Wachezaji
wa Serengeti Boys, Hussein Twaha (shoto), Joseph Lubasha na Selemani
Hamis Bofu wakibadilioshana mawazo wakati wakitoka mapumziko
TIMU ya taifa ya vijana ya Tanzania 'Serengeti Boys' imejiweka
njia panda baada ya kuichapa Congo Brazaville bao 1-0 katika mchezo wa
kwanza wa kusaka tiketi ya kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika
kwa vijana mwakani.
Chipukizi Mudathiri Yahya aliifungia Serengeti
Boys bao pekee katika dakika ya 15 kwa mpira wa adhabu uliompita kipa wa
Congo Brazaville, Ombandea Mpea katikati ya miguu 'tobo' na kujaa
wavuni.
Kwa matokeo hayo sasa Serengeti Boys watalazimika
kufanya kazi ya ziada kulinda ushindi wao huo watakapokuwa jijini
Brazaville wiki mbili zijazo kwenye mchezo wa marudiano ili kukata
tiketi ya kwenda Morocco.

Selemani Hamis Bofu akitafuta mbinu za kumtoka beki wa Congo Brazzaville, Tmouele Ngampio
Selemani Hamis Bofu akitafuta mbinu za kumtoka beki wa Congo Brazzaville, Tmouele Ngampio
Kocha Jacob Michelsen alisema mchezo ulikuwa mgumu kwa vijana wake, lakini anawashukuru kwa kupata ushindi huo.
"Nimefurahi tumeshinda ingawa ni ushindi
mwembamba, sasa tunahitaji kujiandaa vizuri zaidi kwa ajili ya mechi ya
marudiano," alisema Michelsen.
Serengeti Boys sasa inahitaji ushindi au sare
yoyote ili iweze kurudia rekodi yake ya mwaka 2003 walipokata tiketi ya
kwenda Gambia, lakini waliondolewa kushiriki kwenye michuano hiyo na
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kubainika walitumia wachezaji
waliozidi umri akiwamo Nurdin Bakari wa Yanga.
Katika mchezo wa jana, Congo walionekana kucheza
kwa kujiamini na kutumia pasi fupifupi, lakini ngome ya Serengeti
ilikuwa makini kujilinda na kufanya mashambulizi ya kushtukiza.
Katika dakika ya 14 mchezaji Seleman Bofu wa
Serengeti Boys aliangushwa nje kidogo ya eneo la 18 na beki wa Congo
hivyo mwamuzi Miiro Nsubuga kutoka Uganda alitoa adhabu iliyopigwa na
Mudathiri na kwenda moja kwa moja wavuni na kuamsha shangwe kwa
mashabiki wachache waliojitokeza uwanjani hapo.
Baada ya bao hilo, Congo waliamka na katika dakika
ya 26 bado kidogo wangepata bao la kusawazisha baada ya mpira wa kona
wa Ibara Vinny kuunganishwa kwa kichwa na Obassi Gambo na kupaa juu
kidogo ya lango la Serengeti.
Katika dakika ya 32, mchezaji Hussein Ibrahim wa
Serengeti Boys aliwatoka mabeki wa Congo na kupiga shuti lililodakwa na
kipa Mpea.
Vijana wa Congo walitawala sehemu kubwa ya mchezo
huo, lakini washambuliaji wake walikosa mbinu za kuipenya ngome ya
Serengeti Boys ambao wenyewe walikuwa wakicheza kwa kujihami na kutumia
mipira mirefu na kushambulia kwa kushtukiza.
Kipindi cha pili vijana wa kocha Michelsen
walirudi uwanjani kwa kasi zaidi na katika dakika ya 59 shuti la
Mudathiri la umbali wa mita 35 lilitoka sentimita chache.

0 comments:
Post a Comment