BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

CCM BUKOBA WADHALILISHANA.


WAMSUSIA MEYA, WATUMA UJUMBE MZITO KWA MANGULA.
Chanzo  http://www.freemedia.co.tz
 
Mwenyekiti wa chama cha Mapindu (CCM) Dkt, Jakaya Mrisho Kikwete.
 
CHAMA cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Bukoba Mjini, kimeingia katika siasa chafu za kudhalilishana huku vipeperushi vya kuwatusi madiwani 10 wa chama hicho na wale wa Chama cha Wananchi (CUF) vikisambazwa mitaani.

Madiwani hao waliochafuliwa kwa matusi mazito ya nguoni ambayo mengine hayaandikiki kwa kuzingatia maadili ni wale nane wa CCM akiwemo Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki, na wawili wa CUF waliosaini hati ya kumtaka mkurugenzi wa manispaa hiyo kuitisha kikao cha dharura cha Baraza la Madiwani ili kumng’oa Meya Anatory Amani anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi.

Hatua hiyo inakuja siku chache tangu Dk. Amani aamue kupuuza maagizo ya Makamu Mwenyekiti wao chama hicho taifa, Philip Mangula, kwa kufungua kesi mahakamani kupinga kujadiliwa na kung’olewa na madiwani.

Mangula ambaye alilazimika kufika mjini Bukoba mwezi uliopita ili kunusuru mtafaruku huo, aliagiza madiwani nane wa CCM waliokuwa wamesaini hati hiyo, waondoe tuhuma hizo na kuzipeleka kwenye chama ili zipatiwe ufumbuzi.

Lakini katika hatua ambayo imetafsiriwa kuwa mgogoro huo unazidi kushika kasi, juzi vipeperushi hivyo vya matusi vilisambazwa na watu wasiojulikana kwa kuvibandika katika maeneo mbalimbali ya mji wa Bukoba.

Madiwani waliosaini hati ya kutaka kuitishwa kikao cha kumng’oa meya huyo mbali na Kagasheki ni Naibu wake, Alexander Ngalinda (Kata ya Buhende) na Yusuf Ngaiza (Kashai) ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Manispaa ya Bukoba.

Wengine ni Richard Gasper (Miembeni), Dauda Kalumuna (Ijuganyondo), Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe) na Mulubi Kichwabuta (Viti Maalumu) na wale wa CUF ni Ibrahim Mabruk (Bilele) na Rabia Badru wa Viti Maalum.

Taarifa kutoka mjini Bukoba zilisema kuwa madiwani hao nane wa CCM, jana waliandika barua ya malalamiko kwenda kwa katibu wa chama hicho wilaya na nakala zake kwa mwenyekiti wa mkoa, mkuu wa mkoa na Mangula.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, barua hiyo ambayo ilikabidhiwa asubuhi wamekataa kushiriki vikao vyovyote vitakavyoongozwa na Meya Amani wakimtuhumu kuwa ndiye alihusika kusambaza vipeperushi hivyo vya kuwakashfu.

“Na katika kutimiza msimamo wetu, tayari madiwani wote nane wa CCM leo tumesusia kikao cha meya kilichojadili maandanlizi ya Baraza la Madiwani.

“Na kwa mujibu wa kanuni baada ya kukataa idadi ilikuwa haimruhusu kwendelea na kikao kwani wajumbe tuko 17 lakini alibaki na saba ambao ni pungufu,” alisema mmoja wa madiwani hao.

Katika vipeperushi hivyo, madiwani hao kila mmoja ametajwa kwa jina lake, kata na orodha ya tuhuma zake huku wengine wakidaiwa kulaghaiwa kwa fedha na mmoja wa viti maalum akidhalilishwa kwa tuhuma za ngono.

Mgogoro wa Bukoba mjini umekuwa na muda mrefu sasa na Meya Amani katika kujihami ili asing’olewe, kwa kushirikiana na mkurugenzi wake, Hamis Kaputa, walilazimika kuahirisha kikao cha Baraza la Madiwani kinyume na kanuni.

Kwa mujibu wa sheria namba 8 ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 kifungu namba 7 (1), mkurugenzi anapaswa kumwandikia barua kila mjumbe kumweleza mahali na siku vikao vitapofanyika na ajenda zitakazojadiliwa siku saba kabla ya kikao.

Madiwani hao hawakuwahi kujulishwa uwepo wa kikao hicho walichotaarifiwa na mkurugenzi kuwa kimesogezwa mbele kama kanuni hizo zinavyosema.

Kikao hicho kilikuwa cha kujadili utekelezaji wa shughuli za robo mwaka za fedha kati ya Oktoba hadi Desemba 30 mwaka jana, na kwa mujibu wa sheria kilipaswa kufanyika si zaidi ya Januari mwaka huu.

Katika barua hiyo yenye kumb. Na BMC/C.50/5/13, inayosomeka ‘Yah: Kusogezwa mbele ratiba ya vikao vya Baraza la Madiwani’, Kaputa hata hivyo haonyeshi ni lini kikao hicho kitakaa.

Kaputa, katika barua hiyo anadai kuwa baraza haliwezi kufanyika kutokana na wakuu wa idara wengi kuwa safarini kuelekea jijini Dar es Salaam kwa ajili ya vikao vya bajeti 2013/2014.

Amani ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kagondo, aliamua kwenda mbali zaidi huku akikiuka kanuni na sheria ambapo sasa amefungua pingamizi mahakamani ili kuzuia mkurugenzi asiitishe kikao chochote cha kujadili tuhuma zake kwa muda wote atakaokuwa katika wadhifa wake.

Bila kujali kuwa hatua hiyo ni kinyume na sheria namba 8 ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 kifungu namba 5(1)(2)(c) ambacho kinasema kuwa mwamuzi wa mwisho katika migogoro yote ni Waziri wa Tamisemi, Amani aliamua kupiga hodi mahakamani.

Taarifa ambazo gazeti hili limezipata kutoka mjini Bukoba, zilisema kuwa Amani alifungua pingamizi hilo namba 1/2013 Januari 23 mwaka huu mchana, ikiwa ni saa chache baada ya madiwani hao nane kutii agizo la Mangula la kuwasilisha barua za kuondoa tuhuma zao kwa muda.

Madiwani hao nane akiwemo mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagesheki, waliwasilisha barua zao kwa mkurugenzi ili kuondoa tuhuma zao kwa muda, asubuhi ya Januari 23 mwaka huu lakini mchana Meya Amani akafungua kesi hiyo.

Mangula aliwataka madiwani hao kuunda kamati ya kushughulikia mgogoro huo chini ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe.

Mgogoro huo umekipasua chama hicho mjini Bukona kutokana na Massawe, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mwenyekiti na Katibu wa CCM mkoa kudaiwa kumkingia kifua Amani.

Balozi Kagasheki, ambaye pia ni Waziri wa Malialisili na Utalii, anaunga mkono msimamo wa CHADEMA, kupinga miradi ya uuzwaji wa viwanja zaidi ya 5,000 na ujenzi wa soko la kisasa kutokana na mikataba ya siri yenye harufu ya kifisadi aliyoisaini Amani kwa kificho.

Halmashauri hiyo ina madiwani 24, watatu wa CUF, wanne wa CHADEMA na 17 wa CCM. Ili kupitisha uamuzi huo wa kumuondoa meya, ni lazima robo tatu ya madiwani, yaani 16, wapige kura ya kuunga mkono hoja hiyo.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: