1-0, nayo Mtibwa Sugar ilipata ushindi kama huo dhidi ya JKT Ruvu.
Katika mechi ya Azam na Oljoro, mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Kipre Tchetche aliifungia Azam bao pekee katika dakika ya nne kwa mkwaju wa penalti baada ya beki wa JKT Oljoro, Yasin Juma kushika mpira kwenye eneo la hatari.
Azam waliendelea kulisakama lango la Oljoro, lakini washambuliaji wake Tchetche na John Bocco walikosa umakini kwenye umaliziaji katika dakika 20 na 25 wakiwa wao na kipa Musa Lucheke.
Oljoro walijibu mapigo katika dakika ya 47 kupitia kwa mshambuliaji wake Esau Issa, lakini shuti lake lilitoka nje.
Katika mchezo huo timu zote zilicheza soka ya kiwango cha chini tofauti na ilivyotegemewa na mashabiki waliojitokea kushuhudia pambano hilo.
Pia katika mechi hiyo Azam walipata pigo katika dakika ya 87 baada ya kiungo wake Himid Mao kupewa kadi nyekundu ya moja kwa moja na mwamuzi baada ya kumpiga kichwa Amir Omary wa Oljoro.
Azam yafungia watatu
Katika hali isiyo kuwa ya kawaida, jana klabu ya Azam imethibitisha kuwafungia wachezaji wake watatu kipa wake, Munishi (Dida) na mabeki Morad na Nyoni kwa tuhuma za kupokea hongo kwenye michezo Azam waliyocheza na Simba na Yanga.
Azam wamepoteza mechi mbili msimu huu baada ya kufungwa na Simba 3-1 na kusababisha wamtimue kocha wao kabla ya kunyukwa na Yanga 2-0 Jumapili iliyopita.
Kocha wa Azam, Stewart Hall alithibitisha kufungiwa kwa nyota hao watatu kwa tuhuma za kupokea hongo kwenye mechi hizo mbili.
"Ni kweli tumewafungia Munishi, Morad na Nyoni," alisema kwa kifupi kocha Hall.
Mapema chanzo chetu kilitualifu kuwa wachezaji Munishi na Morad walidaiwa kuchukua fedha kwenye mchezo dhidi ya Simba na Yanga, huku Nyoni naye akisemekana kuwa alichukua fedha katika mechi dhidi ya Yanga ingawa hakucheza."
"Munishi hakucheza dhidi ya Yanga, lakini alitumika kugawa fedha kwa baadhi ya wachezaji ili kuhujumu," kilidai chanzo hicho.
Tanga; Katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Mkwakwani, wenyeji Coastal Union wamejiweka vizuri kwenye msimamo wa ligi baada ya mshambuliaji wake Daniel Lyanga kuwafungia bao pekee katika dakika ya 15, akimalizia kazi nzuri ya Kassim Selembe na kuichapa Polisi Morogoro 1-0.
Nao mabingwa wa 2000, Mtibwa Sugar walipata ushindi wao wa pili mfululizo baada ya kuichapa Ruvu JKT bao1-0 kwenye Uwanja wa Manungu huku bao hilo likifungwa na beki Issa Rashid katika dakika ya 22 kwa shuti la mbali.
Imeandaliwa na Kalunde Jamal, Doris Maliyaga na Burhan Yakub,Tanga.


0 comments:
Post a Comment