BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MHARIRI FRANK SANGA AHIMIZA UANDISHI WA HABARI VIJIJINI


WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kuandika habari nyingi za vijijini, ili kuibua changamoto zinazoikabili jamii inayowazunguka na kubainisha mafanikio yanayopatikana ili kuchochea maendeleo ya maeneo hayo.

Hayo yalisemwa na Mhariri  Mtendaji wa Gazeti la Mwanaspoti linalochapishwa na Kampuni ya Mwananchi Communicatios Ltd (MCL), Frank Sanga kwenye mafunzo ya waandishi wa mkoa huo yaliyondaliwa na Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).



Sanga alisema waandishi wengi wa habari nchini wana tabia ya kuandika kwa wingi habari za viongozi pamoja na watu maarufu na kuacha kuandika habari za vijijini ambazo zinachangia kutoa manufaa makubwa kwa jamii ya vijijini.


Alisema Watanzania wengi wanaishi vijijini hivyo kupitia kalamu za waandishi wa habari wataweza kunufaika kwa viongozi kutambua mahitaji yao tofauti na sasa kwani viongozi wao wa kuchaguliwa wamekimbilia mijini.


“Hivi sasa habari nyingi zinazoonekana kwenye runinga na kwenye magazeti pamoja na kusikika kwenye redio ni zile za mijini tu semina, viongozi na watu maarufu lakini zile za vijijini haziandikwi sana labda zile mbaya,” alisema Sanga.


Aliwataka waandishi wa habari wa Mkoa wa Manyara kupitia mafunzo hayo wabadilike kwani kupitia kalamu zao mkoa wa Manyara utaweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo baada ya miaka mitano.


Naye Katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari wa Mkoa wa Manyara(MAMEC) Zacharia Mtigandi alisema japokuwa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa usafiri ili waweze kufika vijijini watajitahidi kubadilika.


“Kupitia mafunzo haya kwa namna moja au nyingine tutaweza kubadilika kwa kiasi kikubwa kwani jamii iliyopo vijiji inahitaji mchango mkubwa kwetu ili waweze kunufaika kwa mambo mbalimbali,” alisema Mtigandi.  


Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Mamec, Mary Margwe alisema jamii nyingi bado hazijajua manufaa ya uwepo wa waandishi wa habari na baadhi yao wanataka waone manufaa ya kuandikwa hapo hapo.


“Unakuta mtu ameteseka polisi hadi mahakamani na wajanja wachache wamemla fedha zake, akishaishiwa anakufuata uandike habari zake na kesho yake anakulalamikia mbona umeandika lakini haki sijapata,” alisema Margwe.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: