CHAMA Cha Wananchi (CUF), kimesema vurugu zinazoendelea
bungeni zinasababishwa na Kambi Rasmi ya Upinzani inayoongozwa na Mwenyekiti wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kushindwa kujenga
hoja na mbinu za kuwabana wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba alisema wabunge wa Chadema wana tabia ya kufuata mfumo
wa kwenda bungeni na hoja zinazobeba chama chao na si za Watanzania wote kama
jinsi CCM wanavyofanya.
“Kambi rasmi ya upinzani imepoteza uwezo wa kujenga hoja
za mashiko na mbinu madhubuti za kuwabana wabunge wa CCM bungeni na badala yake
Chadema, wamekuwa na tabia mbaya ya kubeba chama chao,” alisema Profesa
Lipumba.
Alisema kambi rasmi ya upinzani pia imeshindwa kulinda
utaratibu mzuri wa kutetea masilahi ya umma bila jazba na hoja zenye mashiko
kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ilipokuwa ikiongozwa na CUF, Kiongozi huyo
alisema kambi ya upinzani inapaswa ijipange upya kwa utaratibu na mikakati
mizuri ya kuteta hoja za wananchi bila kuyumbishwa na wabunge wa CCM.
“Bunge usiwe uwanja wa kuonyesha mbwembwe za chama bali
uwe uwanja wa kutetea haki za wananchi, wabunge wanapaswa wabadilishe mitazamo
ya kuona bungeni ni sehemu ya kujionyesha kisiasa na chama chako kinafanya nini
nje ya Bunge,” alisema Lipumba.
Alisema viongozi wa Serikali wanapaswa kubadilika kuhusu
namna ya kutoa majibu bungeni.
Profesa Lipumba alisema mawaziri wengi wanakuwa wakitoa
majibu mepesi katika maswali ya msingi yanayoulizwa na wabunge wa
upinzani.
Alisema Bunge linatumia muda na pesa za walipakodi vibaya
kwa baadhi ya wabunge kuwa na ubishi usiokuwa na tija, kutoleana matusi na
wengine kuingilia hoja za wenzao bila sababu za msingi.
Profesa Lipumba pia alisema Spika wa Bunge, Anne Makinda
amepoteza uwezo wa kuliongoza Bunge.
0 comments:
Post a Comment