Lilian Lucas, Morogoro
BIASHARA ya vyuma chakavu na uharibifu wa miundo mbinu ya umeme, maji, madaraja na simu huenda ikamalizika baada ya kugunduliwa na kutambulishwa kwa teknolojia mpya ya kurudisha uhai wa vyuma, vilivyoanza kuharibika kwa kupata kutu na hatimaye vyuma hivyo kudumu kwa miaka kati ya 10 hadi 45 zaidi.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Mac Donald Liveline Technology, Donald Mwakamele alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika chuo hicho ambacho kimekuwa kikifundisha namna ya kutengeneza umeme bila kuzima kilichopo Mvomero mkoani Morogoro.
Alilazimika kufafanua hayo kwa waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mafunzo kwa wataalamu kutoka nchi za Afrika Mashariki walioanza kunufaika na mafunzo ya matumizi ya teknolojia hiyo mpya maarufu kama ‘zinga’ ikimaanisha ‘zink governise’ iliyobuniwa miaka kadhaa iliyopita nchini Ubeljiji.
Mwakamele alisema kuwasili kwa teknolojia hiyo kutanusuru gharama kubwa zilizokuwa zikitumika kununua vyuma vipya au kutumia njia isiyo endelevu wala tija ya kupaka rangi vyuma vilivyoathiriwa, jambo ambalo lilikuwa halimalizi tatizo.
Alisema ujio wa teknolojia hiyo rahisi na inayopunguza gharama za kununua upya vyuma ambavyo vingine ni aghali, kutasaidia kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwenye kampuni, taasisi na maeneo yanayotumia vyuma kama kwenye ujenzi wa madaraja, nguzo kubwa za kusaifirisha umeme au mawasiliano ya simu, vifaa vya umeme, reli na maeneo mengine.
Baadhi ya wataalamu waliokuwa wakijifunza teknolojia hiyo, Saida Kassim kutoka Dar es salaam na Petter Ogune toka Kampala nchini Uganda, walisema njia hiyo ni ya kitaalamu na rahisi kufanya kazi, na itasaidia kuongeza fursa ya ajira na uhai wa vifaa mbalimbali ambavyo vingine vimekuwa vikiuzwa kwa gharama kubwa.
Aidha wataalamu kutoka nchi za Ubelgigi, Christian Verbrugghe na Kenya, Kayur Patel walibainisha kuwa teknolojia hiyo mbali na kurudisha uhai wa vyuma, itapunguza gharama za ununuzi wa vifaa vipya mara kwa mara na imeonyesha mafanikio makubwa katika nchi mbalimbali duniani.

0 comments:
Post a Comment