
Rais wa Marekani Barrack Obama, mkewe Michelle na binti zake Sasha (kushoto) na Maria (kulia) akiwapungia mashabiki wake usiku wa Uchaguzi jijini Chicago jana baada ya kumwagusha mpinzani wake Mitt Romney.Picha na Jewel Samad, AFP
WASHINGTON, Marekani.
RAIS Barack Obama jana alitangazwa kuwa mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa Marekani uliomalizika usiku wa kuamkia jana. Matokeo hayo yamemfanya kuwa Rais wa kwanza wa nchi hiyo kutetea kiti hicho licha ya rekodi mbaya ya uchumi na ukosefu mkubwa wa ajira.
Hakuna Rais aliyewahi kupata muhula wa pili Marekani tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kukiwa na ukosefu wa ajira wa zaidi ya asilimia 7.2.
Mbali ya rekodi hiyo, Obama ameweka rekodi nyingine ya kuwa Rais wa pili wa Marekani kutoka chama cha Democrat kutetea kiti hicho tangu Vita hiyo Kuu ya Pili ya Dunia akitanguliwa na Bill Clinton.
Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Romney alitoa hotuba ya kukubali kushindwa na kuwapongeza wafuasi wake kwa kumuunga mkono. Pia alimpongeza na kumtakia kila la heri Obama katika muhula wake wa pili wa utawala.
Licha ya kuibuka na ushindi mnono, matokeo ya awali yalionyesha kuwapo kwa mchuano mkali baina ya wagombea hao wawili kabla ya upepo kubadilika kuelekea upande wa Obama.
Rais huyo wa kwanza mwenye asili ya Afrika kuliongoza taifa kubwa zaidi duniani alitangazwa mshindi baada ya kupata Kura za Majimbo (Electoral College Votes) 303 huku mpinzani wake akipata 270.
Hata hivyo, Romney alishinda kura za umma (popular votes) kwa asilimia 50 lakini mfumo wa Marekani unazingatia zaidi ushindi wa kura za majimbo.
Clinton ni miongoni mwa watu waliofurahia ushindi huo. Rais huyo wa zamani wa Marekani, alikaukiwa sauti katika harakati za kampeni kuhakikisha Obama anarejea katika Ikulu ya White House.
“Nimeitoa sauti yangu kwa ajili ya Rais wangu,” alisema Clinton alipokuwa akihutubia zaidi ya watu 24,000 waliofurika kushangilia ushindi huo huko Virginia.
Kwa ushindi huo, Rais Obama ataapishwa Januari 20, mwakani kwa mujibu wa Katiba ya Marekani lakini kwa kuwa itakuwa ni Jumapili, shughuli hiyo itafanywa kwa faragha na kesho yake, Jumatatu ataapishwa katika sherehe ya kitaifa.
Matokeo yalianza kwa kutangazwa ushindi wa Rais Obama katika Jimbo la Vermont, yakifuatia ya Majimbo ya Delaware, Maryland, Michigan, Pennyslivania, Wisconsin na New Hampshire.
Romney alishinda katika majimbo yanayofahamika kuegemea upande wa chama chake cha Republican, ikiwa ni pamoja na Kentucky, Tennesee, South Carolina, West Virginia na Indiana.
Obama alishinda pia New Jersey ambapo wakati wa kimbunga cha Sandy alilitembelea jimbo hilo na kupongezwa na Gavana wake ambaye anatokea Republican.
Akihutubia baada ya ushindi huo, Obama aliwapongeza na kuwashukuru wafuasi wake na kuahidi kushirikiana na wananchi pamoja na wanasiasa kutatua matatizo ya Marekani huku akiwahakikishia Wamarekani kwamba ataiacha Ikulu katika hali nzuri ikiwamo kuongeza idadi ya ajira ikiwa ni sehemu ya kukuza uchumi.
Karata iliyompa ushindi.
Wakati masuala ya kudorora kwa uchumi na ukosefu wa ajira yakiwavutia zaidi waliompigia kura Romney, suala lililowavutia wapiga kura wafuasi wa Obama ni pamoja na bima ya afya.
