ASEMA HAAMINI KAMA DK SLAA ANAWEZA KUMUUA. http://www.freemedia.co.tz
SIKU moja baada ya gazeti la Mtanzania
kuandika habari likidai kuwa siri ya kumuua Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe (CHADEMA) imefichuka, kiongozi huyo amejitokeza akisema ni uzushi.Habari hiyo ilidai kuwa ilipangwa Zitto anyweshwe sumu hotelini na kumtaja Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa kuwa ndiye alimtuma kijana Ben Saanane kutimiza mkakati huo.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa kisiasa walisema habari hiyo inayodai tukio hilo lilitokea Mei mwaka jana jijini Dar es Salaam, ilikuwa ni propaganda ya kuhamisha mjadala wa sakata la kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Absalom Kibanda.
Kibanda alitendewa unyama huo Machi 6 mwaka huu, lakini hadi leo vyombo vya dola vimeshindwa kuwakamata wahusika na badala yake yamekuwa yakiibuliwa matukio mbalimbali ili kupoteza ajenda hiyo inayoonesha udhaifu wa kiutendaji wa vyombo hivyo.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Zitto alisema habari hiyo imemletea usumbufu mkubwa kwani ndugu, jamaa, marafiki na wapiga kura wake wamejawa na wasiwasi kwamba anaweza kuuawa.
“Moja, sijawahi katika maisha yangu yote kukutana na mtu anayeitwa Ben Saanane na hivyo hicho kikao ambacho inasemekana nilikuwa naye na akajaribu kunipa sumu hakijawahi kutokea. Imetajwa Hoteli ya Lunch Time ambayo sio tu sijawahi kufika, pia hata siijui ipo wapi,” alisema.
Alifafanua kuwa haijawahi kutokea yeye kufanya kikao cha pamoja na Ben Saanane, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba. Hivyo habari iliyoandikwa ni ya kufikirika.
“Pili, siamini kamwe kuwa Katibu Mkuu wa chama changu (Dk. Slaa) anaweza kupanga kuniua maana hana sababu ya kufanya hivyo. Napenda kurudia kusema kwamba mimi ninaamini kuwa kila nafsi itaonja mauti.
“Kila mtu atakufa. Kama nitakufa kwa kuuawa na mtu mwingine ndiyo itakuwa nimeandikiwa hivyo na Mungu.
Ndiyo maana hata siku moja silalamiki kuhusu vitisho vya kuuawa.
Kama kuna mtu anafikiria kuwa kumuua Zitto ndiyo furaha ya maisha yake atakuwa anajidanganya tu maana Zitto anaweza kufa kimwili, lakini mawazo, fikra na maono yake yataishi tu,” alisema.
Aliongeza kuwa haogopi kufa maana maisha aliyoyachagua ndiyo haya ambayo yamejaa vitisho, kwamba muhimu kwake ni kufanya kazi zake kwa bidii, uhodari na uaminifu.
“Tatu, nawashauri watu ambao wamehama CHADEMA na kuhamia vyama vingine watumie muda wao kujenga vyama vyao badala ya kila siku kuzungumzia masuala ya chama ambacho wao sio wanachama tena.
“Kama mtu kaamua kuhama CHADEMA anapoteza haki ya kujadili masuala ya CHADEMA, maana kama angekuwa anapenda kuyajadili asingehama. Naonya mtu yeyote ambaye anatumia jina langu ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa,” alionya Zitto.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA (Bara), alisema chama hicho si pango la watesaji wala wauaji, kwamba kuna mwanachama wa chama kingine cha siasa anayedhani kuna mtu ndani ya CHADEMA anapanga mipango ovu aende kwenye vyombo vya sheria kumshtaki.
“Matendo ya mtu mmoja yasifanyiwe propaganda kama ni malengo ya taasisi. Nne, Nawashauri viongozi wa CHADEMA na hasa wanachama tutumie muda wetu kujenga mshikamano ndani ya chama. Fitna, majungu, uongo, uzandiki nk kamwe havijengi chama,” alisema.
Saanane ang’aka
Naye Saanane aliyedaiwa na gezeti hilo kuwa ndiye alikuwa ametumwa kumdhuru Zitto, alisema amesikitishwa jinsi lilivyoshiriki katika dhamira nzima ya kumchafua.
Akizungumza katika ofisi za Tanzania Daima jana, Saanane ambaye ni mjumbe wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) alisema kutokana na habari hiyo ameamua kukutana na wanasheria wake kuangalia hatua za kuchukua ili ukweli ubainike.
“Nasisitiza sijawahi kupanga kumuua mtu yeyote, sijawahi kutumwa kumuua Zitto Kabwe. Nimesikitishwa kuona chombo cha habari kikitumika kwa maslahi binafsi ya kuchafua watu kisiasa,” alisema.
Aliongeza kuwa mara zote alizokutana na Zitto, hawajawahi kufika katika Hoteli ya Lunch Time wakiwa pamoja kama ilivyoelezwa katika gazeti hilo.
Bashe anena
Ofisa Mtendaji Mkuu, New Habari 2006 Ltd, Hussein Bashe.
“Hilo la namna habari ilivyotoka mimi si mwandishi wa habari, ninachoweza kukuambia ni kwamba magazeti ya New Habari hayawezi kutumiwa na mtu yeyote kuzima au kufifisha suala la Kibanda,” alisisitiza.
Alisema kama kuna watu wanafanya siasa rahisi za kuyahusisha magazeti yao na mkakati wa kuzima suala la Kibanda watakuwa wamekosea kwa kile alichoeleza hawezi kuruhusu hali hiyo.
Alipoulizwa atachukua hatua gani kwa mhariri endapo itabainika gazeti hilo kutumika kwa lengo la kuwatoa watu katika kujadili madhila yaliyompata Kibanda, alisema hayo ni masuala ya ndani ambayo hayawezi kuwekwa hadharani pasipo kufuata taratibu.
0 comments:
Post a Comment