Hali hiyo ilitokana na
maswali yaliyotolewa kuwa ya kitaalamu zaidi na hivyo kuwa magumu kwa wanafunzi
wengi kiasi cha kushangaza hata shule zilizokuwa zikifanya vizuri zamani.
Akitoa maoni juu ya
wanafunzi wengi wa kidato cha nne kufeli, Mwalimu wa Taaluma wa kundi la shule
za Feza, alisema matokeo hayo yameishangaza shule hiyo na hivyo kukosa
mwanafunzi mwenye ushindi wa alama saba kama ilivyozoeleka.
Mwalimu Simon Albert
alisema jana, kwamba “maswali yalikuwa ya kitaalamu zaidi,” na kutoa mfano
kwamba mbali na masomo ya Hisabati na Biolojia, masomo mengine yalikuwa magumu
kwa kiwango cha wanafunzi wengi.
Alitoa mfano wa somo la
Jiografia ambalo shuleni kwake -Sekondari ya Wavulana ya Feza-hakuna mwanafunzi
aliyepata alama A isipokuwa mmoja aliyepata B.
Alisema mtihani ulikuwa na
mitego mingi.
Hata hivyo, Feza ilitoa washindi wawili wa kitaifa waliopata
daraja la kwanza kwa alama tisa ambazo imesema haijawahi kukosa mshindi mwenye
alama saba.
Ni janga
Matokeo hayo yameshangaza
wengi na kutajwa kuwa janga na aibu kwa Taifa, hali ambayo wadau wametaka
iundwe Tume kuchunguza mfumo wa elimu na wakati huo huo uwepo uwajibikaji wa
viongozi wa juu wenye dhamana ya elimu.
Watu binafsi, taasisi,
wanasiasa na wataalamu wa masuala ya elimu waliozungumza na gazeti hili jana,
walitaka uandaliwe utaratibu kwa ajili ya waliopata daraja la sifuri.
Walisema wanafunzi 240,903
waliopata daraja hilo kuwaacha ni kupoteza hazina ya vipaji na utaalamu kwa
kuwa kushindwa kwao hakumaanishi kwamba hawana akili isipokuwa ni mfumo mbovu
wa elimu.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Kabwe Zitto pamoja na kutaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru
Kawambwa, Naibu wake, Katibu Mkuu na Kamishna wawajibike kwa matokeo hayo,
alitaka pia Wizara hiyo ihamishiwe Ofisi ya Rais ili kunusuru sekta husika.
“Najua kuwa haina uhusiano
wa moja kwa moja, maana matatizo ya elimu ni makubwa sana nchini. Lakini ni
lazima kitu fulani kitokee ili kufanya mabadiliko.
Uwajibikaji ni njia mojawapo
inayoleta nidhamu na dharura katika utendaji kazi,” alisema Zitto.
Mbunge huyo aliendelea
kusema: “Tumwambie Rais aichukue Wizara ya Elimu, kuwe na Waziri wa Nchi Ofisi
ya Rais Elimu...tuwape masharti.”
Aliendelea: “Matokeo ya
kidato cha nne ya namna hii; zaidi ya nusu ya wahitimu kupata sifuri na
takribani asilimia 90 kufeli kwa kupata daraja la nne na daraja la sifuri ni
mwaka wa tatu sasa mfululizo… lazima uwajibikaji utokee”.
“Hawa watoto wanakwenda
wapi?... ni vema tukope kuwekeza kwenye elimu, maana elimu ni hifadhi ya jamii.
Elimu yetu ya sasa inazalisha matabaka kwenye jamii na ni hatari sana kwa uhai
wa Taifa,” alisema Zitto.
Alitaka mpango wa kujenga
vyuo vya ufundi kila halmashauri ya wilaya uanze mara moja ili kunusuru watoto
hao. Kwa mujibu wake, katika bajeti kivuli mwaka 2011 walipiga hesabu kwamba
zinahitajika Sh bilioni 720 katika kipindi cha miaka mitano ijayo kujenga vyuo
hivyo kila wilaya.
