NI VURUGU ZA WAKULIMA, WACHOMA NYUMBA 10 MOTO, ZIMO ZA MBUGE, MADIWANI NA VIONGOZI WA CCMMkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Said Mwema.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo NIPASHE imezipata na kuthibishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ludovick Mwananzila na Mitambo, tukio hilo limetokea juzi jioni katika kijiji cha Liwale B kilichopo kilomita 12 kutoka Liwale Mjini.
Chanzo cha machafuko hayo ni wananchi kupinga malipo ya awali ya korosho ya Sh. 250 kwa kilo badala ya Sh. 600 walizokuwa wakitegemea kulipwa kulingana na bei ya Sh. 1,200 kwa kilo iliyotangazwa na serikali mwaka jana.
Mitambo akizungumza na NIPASHE jana akiwa njiani kuelekea Liwale akitokea mjini Dodoma alikokuwa akihudhuria mkutano wa Bunge, alisema vurugu ziliibuka wakati wa malipo ya awamu ya pili ya korosho katika Chama cha Msingi cha Mazao cha Minali kilichopo kijiji cha Liwale B.
Alisema wakulima walifika katika ofisi za chama hicho kulipwa fedha zao na wakiwa hapo walielezwa na viongozi kuwa malipo watakayolipwa kwa kilo moja ni Sh. 250 jambo ambalo lilipigwa na wakulima ambao walihoji iweje walipwe kiasi hicho wakati serikali iliwatangazia kwamba watalipwa Sh. 1,200 kwa awamu mbili.
Mitambo alisema kutokana na vurugu hizo, nyumba zake mbili zilichomwa moto na kabla ya kuzichoma moto walianza kurusha mawe na baadaye walivunja milango na kuiba vitu kadhaa vya thamani.
Alisema wakati mawe yakirushwa ndani ya nyumba hizo, ndugu zake ambao walikuwamo ndani walifanikiwa kukimbia kunusuru maisha yao hali iliyotoa fursa kwa wahalifu kupora vitu na kutokomea kusikojulikana na baadaye kumwagia mafuta na kuzichoma moto.
Mbunge huyo alisema watu hao pia wamechoma moto nyumba ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Abbas Kigogolo yenye vyumba 11.
Aliongeza katika nyumba hiyo ya Mwenyekiti wa Halmashauri, pia watu hao walichoma moto pikipiki mbili, Power Tiller na kuua ng’omba 12 kwa kuzikatakata kwa mapanga.
Nyumba nyingine ambazo zimechomwa moto na wananchi hao ni ya Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya Liwale, Abdallah Chande; nyumba ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya, Mohamed Ngomambo; ya Mzee Lihomba ambaye ni mkwe Wa Diwani wa CCM wa kata ya Nangando, Hassan Miyao na yumba ya Mhasibu wa Chama cha Ushirika Ilulu, Mkungula.
Mhasibu huyo pia amepata athari kwa ng'ombe wake zaidi ya 10 kuibwa pamoja na duka ambalo lilivunjwa na watu hao kuporwa bidhaa zote.
Madiwani wa CCM ambao wamechomewa nyumba zao ni Hassan Miayao wa kata ya Nangami ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha msingi cha Minali, Hassan Mtako (kata ya Makanuo) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Umoja.
Wengine ni diwani wa kata ya Liwale Mjini, Ahmed Salehe, wa Viti maalum Amina Mnoche na wa kata ya Likongewele, Mussa Mnkoyage ambaye pia maduka yake mawili ya pembejeo yamevunjwa na bidhaa zilizokuwamo ndani kuibwa.
Akizungumza na NIPASHE jana jioni, Kamanda Mwakajika, alisema hali imekwishatulia wilayani humo na kwamba Kamati ya Ulinzi na Usalama ilikutana kujadili vurugu hizo.
Hata hivyo, alisema asingeweza kueleza kwa kina kuhusu tukio hilo kwa kuwa bado viongozi walikuwa kwenye vikao.
“Kwa sasa tupo kwenye kindumbwindumbwi siwezi kuzungumza lolote, naomba tuwasiliane baadaye, kwa muda huu niache kwanza,” alisema Mwakajinga.
