
WAASI wa M23 wametangaza kuanzisha mazungumzo na rais wa jamhuri ya
kidemokrasi ya Congo Joseph Kabila,saa chache baada ya mkutano wa kimkoa
kulitaka kundi hilo kusitisha mashambulizi yake mashariki mwa nchi
hiyo.
Wakipata ushindi mdogo kwa viongozi hao wa kimkoa, kiongozi wa kisiasa
wa kundi hilo la waasi wa mashariki ya jamhuri ya Congo Jean -Marie
Runiga Lugerero , amesema kuwa alikuwa na mazungumzo ya awali na Kabila
baada ya mkutano huo uliofanyika mjini Kampala kumalizika.
Wakati hakualikwa binafsi katika mkutano huo , Runiga Lugerero
aliliambia shirika la habari la AFP kuwa alifanikiwa kukutana na Kabila
kwa kupitia upatanishi wa rais wa Uganda Yoweri Museveni, ambae
alitarajiwa kufanya nae mazungumzo hii leo Jumapili(25.11.2012).
Viongozi wa Afrika wakikutana mjini Kampala, rais Kabila (kulia) na Museveni (katikati).
"Hali ilikuwa tete lakini baadaye , kila upande ulipunguza jazba katika
majadiliano kwasababu haya si matatizo ya kibinafsi , lakini ni matatizo
ya nchi" ambayo inapaswa kupatiwa ufumbuzi, ameliambia shirika la
habari la AFP kwa simu.
"Nafikiri mkutano huo ulikwenda vizuri sana".
Runiga Lugerero na Kabila watakutana tena leo Jumapili(25.11.2012)
kujadiliana juu ya vipi mazungumzo yao yatakavyoendelea, ameongeza.
"Ndio walikutana," Waziri wa mambo ya kigeni wa jamhuri ya kidemokrasi
ya Congo Raymond Tshibanda ameliambia shirika hilo la habari.
Lakini
amekanusha kuwa mazungumzo zaidi ya ana kwa ana kati ya Kabila na kundi
la M23 yanatarajiwa.
Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Tangazo la Runiga Lugerero limekuja siku chache baada ya Kabila
kuonekana kuondoa uwezekano wa mazungumzo na majeshi hayo ya waasi.
Na saa chache hapo kabla , katika tamko lao la kufunga kikao , viongozi
wa kimkoa wametoa wito kwa wapiganaji wa kundi la M23 kusitisha mapigano
na kuondoa majeshi yao katika mji muhimu wa mashariki wa Goma katika
muda wa saa 48.
Runiga Lugerero , hata hivyo , ameweka wazi kuwa hatua yoyote ya kuondoa
majeshi itakuja pale tu baada ya mazungumzo kati ya kundi hilo la waasi
na Kabila.
Wapiganaji wa M23 watalinda maeneo yao iwapo majeshi ya
Congo yatashambulia, ameonya.
Kagame hakuhudhuria
Mkutano huo hata hivyo haukuhudhuriwa na rais wa Rwanda Paul Kagame.
Maafisa wa Uganda wametangaza hapo mapema Jumamosi kuwa Rwanda badala
yake itawakilishwa na waziri wa mambo ya kigeni Louise Mushikwabo.
Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Kagame amekuwa akikana shutuma , sio tu kutoka jamhuri ya kidemokrasi ya
Congo lakini pia kutoka kwa wachunguzi wa umoja wa mataifa , kuwa
Rwanda inawaunga mkono , na kuliendesha jeshi la waasi la M23 ambalo
wengi wao ni kutoka kabila la Watutsi.
Waasi watakiwa kusitisha mapigano
Katika taarifa yao ya pamoja mwishoni mwa kikao chao , viongozi wa
kimkoa wamelitaka kundi la waasi la M23 , "kusitisha shughuli zote za
kivita", na "kuacha kusema kuwa wanataka kuiangusha serikali
iliyochaguliwa ya Congo."
Siku ya Jumatano Nov 21 mwaka huu 2012), Vianney
Kazarama, mmoja kati ya viongozi wa waasi, amesema kuwa Kabila ni lazima
aondoke madarakani.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uganda Sam Kutesa amesema kuwa mkutano huo
umetoa wito kwa waasi kuondoka kutoka mjini Goma na kurejea katika eneo
karibu kilometa 20 kaskazini mwa mji huo.

0 comments:
Post a Comment