Godbless Lema.
RUFAA ya aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema inatarajiwa kuanza kusikilizwa leo na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani; Salum Massati, Nathalia Kimaro na Bernard Luanda.
Pamoja na mambo mengine, rufani hiyo itakayosikilizwa Dar es Salaam, itawakutanisha wanasheria wawili ndugu; Tundu Lissu na Alute Mghway wa upande wa mashtaka na utetezi.
Lissu ambaye ni kada wa Chadema na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema jana kwamba atakuwapo mahakamani leo na wakili mwenzake, Method Kimomogolo wakishirikiana kumtetea mteja wao.
Wakati Lissu akimtetea Lema, Mghway ni wakili anayewatetea warufani wa (wajiburufaa) ambao ni makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel.
Makada hao walimfungulia Lema kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, wakipinga matokeo yaliyompa ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Hukumu ya kesi hiyo ndiyo iliyomvua ubunge Aprili 5, 2012 mwaka huu.
Baadaye Lema alikata rufaa kupinga hukumu iliyomvua ubunge, lakini ilitupiliwa mbali baada ya Mahakama kuridhika kuwa kulikuwa na dosari za kisheria, kutokana na pingamizi lililowekwa na warufaniwa.
Hata hivyo, tofauti na hoja za wakili wa warufaniwa, Mghway kuwa kutokana na dosari hiyo, mrufani hana nafasi ya kufanya marekebisho, mahakama ilimpa Lema nafasi nyingine ya kufungua upya rufaa hiyo baada ya kusema dosari hizo zinarekebishika.
Mahakama hiyo ilimpa Lema siku 14 kufanya marekebisho na kufungua tena rufaa hiyo, kazi ambayo aliitekeleza.
Awali, rufaa hiyo ilikuwa ikisikilizwa na jopo lililoongozwa na Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman akisaidiana na Jaji Salum Massati na Jaji Nathalia Kimaro, lakini sasa Jaji Mkuu, Othman hayuko katika jopo hilo na nafasi yake imechukuliwa na Jaji Luanda.
Katika rufaa yake ya awali, Lema alitoa hoja 18 za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha iliyomvua ubunge, lakini tarehe ambayo rufaa hiyo ilitarajiwa kuanza kusikilizwa, wakili wa wajiburufaa, Mughwai aliweka pingamizi la awali.
Wajiburufaa katika pingamizi lao walitoa hoja tatu za pingamizi wakidai kuwa kuna mkanganyiko katika vifungu vya sheria kati ya vile vilivyotumika kwenye hukumu na vile vilivyokuwapo kwenye muhtasari wa hukumu.
Hoja nyingine walidai kuwa muhtasari wa hukumu haukuwa na mhuri wa Jaji aliyeitoa wala tarehe na hoja ya tatu ilikuwa ni utaratibu wa kuandika muhtasari huo, kwa kutokuandika maneno.
“Imetolewa kwa mkono wangu na mhuri wa Mahakama.”
0 comments:
Post a Comment