Hata katika suala la uchumi, wengi wanaamini kuwa hatua za kurekebisha uchumi zimeanza kuzaa matunda huku wakihofia kwamba endapo Romney angeshinda, angewapendelea zaidi matajiri.
Ushindi kwa muhula wa pili wa Obama, una maana kwamba sasa mamilioni ya Wamarekani wanaweza kupata bima ya afya na halitakuwa jambo la kuwaumiza kifedha tofauti na msimamo wa Romney ambaye alisema kwamba angeachana na mpango huo.
Mbali ya karata hiyo kumpa ushindi, Obama pia alikonga nyoyo za kinamama hasa katika masuala ya kisheria kama kuhakikisha wanawake wanapata mishahara sawa na wanaume na pia suala la mashoga kutumika jeshini akichukuliwa kuwa Rais anayefuata sera za kibinadamu, tofauti na msimamo wa Republican.
Chereko ‘Kijijini kwao Kenya’
Jana katika Kijiji cha Kogelo, Kisumu - Kenya, alikozaliwa baba mzazi wa Rais Obama, Hussein, kulikuwa na shamrashamra huku ikielezwa kwamba bibi yake, Sarah Obama atahudhuria hafla ya kuapishwa rasmi kwa mjukuu wake Januari mwakani.
“Ingawa ni lazima nishukuru Wamarekani kwa matokeo haya, ushindi ni kwa Afrika kwani tumedumishwa katika uongozi kimataifa,” alisema Sarah.
Alitoa wito kwa Obama kuhakikisha anatimiza ahadi alizotoa ili Wamarekani wazidi kumwamini.
“Wana Kogelo hawajapata usingizi kwa siku tatu sasa, huku wakitaka kuhakikisha ‘mwana wao’ ameshinda uchaguzi huo ambao ushindani wake ulikuwa ‘sako kwa bako’ (mkali).”
Miaka minne iliyopita, ilikuwa ni vigumu kufika Kogelo kutokana na barabara kuwa mbaya lakini sasa hali imebadilika kwani zimejengwa upya pamoja na kupata huduma ya umeme baada ya Serikali kukifanya kijiji hicho kuwa eneo la kitalii.
Wanahabari wa kimataifa walijaa Kogelo tangu wiki iliyopita kujulisha ulimwengu kilichokuwa kinatokea.
Jana, mvua ilitishia kuharibu shamrashamra za kutazama shughuli za upigaji kura kwenye runinga kubwa iliyowekwa katika uwanja ulio nyuma ya Hoteli ya kifahari ya Kogelo Village Resort. Hata hivyo, mmiliki wa hoteli hiyo, Nicholas Rajula alilazimika kuihamishia ndani na kutoa fursa kwa wanakijiji hao wake kwa waume na hata watoto kupata uhondo. Mama Sarah na jamaa zake wengine walikuwa wakitazama matokeo hayo nyumbani kwao.
Matokeo yalipoanza kuonyeshwa, Obama akimshinda Romney mwendo wa saa 12, vifijo vilianza na vikaongezeka zaidi wakati CNN ilipobashiri ushindi kwa Obama.
Ilipotimia saa 1.30, hapakuwa na yeyote hotelini kwani wote walikimbia nje kusherehekea huku wakiimba nyimbo za kumpongeza Obama.
Hata hivyo, sherehe za mwaka huu hazikufana kama ilivyokuwa 2008, hali ambayo wanakijiji wanasema imetokana na matumaini makuu ambayo hayakutimizwa.
Wakazi hao, pamoja na Mama Sarah wanaamini kuwa awamu hii ya pili imetoa nafasi bora kwa Obama kuzuru Kogelo.
Baba mdogo wa Rais Obama, Said Obama alisema mkesha huo utahitimishwa kwa sherehe kubwa itakayojumuishwa kuchinjwa kwa mifugo mingi kama shukrani kwa Mungu.
Mwanamuziki wa mtindo wa Ohangla, Othieno Aloka ambaye pia ni mkazi wa eneo hilo, aliwaburudisha wakazi hao na kusaidia katika kuwaepushia usingizi.
