NDUGAI NAYE AONYWA KUACHA UCHOCHEZI BUNGENI, http://www.freemedia.co.tz
WANANCHI wa Njombe Kusini wamemshtaki Mbunge wao, Anne
Makinda, kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.Walisema kuwa licha ya CHADEMA kukusanya saini zao ili kulishinikiza Bunge kuilazimisha serikali kupunguza athari za ongezeko la gharama za maisha na mfumko wa bei, Makinda hana utamaduni wa kulitembelea jimbo lake mara kwa mara.
Dk. Slaa alipewa malalamiko hayo juzi katika uwanja wa NHC mjini hapa, wakati akihutubia mamia ya wananchi ikiwa ni ziara ya kuwasindikiza wabunge sita wa CHADEMA waliokuwa wamezuiliwa kuhudhuria vikao vitano vya Bunge kwa madai ya utovu wa nidhamu.
Wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina yao gazetini, walisema kuwa mbunge wao ambaye pia ni Spika wa Bunge, alifika katika kijiji chao mara moja tangu alipochaguliwa kwa kipindi cha tatu.
“Makinda ni mbunge wetu lakini hana desturi ya kulitembelea jimbo hili mara kwa mara kwa hiyo tunaomba muwe karibu na sisi, msije tu wakati mnapofukuzwa bungeni, mje mara kwa mara,” alisema mmoja wa wananchi.
Kutokana na madai hayo, Dk. Slaa alipoanza kuhutubia jukwaani alilazimika kuwauliza maswali wananchi ni lini mbunge wao aliwahi kufika jimboni kuwasikiliza.
“Hajawahi kuonekana hapa ila huwa tunasikia wakati mwingine kuwa yupo hotelini kwake kukusanya mapato…,” walijibu wananchi hao kwa sauti kubwa.
Dk. Slaa alisema kwa muda mrefu serikali ya Rais Jakaya Kikwete imekuwa ikitafuta mchawi huku ikitumia propaganada kuwa CHADEMA ni chama chenye migogoro badala ya kuangalia maisha ya Watanzania wanaoishi kwa kula kwa taabu.
“Nawaambieni wananchi wa Njombe Kusini kuwa propaganda zinazotolewa na serikali ya Kikwete kuwa CHADEMA ina migogoro ni uongo mtupu.
“CHADEMA haina migogoro wala haijawahi kuwa na migogoro. Hizo ni propaganda za mtu anayeshindwa hoja na kutetea watu wake waliomtuma kuwawakilisha,” alisema.
Alitaja sababu mojawapo ya uvunjifu wa amani nchini kuwa ni serikali yenyewe kushindwa kuwahudumia wananchi kwa haki stahiki.
“Malipo duni kwa wafanyakazi na watumishi mbalimbali ni chanzo cha kukosekana kwa amani.
Na adui wa serikali ni kushindwa kutekeleza mahitaji ya wananchi,” alisema.
Alieleza kuwa serikali imekuwa ya kiuendawazimu kutokana na uongo inaoueleza kwa wananchi kuhusu mambo yanayohusiana na maisha yao.
Mbowe amuonya Ndugai
Katika hatua nyingine, CHADEMA imemuonya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuacha kauli za uchochezi bungeni.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma.
Mbowe alizungumza na wanahabari ukiwa ni utaratibu mpya aliouanzisha wa kuelezea yaliyojiri bungeni kila mwisho wa wiki.
Alisema moja ya kauli ya kichochezi ya Ndugai ni ile aliyoitoa juzi kwamba adhabu ya kutolewa nje kwa siku tano kwa wabunge wa CHADEMA iongezwe.
Mbowe alisema kauli hiyo ni ya kuudhi na uchochezi na haikupaswa kutolewa na Ndugai ambaye amekuwa akilalamikiwa kukiuka katika kutoa adhabu kwa wabunge hao.
