UJUMBE WA RAIS KIBAKI JUU YA UCHAGUZI MKUU WA KENYA.
RAIS wa Kenya Mwai Kibaki anayehudumu muhula wake wa mwisho , amewataka wakenya kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa njia huru na ya haki watakapokwenda kwenye debe Jumatatu.
Amesema kuwa wakenya watakuwa wanaandika historia ya nchi kwa kushiriki katika uchaguzi siku hiyo.
Akihutubia taifa kwa kupitia kwa televisheni ya taifa, Kibaki pia alisema kuwa serikali imehakikisha kuwa imedhibiti usalama kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa amani.
Aidha amewataka wagombea kukubali matokeo ikiwa watashindwa wakati akiwataka washindi kuwa wanyeyekevu katika kupokea ushindi.
Kibaki aliapishwa kwa muhula wa pili tarehe 30 mwezi Disemba mwaka 2007 baada ya uchaguzi uliokumbwa na utata mkubwa kiasi cha kusababisha maafa huku maelfu wakiachwa bila makao hadi leo.
Serikali ya Muungano iliundwa baadaye kama hatua ya kutuliza ghasia huku makubaliano yakitiwa saini ambapo Raila Odinga aliyekuwa mpinzani wake mkali akipewa wadhifa wa waziri mkuu Kibaki.
0 comments:
Post a Comment