SAKATA
la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini,
Dk. Steven Ulimboka, limeanza kuibua taswira mpya kwa umma, kutokana na hatua
ya Jeshi la Polisi kukwepa kumhoji wala watu wake wa karibu aliokuwa nao kabla
na baada ya kutekwa.
Hata baadhi ya watu aliowatuhumu kwa kuwataja kuhusika na
kutekwa kwake nao hawajawahi kuhojiwa.
Na wale waliomwokota katika msitu wa Mabwepande na kumkabidhi
katika kituo cha polisi hawajahojiwa. Huku mtuhumiwa pekee Joshua Mulundi akiwa
anashinikiza polisi impeleke Dk. Ulimboka amtambue kama alihusika na utekaji
huo au la, ili kesi yake iweze kuendelea.
Jana polisi waliibuka na kumwita wakili wake, Nyaronyo Kicheere,
afike makao makuu ya jeshi hilo kwa mahojiano leo.
Watu ambao hawajahojiwa ni pamoja na mkazi wa Mabwepande
aliyemwokota muda mfupi baada ya kuteswa kwake na Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria
na Haki za Binadamu, aliyekwenda kumchukua mstuni na kumkabidhi polisi.
Wapo pia daktari mwenzake aliyekuwa naye wakati akitekwa na
Ramadhani Abeid Ighondu, ambaye Dk. Ulimboka alimtaja kuwa ni mtumishi wa
Ikulu, akidai alihusika kumteka.
Ni katika mkorogano kama huo, wadadisi wa masuala ya kijamii
wanalifananisha sakata la Dk. Ulimboka na lile la aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu
wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Dk. Daudi Balali.
Dk. Balali alihusishwa na tuhuma za ubadhirifu wa mabilioni ya
fedha za Akaunti ya Malipo ya Nje ya benki hiyo (EPA), lakini wakati wote
hakuwahi kuhojiwa na serikali, kwa kile kilichoelezwa kuwa hawakufahamu alipo
hadi baadaye wananchi walipoelezwa kuwa alifariki dunia nchini Marekani.
Kesi za EPA zinaendelea hadi leo kwa baadhi ya wafanyabiashara
na vigogo waliodaiwa kuhusika kuchota fedha hizo, ingawa Dk. Balali ambaye
alikuwa awe shahidi namba moja inaelezwa kuwa hayupo tena.
Sakata la Dk. Ulimboka nalo linaelekea kuchukua mkondo wa lile
la Dk. Balali, kwani kama shahidi namba moja, serikali haitaki kumhoji kupata
ukweli wa tukio zima au kuwahoji watu wake wa karibu pamoja na anayetajwa kama
mtumishi wa Ikulu ili kuwaondoa hofu wananchi, badala yake wanatafutwa na
kuhojiwa watu wa kando.
Wakati wananchi wakihoji alipo Dk. Balali na kutaka arejeshwe
nchini, Msemaji wa Rais Ikulu, Salva Rweyemamu, alijibu kwa tambo kuwa serikali
ina mkono mrefu, hivyo akihitajika ataletwa nchini.
Ni katika kauli kama hiyo, baadhi ya watu wanahoji kuwa serikali
inamaanisha kwamba hata Dk. Ulimboka hahitajiki kwa sasa, ndiyo maana haitaki
kumhoji kupata ukweli wa kutekwa kwake.
Lakini katika hatua ya kushangaza, Jeshi la Polisi limemwandikia
barua wakili wa wake, likimtaka afike makao makuu leo kwa ajili ya mahojiano
akielezwa kuwa ni kwa amri ya polisi chini ya kifungu namba 10(2) na 2(a) cha
sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai jalada namba WH/IR/5511/2012..PI Na
5/2012.
Kicheere ndiye alisoma tamko aliloliandika Dk. Ulimboka, Oktaba
17, mwaka jana, kuelezea mkasa mzima uliompata na kuwataja watu aliodai
wanahusika katika tukio hilo.
Akizungumza na gazeti hili jana jioni kwa simu, Kicheere alisema
kuwa alipokea barua hiyo lakini akawaeleza kwamba leo ana kesi mahakamani
asubuhi, hivyo atakwenda kuhojiwa mchana akiwa na wakili wake, Mabere Marando.
“Nimesoma barua yao lakini kwa kumbukumbu zangu sina kosa lolote
la jinai kwa mujibu wa jalada hilo, nadhani ni masuala ya Dk. Ulimboka kuhusu
tamko lake nililolisoma kwa niaba yake mwaka jana,” alisema.
Alisema kuwa ameona ni vema akajipanga kuongozana na wakili wake
pamoja na baadhi ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari marafiki zake, kwa
ajili ya kumwekea dhamana ikiwa itahitajika.
Alipotafutwa jana jioni kwa simu yake ya kiganjani kuthibitisha
kuitwa kwa wakili wa Dk. Ulimboka kwa mahojiano, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai
(DCI), Robert Manumba, msaidizi wake alisema asingeweza kupatika kwa wakati
huo.
Dk. Ulimboka alitekwa, kuteswa na kuumizwa vibaya, ikiwa ni
pamoja na kung’olewa kucha na meno usiku wa Julai 26, mwaka jana na kisha
kutelekezwa katika msitu wa Mabwepande, nje kidogo ya Jiji la Dar e Salaam.
Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam chini ya Kamanda Suleiman Kova, alitangaza kuunda kamati ya wataalamu
kutoka ndani ya jeshi hilo ili kuchunguza sakata zima na kuanika ukweli ndani
ya muda mfupi.
Hata hivyo tangu kuundwa kwa kamati hiyo, Kova amekuwa akipiga
danadana kutoa ripoti akidai amekwisha kuikabidhi kwa wakubwa wake, lakini hivi
karibuni Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso, alisema hakuna chombo kama hicho
na wala Dk. Ulimboka hatahojiwa.
CHANZO http://www.freemedia.co.tz
0 comments:
Post a Comment