MBIO za kuelekea ikulu ya White House nchini Marekani zimeingia katika
saa za mwisho huku wagombea wakiizunguka nchi kutoa hoja za mwisho
kuhusu uchumi, uokozi wa viwanda vya magari na msongamano jijini
Washington.
Obama mwenye umri wa miaka 51 na mpinzani wake Mitt Romney mwenye umri
wa miaka 65 wanazidiana kidogo kwa mujibu wa maoni yanayochapichwa na
vyombo vya habari, na kila moja anapambana kuwashawishi wapiga kura
ambao bado hawajaamua nani wamchague.
Walipishana jimboni Ohio Jumapili, ambalo ndilo linalosemakana kuwa
muhimu zaidi miongoni mwa majimbo saba yenye maamuzi katika uchaguzi wa
Marekani.
Juu ya hilo, Obama alizitembelea New Hampshire, Florida na
Colorado siku hiyo ya Jumapili, wakati Romney alizitembelea Iowa,
Virginia na Pennslyvania.
Msisitizo wa Obama katika kipindi hiki ni kwa
wapiga kura kuchagua kati ya dira mbili.
"Huu siyo tu uchaguzi kati ya
wagombea wawili au vyama viwili, ni uchaguzi kati ya dira mbili tofatu
za Marekani," alisema Obama.
Rais Barack Obama akitambulishwa na rais wa zamani Bill Clinton katika mkutano wa kampeni mjini Concord, New Hampshire.
Hoja za mwisho za Obama jimboni Ohio zilijikita katika uokozi wa kampuni
za magari za Chrysler na General Motors mwaka 2009, ambao Romney
aliupinga akiwa gavana wa jimbo la Massachusets wakati huo na kisema
sekta ya magari ilipaswa kuachwa ifilisike. Matamshi hayo yamekuja
kumuathiri, hasa katika jimbo lenye viwanda vingi la Ohio.
Katika mkutano siku ya Ijumaa mjini Springfield, Ohio, Obama aliwaambia
wafuasi wake waliyozomea alipotaja jina la Romney, kwamba kupiga ndiyo
kisasi bora zaidi.
Romney alitumia mkutano wake mjini Cleveland
kumshambulia Obama kuhusiana na kauli yake hiyo, na kusema badala yake,
yeye anawaomba wapiga kura wachague kwa mapenzi ya nchi yao. Romney
alisema mabadiliko aliyoahidi Obama yameshindikana.
"Mabadiliko hayawezi kupimwa kupitia hotuba, mabadiliko yanapimwa
kupitia mafanikio, na miaka minne iliyopita mgombea Obama aliahidi mambo
mengi kwa watu wengi lakini ametimiza kidogo sana," alisema Romney.
Wapambe wapishana kushawishi wapiga kura
Makundi yanayojitolea kwa ajili ya wagombea yalikuwa yanapishana katika
majimbo yenye maamuzi, wakiwasiliana na wafuasi wao kuhakikisha kuwa
watapiga kura na kujitolea kuwasafirisha kwenda kwenye vituo vya kupigia
kura.
Wakati Romney akiwasihi wafuasi wake waende kwa wingi katika
vituo vya kupigia kura siku ya jumanne, Obama anaelekeza juhudi zaidi
katika majimbo yenye maamuzi.
Maoni yamekuwa yakiwaonyesha wawili hao wakikaribiana kwa sana lakini
wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema Obama bado ana nafasi ya
kushinda.
Edward Wycof William, mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema
maoni yamekuwa yakibadilika kutoka wiki moja hadi nyingine, lakini
kilichoonekana ni kwamba Romney hajaongoza kabisaa katika maoni yoyote
katika majimbo muhimu.
Mitt Romney akiweka sahihi yake katika fulana ya mfuasi wake mjini Des Moines, Iowa Novemba 4.
Obama akumbushia hali ngumu aliyoikuta mwaka 2008
Obama anatafuta awamu ya pili huku kiwango cha ukosefu wa ajira kikiwa
asilimia 7.2.
Hakuna rais aliyefanikiwa kupata muhula wa pili tangu
kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia kukiwa na kiwango cha
ukosefun wa ajira kilicho juu ya asilimia 7.2.