Ubalozi wa Marekani wakesha
Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam uliandaa hafla maalumu ya kufuatilia matokeo ya uchaguzi wa Marekani iliyohudhuriwa na zaidi ya waalikwa 200 wakiwamo viongozi na maofisa wa Serikali ya Tanzania, mabalozi wa nchi mbalimbali, waandishi wa habari, wawakilishi wa taasisi huru za kiraia na Wamarekani wanaoishi Tanzania.
Katika hotuba yake baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Balozi Alfonso Lenhardt alisema mshindi ametangazwa baada ya kampeni kali zilizoshuhudia wagombea wa urais kutembelea nchi nzima na kufanya midahalo mitatu na mdahalo mmoja wa wagombea wenza.
Balozi Lenhardt alisema kuwa bila kujali matokeo ya uchaguzi huo, Marekani itaendelea kuisaidia Tanzania.
“Maajabu na uzuri wa demokrasia hujidhihirisha katika nyakati kama hizi.
Mojawapo kati ya mafunzo muhimu tunayoweza kuyapata ni kwamba iwe Marekani, Tanzania au nchi yoyote ile, hapawezi kuwa na demokrasia ya kweli bila ya wagombea na wananchi kukubali kwa amani kuwa wameshinda au wameshindwa, kuweka dhamira ya kuendelea kushindana tena na kuheshimiana bila kujali tofauti za kisiasa.
“Ni lazima wananchi waheshimu matokeo ya uchaguzi uliofanyika kwa haki, uwazi na kwa njia za kidemokrasia. Msingi huu umeshuhudiwa hivi leo katika uchaguzi wa Marekani,” alisema Balozi.
Salamu za pongezi.
Viongozi wa mataifa mbalimbali wamekuwa wakituma salamu zao za pongezi tangu kutangazwa kwa matokeo hayo. Katika taarifa yake, Umoja wa Ulaya (EU), umesema ushindi huo wa Obama utaongeza uhusiano wao na Marekani.
Viongozi wa EU, Herman Van Rompuy na Jose Manuel Barrosso walisema Marekani ni mshirika muhimu kimkakati na umoja huo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Kujihami wa Nchi za Magharibi (Nato), Anders Fogh Rasmussen alisema Obama ameonyesha uongozi bora katika masuala ya umoja huo.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amempongeza kiongozi huyo kwa kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo na pia kupambana na mgogoro wa kiuchumi duniani.
Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas pia amempongeza Rais Obama huku akimtaka kuendeleza juhudi za amani katika Mashariki ya Kati.
Rekodi nyingine
Obama amevunja rekodi nyingine ya taarifa ya ushindi wake kusambazwa kwa watu wengi zaidi kwa kipindi kifupi katika historia ya masuala ya kisiasa ya Marekani.
Katika mtandao wa Twitter, zaidi ya watu milioni 20 wali-twiti katika mtandao huo siku ya uchaguzi baada ya Obama kuweka picha akiwa amemkumbatia mkewe mara baada ya ushindi.
Mtandao wa Twitter umetangaza kuwa baada ya kuwekwa picha hiyo kwenye mtandao huo, imevunja rekodi ya wanachama wake kusambaziana mara nyingi kitu ambacho hakijawahi kutokea.
Baadhi ya watu maarufu waliosambaziana picha hiyo ni mwanamuziki Mariah Carey ambaye alisema: “Hotuba nzuri, naiangalia nikiwa na watu ninaowapenda na wote tumefurahia. Asante sana Wamarekani kwa miaka mingine minne ya Rais Obama.”
Mwigizaji, Eva Longoria alisema: “Hotuba bora kutoka kwa Barack Obama, amechaguliwa kwa awamu ya pili.”
Mke wa Obama, Michelle Obama alisema: “Ni zaidi ya kitu chochote, nataka niwashukuru kwa kila kitu. Nina furaha kwa kutuunga mkono na sala zenu.”
Obama aliwashukuru waliompongeza katika mtandao huo na ule wa Facebook akisema: “Haya yametokea kwa sababu yenu... Ahsanteni.”

0 comments:
Post a Comment