HUKU ikiwa zimesalia chini ya saa 24 kabla ya zoezi la uchaguzi mkuu
kuanza nchini Kenya, makundi ya waangalizi nchini humo yameonyesha
kuridhika na jinsi maandalizi ya uchaguzi huo yanavyoendelea.
Katika kikao na waandishi wa habari, rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa
Mataifa ya Afrika, AU, Bi Nkosazana Dlamini Zuma amesema kuwa ujumbe
wake umekutana na Rais Mwai Kibaki na kuwahakikishia kuwa shughuli za
uchaguzi zitafanywa kwa njia ya amani.Aidha kiongozi huyo alikutana pia na viongozi wa vyama mbalimbali, maafisa wa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka na pia Inspekta Mkuu wa Jeshi la Polisi ambao wote walimwelezea kuridhika kwao na matayarisho ya uchaguzi.
"Wakenya wako tayari kwenda kwenye uchaguzi mnamo Jumatatu na ujumbe wetu umekutana na baadhi ya wagombea wa kiti cha Urais na wako tayari kupiga kura kwa amani na kukubali matokeo".
Bi Zuma aliandamana na aliyekuwa Rais wa zamani wa Msumbiji Joachim Chissano, ambaye ni kiongozi wa waangalizi wa Umoja wa Mataifa ya Afrika.
Alisema kulikuweko na hali ya taharuki katika maeneo kadha nchini kufuatia uvumi kuwa baadhi ya watu walikuwa wanasambaza vikaratasi kwa nia ya kueneza chuki, japo walipewa hakikisho kuwa suala hili lilikwisha dhibitiwa na polisi.
Chisano anahimiza wagombea wazingatie imani walionayo kwa katiba na kuwasilisha malalamiko yote kortini.
"Bi Dlamini ametoa mwito kwa Wakenya kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Jumatatu ili kumchagua kiongozi wampendaye.
Wakati huo huo amewahimiza wale wanaowania viti vya uongozi waitikie uamuzi wa wananchi".
Uhuru Kenyatta akiwa na mgombea mwenza William Ruto
"Washindi waitikie ushindi kwa unyenyekevu na kwa wale watakao
shindwa wakumbuke kwamba bado wanahitajika katika ujenzi wa
taifa.Tunatumai mambo yatakuwa shwari".
Zaidi ya waangalizi wapatao 20,000 kutoka makundi mbali mbali, miongoni mwao wale kutoka Jumuiya ya Ulaya, Umoja wa Kiafrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki wamo nchini Kenya kwa shughuli ya hii muhimu.
0 comments:
Post a Comment