Wakati akiahirisha kikao cha Bunge juzi jioni, Ndugai alisema Bunge sasa limetulia baada ya wabunge sita wa CHADEMA kutolewa nje na amepata simu nyingi za pongezi.
“Waheshimiwa wanahabari, Aprili 4, mwaka huu, wakati akiahirisha Bunge la jioni, Ndugai alitoa kauli kwamba anapendekeza adhabu ya kutolewa nje kwa siku tano bila kufuatwa kwa kanuni za Bunge kuwa ingefaa iongezwe kwani sasa Bunge limetulia.”
“Kambi ya upinzani inaona kuwa hii ilikuwa kauli ya kuudhi na ya kuchochea,” alisema Mbowe.
Mbowe aliongeza kuwa wiki hii Bunge limetulia kutokana na ukweli kwamba kiti cha spika akijavunja kanuni wala kutoa maamuzi ya upendeleo, huku wabunge wa CCM hakuna hata mmoja aliyetukana wala kukashfu upinzani.
“Tunataka jamii ijue kwamba sisi hatuanzishi vurugu. Wakianza wao, au kiti cha spika kikivurunda na kupindisha haki, tunajibu na wakitulia basi tunatulia kama ilivyokuwa wiki hii,” alisema.
Kwa mujibu wa Mbowe, jambo jingine lililojiri wiki hii ni pamoja mwenendo wa Spika Anne Makinda katika kufikia uamuzi kwa kupiga kura za ndiyo au hapana kwa mdomo.
Alisema kambi rasmi inataka utaratibu wa kutumia mashine za kupiga kura zilizoko ndani ya ukumbi wa Bunge kwenye meza ya kila mbunge uanze kutumika.
Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai, alisema utaratibu huo wa kisasa utakuwa mbadala wa kura za ndiyo na hapana ili kuondokana na mikanganyiko ambayo haina sababu wakati mashine zipo na zimetumia gharama kubwa kuwekwa.
Akitolea mfano jinsi Spika Makinda alivyobabaika wakati wa kupitisha hoja ya Zitto Kabwe (CHADEMA) kutaka sh bilioni 75 zilizotengwa kwa ajili ya ruzuku ya mbolea ziingizwe kwenye miradi ya umwagiliaji, alisema spika alibabaika sana na hatimaye kuwapa ushindi wabunge wachache waliopingana na hoja ya Zitto.
“Pamoja na spika kuamua kwa kupiga kura za ndiyo na hapana ila waliokubaliana na hoja ya Zitto kwa sauti walishinda, lakini spika aliamua vinginevyo na kuwapa ushindi waliosema hapana,” alisema.
Hoja nyingine aliyoiibua Mbowe ni kwamba Waziri Mkuu Mizengo Pinda alishindwa kutoa majibu ya kuridhisha juu ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge yaliyotokana na ripoti ya David Jairo.
Alisema ingawa muuliza swali, John Mnyika, alilenga suala la Jairo, lakini serikali imekalia maazimio mengi ya Bunge ambayo sasa wanataka kusikia utekelezaji wake.
Mbowe aliyataja mengine kuwa ni pamoja na utekelezaji wa maazimio ya kashfa ya Richomnond, maazimio ya Kamati Ndogo ya Maliasili na Utalii na usafirishaji wa twiga na wanyama wengine hai nje ya nchi.
Alisema kibaya zaidi katika maazimio hayo ya maliasili na utalii, mhusika mmoja mkuu, Dk. Ladislaus Komba, aliteuliwa kuwa Balozi nchini Uganda wakati kamati ndogo ilikwisha kumtaja kuhusika na ufisadi wa kusafirisha wanyama hai nje.
Kwa mujibu wa Mbowe, maazimio mengine ni kuhusu hoja binafsi ya ardhi na mwisho ni utekelezaji wa azimio la Bunge kuhusu mabilioni ya fedha za Uswisi.
0 comments:
Post a Comment