Mbatia na Tume
Chama cha NCCR-Mageuzi
katika maoni yake, kilimwomba Rais Jakaya Kikwete kuunda Tume itakayojumuisha
wataalamu waliobobea katika elimu ili kupata suluhu ya kuendelea kushuka kwa
elimu kwa kuwa limekuwa janga la kitaifa.
Mwenyekiti wa Chama hicho,
James Mbatia alitaka wadau wanasiasa, viongozi na wengine kuweka kando itikadi
za kisiasa na kutumia ujuzi wao kutetea sekta ya elimu, kwa kuwa ni suala la
kitaifa lenye kumwathiri kila mmoja.
Akizungumza na waandishi wa
habari, Mbatia alisema Tume hiyo itatakiwa ilenge kuweka mikakati ya kuboresha
elimu nchini.
“Sera ya elimu inayotumika
sasa ni ya mwaka 1995 iliyosainiwa na Profesa Philemon Sarungi licha ya
mabadiliko yote ya kidunia ambayo yamekuwa yakitokea,” alisema Mbatia.
Washindi kitaifa
Washindi wa kitaifa
walioongoza kwa kupata pointi tisa kutoka shule hiyo ya Feza ni Said Juma (17)
na Jasper Kajule (18).
Wakizungumza na mwandishi
wa habari hizi kwa nyakati tofauti jana, wanafunzi hao walisema baadhi ya
maswali yaliyotoka kwenye mtihani yalikuwa tofauti na waliyofundishwa.
Walitaka wanafunzi kutumia
vizuri mitandao huku wakishukuru uamuzi wa shule hiyo kuzuia matumizi ya simu
za mkononi shuleni.
Matokeo ni aibu Chadema kupitia kwa Waziri Kivuli wa Elimu
na Mafunzo ya Ufundi, Suzane Lyimo ilisema matokeo ya mwaka huu ni aibu kwa
Taifa.
Alitaka Serikali ichukue
uamuzi mgumu kudhibiti matokeo mabaya ili kuwezesha nchi kufanya vema katika
soko la pamoja la Afrika Mashariki.
Hali mbaya vijijini
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Tanzania Coalition on
Debt Development (TCDD), Hebron Mwakagenda alitaka hatua zichukuliwe haraka
kuondoa hali mbaya ya elimu vijijini.
“Hotuba ya Waziri inaungana
na TCDD kwamba hali ni mbaya zaidi vijijini kwa kila kitu … tunaomba hatua za
haraka zichukuliwe ili kuondoa tatizo hilo,” alisema Mwakagenda.
Alisema shule ili iwe
sekondari, vipo vitu vya msingi kama madarasa, walimu, viwanja vya michezo,
maabara na maktaba ambavyo ni lazima viwepo.
Utafiti wa TCCD ambao
taarifa yake iliwasilishwa hivi karibuni kwa wabunge, unabainisha kuwapo
ongezeko kubwa la wanafunzi katika shule hususan za kata bila kuzingatia
miundombinu ya mabweni, madarasa, vyoo, vitabu na walimu.
Katika uwiano baina ya
walimu na wanafunzi ambacho ni kigezo muhimu katika kupima ubora wa elimu,
utafiti unaonesha lipo tatizo kubwa.
Kwa mfano utafiti huo
ulibaini wilayani Kiteto, ipo shule moja ya sekondari ambayo mwalimu mmoja
anahudumia wanafunzi 1,180.
Wakati uwiano wa kitaifa ni mwalimu mmoja kwa
wanafunzi 35, utafiti uliofanyika katika wilaya saba ukihusisha sekondari 65 za
kata, unaonesha wastani wa uwiano Kiteto ni 1:72, Iramba (1:67), Lindi (1:31)
na Kibaha (1:28).
0 comments:
Post a Comment