Uchumi bado unakua kwa
chini ya asilimia 2, lakini Obama amewakumbusha wapiga kura juu ya
mazingira ya mgogoro alimochaguliwa miaka minne iliyopita.
"Kumbukeni mwaka 2008 tulikuwa katikati ya mgogoro mbaya zaidi tangu
mdororo mkubwa wa uchumi. Tulikuwa katikati ya vita viwili.
Na sasa
biashara zetu zimetengeneza ajira karibu milioni 5.5, viwanda vya magari
vinafanya vizuri na sekta ya nyumba inaanza kurejesha thamani yake,
tunategemea mafuta kutoka nje kwa kiasi kidogo kuliko wakati wowote
katika kipindi cha miaka 20," alimesema.
Obama na kuongeza kuwa vita vya Iraq
vimekwisha, vile vya Afghanistan vinakaribia mwisho na Osamba bin Laden
aliuawa.
Wanajeshi wa Marekani wakiushusha shehena ya msaada kwa ajili ya
waathirika wa kimbunga Sandy.
Marekani inakwenda kwenye uchaguzi wakati
eneo la kaskazini mashariki likikabiliana na madhara ya moja ya tufani
kubwa zaidi katika historia ya nchi hiyo.
Takriban watu milion 27 wamekwisha piga kura katika uchaguzi wa mapema.
Zaidi ya milioni 130 walipiga kura mwaka 2008. Wapiga wanatarajiwa
kuamua hatma ya viti vyote 435 vya Bunge la wawakilishi ambalo
linatarajiwa kuendelea kudhibitiwa na chama cha Republicans, na theluthi
moja ya viti vya bunge la Seneti lenye viti 100, ambako chama cha
Democrats kinatarajiwa kuedeleza udhibiti mdogo.
Uchaguzi wa mwaka huu
unafanyika wakati sehemu ya kaskazini mashariki inakabiliana na madhara
ya kimbunga cha Sandy kilichoharibu maelfu ya makaazi na kuua watu zaidi
ya 100.
Waendesha kura za maoni wamtabiria ushindi Obama
Obama anaendelea kuwa na faida dhidi ya Romney katika majimbo yenye
maamuzi, ambayo ndiyo yanaamua mshindi wa urais.
Ili kushinda kiti
hicho, mgombea laazima kura 270 za majimbo. Obama anahitaji
kujihakikishia kura 243 za majimbo yanayoegemea chama cha Democrats,
wakati Romney anaweza kujihakikishia kura 206, na hii inamuongezea
shinikizo la kutafuta zaidi kura za majimbo yenye maamuzi.
Tayari mawakili wa kambi zote wanajianda kwa mpanbano mrefu wa mahakani
katika majimbo yenye ushindani mkubwa. Baadi ya wataalamu wanatarajia
vuta nikuvute kama zile za mwaka 2000, zilizochukua wiki tano kumpa
ushindi George W.
Bush. Tayari mvutano umeripotiwa jimboni Florida,
baada ya wapiga kura wanaodhaniwa kuwa wa Democrats kuzuiwa na gavana wa
jimo hilo ambaye ni wa chama cha Republican.
Obama na timu yake wakifuatilia mauaji ya Osama bin Laden. mauaji hayo yamekuwa moja ya hoja zake za kutaka muhula wa pili.
Maoni yaliyochapishwa na gazeti la Wall Street Journal siku ya Jumapili
yalimpa Obama asilimia moja zaidi ya Romney kitaifa akiwa na asilimia 48
dhidi ya 47 za Romney.
Tovuti ya Real Clear Politics ilimpa Obama
uongozi wa asilimia 0.2.
Karibu waendesha kura za maoni wote
wamemtabiria ushindi Obama katika kura za majimbo.
Talking Point Memo
imempa Obama kura 303 dhidi ya 191 za Romney, Fivethirtyeight.com imempa
Obama kura 307 dhidi ya 231 za Romney na Pricneton Election Consortium
ilimpa Obama kura 277 dhidi ya 206 za Romney.

0 comments:
Post a Comment