Sakata
la biashara ya binadamu ambalo limeibuka kwa kasi nchini limeanza
kufanyiwa kazi na serikali baada ya Jeshi la Polisi Kikosi cha Maji
kuwatia mbaroni mawakala watano ambao ni wanawake wakituhumiwa
kujihusisha na biashara hiyo.
Kamanda
wa Polisi wa Kikosi cha Maji, Mboje Kanga, akizungumza na NIPASHE jana
kuhusu hatua ambazo zinachukuliwa na jeshi hilo kukabiliana na tatizo
hilo, alisema mawakala waliokamatwa ni wakazi wa Zanzibar na kwamba
hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa dhidi yao.
Kamanda
Kanga ambaye hata hivyo, hakutaja majina ya mawakala hao, alisema
walikamatwa kati ya Januari 23 na 24, mwaka huu wakiwa na watoto watano
ambao waliwanunua kutoka mikoani.
Alisema watoto ambao ni wanafunzi wa shule za msingi walikamatwa
wakitaka kusafirishwa na mawakala hao kwenda Zanzibar, umri wao ni kati
ya miaka 14 na 15 na walitoka katika wilaya za mikoa ya Ruvuma, Tabora
na Mtwara.
Aliongeza kuwa katika mahojiano na watoto hao walisema walipata ridhaa
ya kuchukuliwa na mawakala hao ambao haijafahamika baada ya kusafirishwa
kwenda Zanzibar wangepelekwa katika nchi gani.
“Biashara ya binadamu imeshamiri sana nchini, lakini tumejipanga
kukabiliana nayo, tutaendelea kuwasaka mawakala wengine zaidi
wanaojihusisha na biashara hiyo,” alisema Kamanda Kanga.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE, umebaini kuwa biashara hiyo iliibuka
kuanzia Desemba mwaka jana na kushika kasi Januari mwaka huu na
wanaosafirishwa wengi ni watoto wa kike kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Wapo wachache wa kiume pia.
Uchunguzi huo ulibaini kuwa mikoa ambayo watoto hao wananunuliwa na
mawakala kabla ya kusafirishwa kupelekwa nchi za Uarabuni kufanya kazi
mbalimbali zikiwamo za ndani ni Mtwara, Lindi, Manyara, Pwani, Tabora,
Ruvuma, Tanga na Shinyanga.
Jana gazeti hili liliandika habari kubwa ikielezea jinsi watoto hao wanavyosafirishwa kwenda kutumikishwa na maeneo wanayotoka.
Watoto hao ambao NIPASHE iliwagundua, kuwaona na kuzungumza na baadhi
yao lakini majina yao tuliyasitiri kwa sababu za kimaadili wana umri wa
miaka 14 na 15 wote kutoka kijiji cha Nakapanya wilaya ya Tunduru mkoani
Ruvuma; mmoja mwenye umri wa miaka minane anatoka mkoa wa Tabora;
wakati mwingine wa kiume mwenye umri wa miaka 15 anatoka kijiji cha
Mkangula mkoa wa Mtwara, ilhali mwenzake kutoka kijiji cha Mbembaleo
mkoani Mtwara ana umri wa miaka 14.
Pia NIPASHE iliripoti kuwa Januari 25, mwaka huu watoto waliokamatwa
bandarini wakitaka kusafiri kwenda Zanzibar ni binti mwenye umri wa
miaka 13 kutoka kijiji cha Manoro wilaya ya Lushoto mkoa wa Tanga;
mvulana mwenye umri wa miaka 13 kutoka wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma
na binti mwenye umri wa miaka 12 kutoka Tunduru Mjini.
Wengine ni binti mwenye umri wa miaka 14 kutoka kijiji cha Namalumbusi
wilaya ya Masasi mkoa wa Mtwara, mvulana mwenye umri wa miaka 12 kutoka
mkoa wa Manyara na mvulana mwingine mwenye umri wa miaka 10 kutoka
wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi.
Watoto waliokamatwa Januari 26, mwaka huu ni binti mwenye umri wa miaka
12 kutoka kijiji cha Ndanda mkoa wa Mtwara; binti mwenye umri wa miaka
13 kutoka kijiji cha Mteruka wilayani Nachingwea mkoa wa Lindi na
mwingine mwenye umri wa miaka 13 kutoka kijiji cha Mnazi Mmoja mkoa wa
Mtwara.
Wengine ni binti (13) kutoka kijiji cha Mnazi Mmoja mkoani Mtwara, binti
(14) kutoka mkoa wa Manyara na binti (17) ambaye ni mwanafunzi wa
kidato cha tatu kutoka kijiji cha Kokoro wilayani Kishapu mkoa wa
Shinyanga.
Januari 27, mwaka huu alikamatwa binti (14) mkazi wa Manispaa ya Iringa mkoani Iringa.
Taarifa kutoka ndani ya Kituo cha Kikosi cha Polisi Maji, zinaeleza kuwa
watoto hao wakishakamatwa na kuzuiwa kusafiri, wamekuwa wakichukuliwa
maelezo na baadaye kuachiwa warejee walikotoka, lakini wengine hushindwa
kurejea kutokana na kukosa nauli hivyo mawakala kupanga njama za
kuwasafirisha kinyemela.
Taarifa zinaonyesha kuwa mawakala hao wakishafanikiwa kuwapata watoto
hao kutoka katika mikoa hiyo huwapeleka jijini Dar es Salaam na baadaye
kusafirishwa kwa usafiri wa majini kutoka Bandari ya Dar es Salaam
kwenda Zanzibar.
Imebainika kuwa watoto hao wakifikishwa Zanzibar hukutana na watu maalum
ambao huwapokea na kufawanyia mipango ya kuwasafirisha kwa usafiri wa
ndege au wa majini kwenda Uarabuni ambako hutumikishwa kazi mbalimbali.
Mawakala hao wakishafanikiwa kuwasafirisha kutoka Bandari ya Dar es
Salaam hulipwa wastani wa Dola za Marekani 5,000 (Sh. milioni 8) kwa
kila mtoto wanayefanikisha kumvusha kutoka Tanzania Bara kwenda
Zanzibar.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, ili kuhalalisha safari za kuwasafirisha
watoto hao, mawakala hula njama na baadhi ya wenyeviti wa serikali za
mitaa kwa kuandika barua zinazoelezea sababu za watoto hao kwenda
Zanzibar.
Wastani wa watoto kati ya watano hadi 10 hufika katika Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusafiri kwenda Zanzibar kila siku.
Uchunguzi huru wa NIPASHE umebaini kuwa Januari 23, mwaka huu
waliwatilia shaka na polisi na kuzuiwa kusafiri ni watoto wanne ambao
walifunguliwa jalada la upelelezi kituo cha Polisi Maji ambazo ni
MUD/RB/40/2013 na MUD/RB/36/2013.
HABARI NA THOBIAS MWANAKATWE CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment