
Midundo ya ngoma imekuwa moja ya matukio katika marekebisho ya katiba kama wanakijiji hawa mkoani Singida wanavyoonekana.
WATANZANIA wametakiwa kujifunza uandikaji wa Katiba mpya kutoka kwa jirani zao Wakenya ili kupata Katiba bora waitakayo.
Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba la Kenya, Kawive Wambua alipokuwa akitoa mada katika semina ya Katiba kwa asasi za kiraia inayoendelea Dodoma.
Wambua alisema Kenya imekuwa katika historia ndefu ya uundwaji wa Katiba, ambapo hatimaye iliipata mwaka 2010 baada ya mivutano mingi.
“Kwanza Watanzania wajue kuwa kupata Katiba mpya siyo kazi rahisi, kwani Serikali inaweza kuuteka mchakato mzima na kuwaacha wananchi nje hivyo wasiipate Katiba wanayoitaka,” alisema Wambua.
Alisema kati ya mambo ambayo mchakato wa Katiba unaoendelea yameshaanza kukosewa ni Tume ya Katiba kukataza utoaji wa elimu ya uraia kabla ya utoaji wa maoni.
“Sheria ya Katiba ya Tanzania ina upungufu mwingi, Kitendo cha kukataza watu au asasi za kiraia kutoa elimu ya uraia ni kuwanyima fursa wananchi kujua kile wanachotakiwa kukitoa mbele ya tume hiyo.’ Alisema na kuongeza:
Ilitakiwa angalau itolewe miezi mitatu ya elimu ya uraia, ndipo wananchi watoe maoni, Ndivyo tulivyofanya Kenya, vinginevyo wananchi wengi wamekurupushwa tu na hawajui cha kusema mbele ya Tume,” alisema Wambua.
Wambua pia alizitaka asasi za kiraia kuungana na kuwa kitu moja katika mchakato wa Katiba, badala ya kukaa kimya hasa wakati huu ambao tayari upungufu umeshajionyesha.
“Je, asasi za kiraia ziko pamoja katika mchakato huu unaoendelea?kama sheria na ukusanyaji wa maoni unaonekana kuwa na upungufu, bado asasi zimekaa kimya tu?” alihoji.
Akizungumzia zaidi kuhusu umuhimu wa asasi za kiraia, Wambua alisema utungwaji wa Katiba hauwezi kufanikiwa bila uwepo wa awasasi hizo.
“Asasi za kiraia zinasaidia mchakato wa Katiba kwa kufanya uchambuzi wa masuala ya kisheria, kuhamasisha watu, kutoa miongozo, kutoa mapendekezo, mapingamizi na ikishindikana kabisa kuchochea maandamano na migomo,” alisema Wambua.
Alisema Katiba ni ya wananchi hivyo wao ndiyo wanatakiwa kupewa nafasi ya kutosha badala ya Serikali kuuteka mchakato huo.
Katiba ndiyo inayounda Serikali na mfumo wake mzima, sasa kama Serikali inayoundwa na Katiba inataka ndiyo iiunde Katiba, nini kitatokea? Uundwaji wa Katiba unatakiwa kuwa sawia kwa matakwa ya wananchi na makundi yao,” alisema.
Aliyataja makundi ya wananchi yanayopaswa kuhusika kuwa ni vyama vya siasa, asasi za kiraia, makundi ya kidini, wanataaluma, sekta binafsi, wanawake na watu wa hali ya chini.
“Watu wote katika tamaduni zao, wawe wanawake na wanaume wana haki sawa katika uundwaji wa Katiba, Uundwaji wa Katiba unapaswa kuheshimu hali za wananchi hao kiuchumi, tamaduni zao, jinsia, dini zao, imani zao, kazi zao na hali zao kimaumbile,” alisema.
Alisisitiza kuwa mchakato huo unapaswa kuwa wazi na wa mashauriano zaidi huku ukifuata kanuni zote za utawala bora, ikiwa ni pamoja na uwajibikaji, uaminifu, ukweli na maadili.

0 comments:
Post a Comment