WAPATANISHI wakuu katika mgogoro wa Mali wanajaribu kukishawishi kikundi
kimoja cha kiislamu kaskazini mwa nchi hiyo kujitenga na tawi la
al-Qaida.
Kuna taarifa kwamba kikundi hicho kiko tayari kuitikia wito
huo.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Burkina Faso, Djibrill Bassole ambaye
anasaidia juhudi za usuluhishi zinazofanywa na nchi yake kujaribu
kuumaliza mgogoro wa Mali uliodumu kwa miezi saba, amesema atakutana kwa
mazungumzo na viongozi wa kikundi hicho, Ansar Dine mwishoni mwa juma
hili.
Ansar Dine imetuma ujumbe nchini Burkina Faso na Algeria kuzungumzia
kupatikana kwa amani.
Rais wa Burkina Faso Blaise Compaore ambaye ni
mpatanishi mkuu wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi,
ECOWAS, katika mgogoro wa Mali, atakutana pia na ujumbe wa Ansar Dine,
hii ikiwa ni kwa mujibu wa waziri wake wa mambo ya nchi za nje, Djibrill
Bassole.
Viongozi wa ECOWAS wanaongoza juhudi za upatanishi nchini Mali.
Compaore anatarajiwa kuwaeleza kinaganaga wajumbe wa Ansar Dine matakwa
ya ECOWAS, ambayo ni kulitaka kundi hilo lijitenge na mienendo ya
kigaidi na kihalifu, na kurejea kwenye mchakato wa kisiasa.
Ansar Dine tayari kuitupa mkono al-Qaida
Kiongozi wa Ansar Dine Algabass Ag Intalla ameliambia shirika la habari
la AFP kwamba kikundi chake kinajitegemea na kiko tayari kufanya
mazungumzo ya amani.
Vile vile ameelezea utayari wake wa kukutana ana
kwa ana na waziri wa serikali ya mpito ya Mali ambaye kwa sasa yuko
mjini Ouagadougou, ikiwa mpatanishi atataka iwe hivyo.
Afisa wa serikali
ya Mali amesema mkutano baina yao na kiongozi huyo wa Ansar Dine
unawezekana.
Blaise Compaore anashinikiza kupatikana kwa suluhisho la amani katika
mgogoro wa Mali, ingawa maandalizi ya hatua za kijeshi pia yako mbioni.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi uliopita lilipitisha azimio
linaloutaka Umoja wa Afrika kufanya matayarisho ya uingiliaji kati
kijeshi, ambao utashirikisha wanajeshi zaidi ya 3,000 kulikomboa eneo la
kaskazini mwa Mali.
Ansar Dine ni mojawapo ya makundi yanayoishikilia sehemu kubwa ya
kaskazini mwa Mali, baada ya kuupiku uasi wa kundi la wapiganaji wa
kituareg, kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyoiangusha serikali ya Mali
mapema mwanzoni mwa mwaka huu.
Kundi hilo linaloongozwa na Iyad Ag
Ghaly, limetuma ujumbe mwingine nchini Algeria, ambayo pia inapakana na
Mali.
Umuhimu wa Algeria.
Sehemu kubwa ya kaskazini mwa Mali iko mikononi mwa makundi ya kiislamu.
Kiongozi huyo amekaririwa na gazeti la Algeria, El-Watan, akisema
yuko tayari kuvunja uhusiano wake na tawi la Al-Qaida kaskazini mwa
Afrika, AQIM, na kujiunga na juhudi za kimataifa kutafuta amani nchini
Mali.
Algeria inachukuliwa kama mshirika muhimu katika mapambano dhidi
ya makundi yenye misimamo mikali ya kiislamu na mwanzoni mwa Juma hili
nchi hiyo ilitembelewa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani,
Hillary Clinton, ambaye alikuja kuunga mkono mchakato wa kutafuta suluhu
kwa mgogoro wa Mali.
Vyanzo vingine vya habari ndani ya kikundi cha Ansar Dine kimeelezea
uwezekano wa ujumbe mwingine wa kikundi hicho kuizuru Nigeria.

0 comments:
Post a Comment