Taarifa zaidi zilieleza kwamba wananchi hao walikuwa na silaha mbalimbali za jadi zikiwamo pampu za baiskeli na petroli.
Inadaiwa kwamba nyumba 11 za kuishi na maduka 13 yaliyokuwa na bidhaa mbalimbali yameteketea.
Akisimulia mkasa huo, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika, Hassani Mpako, alisema akiwa nje ya nyumba yake ghafla alijikuta akivamiwa na kundi kubwa la watu wakiwa na pampu za baiskeli ambazo ndani yake waliwekwa mafuta ya petroli kisha kuelekezwa kwenye nyumba yake na kulipuliwa.
Alisema watu hao walielekeza pampu hizo zilielekezwa kwenye paa la nyumba yake na walipozipuliza ghafla nyumba ikawaka.
Alisema kabla ya kitendo hicho, alipoona kundi hilo la watu alichukuwa tahadhari kwa kuitaka familia yake kuondoka eneo hilo la nyumba yao na kwenda kusikojulikana ili kunusuru maisha yao.
Kwa upande wake, Meneja wa Chama cha Ushirika Mkoani Lindi, Hamza Mkungura, alithibitisha kufanyiwa fujo hizo na kutaja mali zake zilizoteketezwa kuwa ni ng’ombe 10 wa maziwa, nyumba moja ya kulala na maduka manne yakiwamo ya dawa muhimu.
Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Ephem Mbaga, alipoulizwa kwa njia ya simu, alisema yupo nje ya kituo chake cha kazi, lakini akathibitisha kupokea taarifa ya matukio hayo.
SAKATA LAIBUKIA BUNGENI
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Zainabu Kawawa, ameitaka serikali kutengeneza utaratibu ambao utawezesha wakulima kulipwa Sh. 400 walizopunjwa katika malipo ya korosho.
“Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa masikitiko yangu juu ya tukio lililotokea jana (juzi) usiku katika wilaya ya Liwale, wakulima wa korosho wameghadhabika sana, kulikuwa na mapambano makali kati yao na polisi na hatimaye walichoma moto baadhi ya nyumba za viongozi,” alisema.
Kawawa alisema sababu hiyo inatokana na ukweli kwamba waliahidiwa wangelipwa fedha za mauzo ya korosho Sh. 1,200 ambapo awamu ya kwanza walilipwa Sh. 600 na ya pili wakalipwa Sh. 200.
“Kwa maana hiyo, jumla wamelipwa Sh. 800 … sasa wakulima hao wanadai ile tofauti ya Sh. 400,” alisema na kuongeza:
“Nimezungumza na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, amenieleza kwamba bei ya korosho imekuwa ikibadilika.”
Kutokana na hali hiyo, aliiomba serikali itoe majibu ni kiasi gani ingeweza kufidia Sh. 400 ili mkulima alipwe Sh. 1,200.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima alisema: “Mheshimiwa Naibu Spika ili tukio la Liwale ni tukio la kusikitisha sana kwa sababu hii tabia ya wananchi ya kuchukua sheria mkononi na kwenda kuchoma nyumba za viongozi … ni lazima tukubaliane kuwa kuna vitu vimejificha humu.”
Malima alisema sehemu zote ambazo zinalima korosho likiwamo jimbo lake la Mkuranga kuna matatizo ambayo yamesababisha korosho kutokuuzwa.
“Kwingine kuna matatizo ya vyama vya ushirika, kwingine kuna matatizo ya wanunuzi … kwa hiyo tunasema kwamba serikali tutakwenda kote ambako kuna matatizo ya zao la korosho, tutapitia na tutakutana na wananchi kujua tatizo nini,” alisema Malima na kuongeza:
“Kuna maeneo mengine tatizo linatokana na vyama vya ushirika. Unaweza kukuta hao hao viongozi wa vyama vya ushirika ndiyo wanawahimiza watu kuchoma nyumba ili kufunika madhambi yao.”
Kuhusu waliochoma nyumba, alisema wataonana na Waziri na Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment