MATUKIO YA AFRIKA.
MUTULA Kilonzo seneta wa jimbo la uchaguzi la Makueni amekutikana akiwa
amefariki leo (Jumamosi 27.04.2013) akiwa katika nyumba yake ilioko
kwenye shamba la Maanzoni katika jimbo la Machakos.
Sababu ya kifo chake haijulikani isipokuwa taarifa za awali zimedokeza kwamba Kilonzo alikwenda kulala wakati wa usiku na kushindwa kuamka ilipofika saa nne asubuhi.
Wafanyakazi wake walishangaa kuona hakuamka hadi saa saba mchana na walilazimika kuvunja mlango ambapo waliukuta mwili ukiwa umelala kitandani.
Wakati akithibitisha kifo hicho Kaindi amesema wamejiandaa kuchukuwa hatua zote kujuwa sababu ya kifo hicho. Wafanyakazi waliwaambia polisi kwamba Kilonzo alichelewa kulala hapo jana usiku na alikuwa katika hali ya uchangamfu.
Musalia Mudavadi aliekuwa naibu waziri mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa iliopita ametuma rambi rambi zake kwa familia ya marehemu kwa kusema kwamba seneta Kilonzo alikuwa mwanasheria mahiri ambaye alikuwa akihusudiwa na jamii ya mawakili kutokana na hoja zake nzito za kisheria na kujenga vipaji vya wanasheria vijana.
Mudavadi amesema "katika seneti,Kilonzo angelikuwa anasubiriwa kuingiza hewa mpya kwa ahadi ya taifa kutekeleza wajibu wake." Watu wa kwanza kukimbia nyumbani kwa Kilonzo alikuwa ni Bw.Chris Musau mwenyekiti wa Manzoni Lodge ambaye pia ni shemegi wa waziri huyo wa zamani.
Kilonzo aliwahi kuwa waziri wa sheria na masuala ya katiba na baadae waziri wa ulinzi wakati wa utawala Mwai Kibaki.
Aliwahi pia kuzitumikia nyadhifa mbali mbali tokea ajiunge na siasa.
Mutula amejipatia elimu yake katika Shule ya Msingi ya Mboni na Shule ya Sekondari ya Machakos kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam hapo mwaka 1969 na kuhitimu kwa kujipatia Shahada ya Sheria ya Daraja la Kwanza.
Pia aliwahi kuwa waziri Maendeleo ya Jiji la Nairobi hadi pale alipochaguliwa kuwa waziri Sheria na Masuala ya Katiba hapo tarehe 4 mwezi wa Mei mwaka 2009 na baadae kuwa waziri wa elimu.
Huko nyuma aliwahi kuwa mwanasheria binafsi kwa rais mstaafu Daniel arap Moi. Mara ya kwanza Mutula Kilonzo aliingia bungeni akiwa mbunge wa kuteuliwa kwa tiketi ya chama cha KANU hapo mwezi wa Januari mwaka 2003.
Hadi kufa kwake tarehe 27 mwezi wa April 2013 alikuwa seneta wa jimbo la uchaguzi la Makueni lilioko mashariki ya Kenya.
0 comments:
Post a Comment