YAPELEKA HATI YA DHARURA MAHAKAMNI IINGIE KATI
http://www.freemedia.co.tz
SAKATA la Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare, kufunguliwa kesi ya ugadi akidaiwa kupanga mikakati ya kudhuru watu, limechukua sura mpya baada ya chama hicho kudai kunasa mawasiliano ya watu kinaowatuhumu kuandaa video hiyo.
Pia CHADEMA imesema kuwa mawakili wake wamepeleka hati ya dharura katika Mahakama Kuu wakiiomba iingilie kati kwa kuitisha mafaili yote mawili ya kesi hiyo inayomkabili Lwakatare na mwenzake Ludovick Joseph.
Lwakatare alikamatwa Machi 13 mwaka huu na kuhojiwa kwa siku nne kisha kufikishwa mahakamani Machi 18 na kufunguliwa kesi namba 37/2013 yenye mashtaka manne huku Ludovick akisomewa mashtaka matatu.
Akizungunza na waandishi wa habari jana makao makuu ya CHADEMA, mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu, alidai kuwa wamenasa mawasiliano ya watu mbalimbali wanaowahisi kuhusika kurekodi video hiyo.
Lissu aliwataja watu hao kuwa ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky, Ludovick na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Mwigullu Nchemba.
Alifafanua kuwa Desemba 27 siku moja kabla ya video hiyo haijarekodiwa kulikuwa na mawasilano ya simu kutoka kwa Msacky kwenda kwa Lwakatare akimuulizia sehemu alipo.
Alisema katika mawasiliano hayo, Msacky anayetajwa kudhuriwa na mkakati huo alimpigia simu Lwakatare na kumuulizia mahali alipo ambapo alijibiwa kuwa alikuwa yuko njiani kurejea Dar es Salaam.
Lissu ambaye pia ni mmoja wa jopo la mawakili wanaomtete Lwakatare, aliongeza kuwa Desemba 28, Ludovick alifika nyumbani kwa Lwakatare siku ambayo video hiyo ilirekodiwa saa 11:59.
Aliongeza kuwa kulikuwa na mawasiliano baina ya Ludovick na Nchemba kwa kutumia namba za simu ya Nchemba inayoonekana katika kitabu cha Bunge.
Lissu alidai kuwa baada ya mawasiliano hayo kati ya Desemba 29 mwaka jana na Januari 2 mwaka huu, Nchemba alinukuriwa katika kituo cha televisheni akisema anayo video inayowaonyesha viongozi wa CHADEMA wakipanga njama za mauaji.
“Tumegundua mengi katika haya na kama tutafika mahakamani jaji au hakimu atakayekuwa anasikiliza tukiwa na hoja zetu atamaliza kesi hii ndani ya saa zisizozidi tatu,” aliongeza Lissu.
Alipotafutwa Msacky kwa simu yake ya kiganjani ili afafanue madai hayo, alikataa akidai kuwa kesi iko mahakamani.
Kuhusu kupeleka hati ya dharura kuiomba mahakama iitishe mafaili yote mawili na kutengua uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka wa kumfutia Lwakatare mashtaka uliotolewa juzi, Lissu alisema wanatambua mamlaka ya kiongozi huyo katika kufungua na kuiondoa kesi mahakamani.
Alisema lengo ni kulinda maslahi ya taifa au kuboresha utendaji wa haki, suala alilodai halikufanyika katika dhamira nzima ya kufuta kesi ya kwanza ya Lwakatare.
“Tumekaa jopo la mawakili watano; tumeiomba mahakama kuu iingilie kati na kuitisha mafaili yote mawili ya kesi hii na kisha ijiridhishe kama sababu ya kufutwa kwa kesi ya kwanza ni kwa ajili ya maslahi ya taifa,” alisema.
Alisema maombi mengine katika hati hiyo ni pamoja na kuiomba mahakama ichunguze ili kuona kama haki imetendeka kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, pia wameiomba ifute hati ya kufutiwa mashtaka kwa Lwakatare na ifute amri ya kumaliza kesi hiyo.
Pia alieleza kuwa wameiomba mahakama kuu iiamuru mahakama ya hakimu mkazi kisutu kuendelea na kesi ya awali iliyofunguliwa Machi 18 mwaka huu na pia itamke kuwa kilichofanywa na mawakili wa serikali ni kuingilia uhuru wa mahakama wa kufanya uamuzi.
Aliongeza katika kesi ya awali walihoji uwepo wa hati ya ridhaa ya DPP juu ya mteja wao kushtakiwa kwa sheria ya kupambana na ugaidi na wakaonyeshwa makaratasi yasiyokuwa na nembo yoyote ya taifa, hali iliyowafanya wahoji na kumuomba hakimu aifute kesi hiyo ombi lililokuwa linatarajiwa kutolewa uamuzi juzi.
Lissu alisema kuwa kwa mujibu wa sheria ya ugaidi ili kosa liwe la kigaidi lazima maelezo ya kosa hilo yaonyeshe kuwepo kwa malengo ya ugaidi hali aliyosema katika mashtaka yote mawili suala hilo halionekani.
0 comments:
Post a Comment