Kwa ufupi:
Waandishi hao walitoroshwa na polisi jana saa 11:00
alfajiri kwenda mkoani Lindi ambapo pia polisi walifanikiwa kusitisha
maandamano yaliyokuwa yameandaliwa na Chama cha Wananchi (CUF), kwa
lengo la kutaka kupata tathmini ya mwendelezo wa miradi ya gesi na maji.
Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Wafanyabiashara wa Mtwara kuhusu
mgogoro wa gesi kwenye ukumbi wa VETA mjini Mtwara, Januari 28, 2013.
HALI ya usalama mkoani Mtwara bado tete baada ya jana Jeshi la
Polisi kuwahamishia mkoani Lindi waandishi wa habari 150, waliokuwa
katika mkutano wa siku tatu wa Kongamano la Nane la Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya (NHIF), uliofanyika Mtwara.
Waandishi hao walitoroshwa na polisi jana saa
11:00 alfajiri kwenda mkoani Lindi ambapo pia polisi walifanikiwa
kusitisha maandamano yaliyokuwa yameandaliwa na Chama cha Wananchi
(CUF), kwa lengo la kutaka kupata tathmini ya mwendelezo wa miradi ya
gesi na maji.
Habari zinasema wananchi hao walitaka kuwateka
waandishi wa habari kwa madai kuwa waliandika habari za kuzimwa kwa uasi
wao kuhusu gesi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda jambo wanalodai siyo
kweli.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Wilman Ndile alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Hata hivyo, alisema kuwa taarifa hizo zilikuwa ni
tetesi tu, akiongeza kwamba katika Mkoa wa Lindi kulikuwa na taarifa
kwamba yangefanyika maandamano makubwa, lakini hakuna kilichotokea.
“Ulikuwa ni uvumi wa watu, unajua hivi sasa
anaweza kuibuka mtu na kutuma ujumbe mfupi wa maneno kuhusu jambo lolote
tu, ila suala hilo la waandishi wa habari ni kweli na asubuhi
niliambiwa na OCD, lakini hali ni shwari sasa,” alisema.
Mgogoro wa gesi uliibuka mwishoni mwa mwaka jana,
baada ya Serikali kutangaza mpango wake wa kutandaza bomba la gesi
kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam.
Baadhi ya wananchi wa mkoa huo walipinga mpango
huo huku wakiungwa mkono na watu wa kada mbalimbali nchini, vikiwamo
vyama vya siasa.
Katika kuonyesha kutotaka gesi itoke mkoani humo,
wananchi hao walifanya maandamano, sambamba na kuchoma moto nyumba za
baadhi ya wabunge, ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) na jengo la
Mahakama ya Mwanzo Mtwara.
Januari 29 mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
alizungumza na wananchi wa mkoa huo na kuwatuliza jazba, baada ya
kueleza jinsi watakavyonufaika na gesi itakayozalishwa mkoani humo kabla
ya kusafirishwa kwa bomba hadi Dar es Salaam.
Pinda alisema kuwa hakuna tone la gesi ghafi
itakayosafirishwa kwa njia ya bomba na kueleza kwamba kiwanda cha
kusindika gesi ghafi kitajengwa katika Kijiji cha Madimba, mkoani humo
na mabaki yatokanayo na gesi hiyo yatumike kuvutia uwekezaji wa viwanda.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Pinda ilipingwa na
wananchi wengi ambao walidai kuwa imejaa siasa, ndiyo chanzo cha
wananchi hao kutaka kuwateka waandishi wa habari kwa maelezo kuwa
waliandika habari zenye kichwa cha habari ‘Pinda azima uasi Mtwara’,
jambo ambalo walisema siyo kweli.
0 comments:
Post a Comment