WAZIRI MTWARA OYEEEEE....WANANCHI HAITOKI, KAMA SINEMA VILE MAANA DAH.
http://www.freemedia.co.tz
Mawaziri hao ni Dk. Abdallah Kigoda wa Wizara ya Viwanda na Biashara na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Charles Tizeba, waliokuwa wameongozana na Balozi wa Nigeria hapa nchini, Nshaya Manjabu, na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Dangote ya Nigeria, Deva Kumar.
Tukio hilo limekuja zikiwa ni wiki chache tangu kutokea kwa vurugu kubwa mkoani humo katika wilaya za Mtwara Mjini na Masasi ambapo wananchi waliharibu mali za baadhi ya viongozi wa kisiasa na serikali na kumuua askari mmoja huku watu wengine wanne nao wakiuawa kwa kupigwa risasi.
Wananchi hao wa Mtwana na Lindi wamekuwa na msimamo mkali wakipinga serikali kujenga bomba la kusafirisha gesi asili kutoka kwao kwenda jijini Dar es Salaam bila kuwekewa mazingira mazuri ya kiuchumi.
Katika kuonyesha kuwa wananchi hao walikuwa wamepania kuwasulubu mawaziri hao, walifika mkutanoni huku baadhi yao wakiwa na mabango yaliyokuwa na ujumbe wa kuhoji mkutano huo umeruhusiwa na nani wakati serikali imepiga marufuku mikutano na maandano mkoani humo kwa muda.
Mara baada ya viongozi hao kufika uwanjani, Waziri Kigoda aliwasalimia wananchi akisema: “Mtwara oyeee!!!”
Waziri huyo aliitikiwa na wananchi: “Haitoki hata kama umekuja wewe hatutaki wala hatukuelewi! Mlikuwa wapi kuja huku mapema kutuelewesha habari za viwanda?”
Wanachi hao walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe uliosomeka: “Kauli mbiu: gesi haitoki, tunashukuru baada ya kimya kirefu sasa leo mmefungua rasmi mikutano tukianzia huu mkutano wenu na gesi ndio roho yetu.”
Wakati ‘zomeazomea’ hiyo ikiendelea, baadhi yao walianza kurusha mawe katika hali iliyowalazimu viongozi kuufunga mkutano huku Jeshi la Polisi likiamuru wananchi kutawanyika katika viwanja vya mkutano.
Mara baada ya hali hiyo ya vurugu, Naibu Waziri wa Uchukuzi alilazimika kuwatuliza wananchi ili wasikilize akisema: “Nisikilizeni mtaelewa tu, mwekezaji amepatikana na amemaliza hatua ya kwanza ya kufanya makadilio ya gharama za ujenzi.”
Aliongoza kuwa mamlaka ya viwanja vya ndege inafanya mazungumzo naye ili masharti ya uwekezaji yaweze kufahamika na upanuzi wa uwanja kuanza mapema.
Hata hivyo, wananchi hao hawakutulia huku wakiendelea kupiga kelele na kuwazomea: “Hilo ni changa la macho, hatutaki propaganda zenu, tumechoka na siasa zenu.”
Mkuu wa Mkoa Mtwara, Kanali mstaafu Joseph Simbakalia, hakupata nafasi ya kuzungumza kutokana na wananchi hao kuzomea huku wakimtaka aondoke.
Awali, Kigoda akizungumza katika viwanja vya bandari ya Mtwara na watumishi mbalimbali, alisema kuwa lengo la ujio wake mkoani humo ni makabidhiano ya makontena 38 ya vifaa vya ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Dagonte kinachotarajiwa kujengwa katika kijiji cha Msijute, wilaya ya Mtwara vijijini.
Makabidhiano hayo yalikuwa kati yake na Naibu Waziri wa Uchukuzi. Pamoja na mambo mengine, Kigoda alisema kuwa serikali itaendelea kupokea wawekezaji mbalimbali watakaoomba kuwekeza katika mkoa huo.
Alisema wanaangalia zaidi uwekezaji katika ujenzi wa viwanda kwa kuwa Mtwara ni kitovu cha uchumi wa taifa huku akisisitiza kuwa utafiti wa kitaalamu na kisayansi unaonyesha gesi hapa Mtwara ni nyingi sana.
Alisema viwanda vingi vitajengwa hapa na gesi itakayobaki lazima itapelekwa katika maeneo mengine.
0 comments:
Post a Comment