Baadhi
ya Ng’ombe sita mali ya John Theodore Ghumpi wa kijiji cha Minyinga
jimbo la Singida mashariki,waliokatwa katwa juzi na diwani wa CHADEMA
kata ya Mungaa Matheo Alex kwa kile kilichodaiwa kuwa ni ugomvi wa
kugombea ekari 50 za mbuga.
Mkulima
na mfugaji wa kijiji cha Minyinga kata ya Mungaa jimbo la Singida
Mashariki, John Theodore Ghumpi akionyesha Ng’ombe wake aliyekatwa kwa
shoka na diwani wa kata ya Mungaa Matheo Alex kwa tuhuma ya kugombea
mbuga ya ekari 50.
Kaimu
OCD wilaya ya Ikungi, Deo Batete akiangalia kwa masikitiko Ng’ombe wa
John Theodore Ghumpi aliyekatwa shoka na diwani wa kata ya Mungaa.Wa
pili kushoto ni mkuu wa kituo kidogo cha polisi kata ya Mungaa D/S/SGT
Elibariki Urio.
Sehemu
ya shamba la Alizeti mali ya mkulima John Theodore Ghumpi mkazi wa
kijiji cha Minyinga linalodaiwa kufyekwa na diwani Matheo Alex.
Baadhi
ya wakazi wa kijiji cha Minyinga kata ya Mungaa waliofika nyumbani kwa
John Theodore Ghumpi ambaye Ng’ombe wake sita wanadaiwa kukatwa katwa
kwa shoka na diwani Matheo Alex na vijana wake wawili .Pia diwani Matheo
anadaiwa kufyeka shamba la Alizeti la ekari mbili na nusu.(Picha na
Nathaniel Limu).
Na
Nathaniel Limu
DIWANI wa
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Mungaa jimbo la Singida
Mashariki, Matheo Alex amewaacha midomo wazi wapiga kura wake na wananchi wa
kata hiyo kwa kitendo chake cha kukata kata ng’ombe sita kwa shoka na kufyeka
ekari mbili na nusu za shamba la Alizeti.
Imedaiwa
kuwa diwani huyo kijana ametenda kitendo hicho ,kutokana na ugomvi wa kugombea
mbuga ya ukumbwa wa ekari 50.
Ng’ombe
hao waliokatwa katwa na diwani Matheo akishirikiana na watoto wake, watatu wana
mimba, wawili wananyonyesha na moja ni dume wote ni mali ya John Theodore
Ghumpi mkazi wa kijiji cha Minyinga kata ya Mungaa.
Ng’ombe hao na ekari la
shamba la Alizeti lililofyekwa vyote vina thamani ya zaidi ya shilingi 4.5
milioni.
Tukio
hilo la kusikitisha, limetokea mei 13 mwaka huu saa 5.00 asubuhi katika kijiji
cha Minyinga jimbo la Singida Mashariki.
Diwani
Matheo ambaye miaka miwili iliyopita aliwahi kushitakiwa katika mahakama ya
hakimu mkazi mjini Singida kwa kosa la kuvunja/kuharibu kwa makusudi kizuizi
(geti) la kudhibti ushuru wa mazao ya misitu na kumpiga mlinzi wa geti
hilo,anatuhumiwa pia kufyeka ekari mbili na nusu za shamba la Alizeti.
Akisimulia
mkasa huo wa kusikitisha, Joseph Albino (mtoto wa kaka yake mkubwa na John
mwenye ng’ombe zilizokatwa) amesema siku ya tukio alipita jirani na kaya ya
diwani Matheo na kukuta diwani akiwa kwenye kikao na watu wasiopungua kumi.
Akifafanua,
Albino amesema alipoonwa na diwani, diwani huyo aliwaamrisha waliokuwa kwenye
kikao hicho,kuwa waanze kumuuwa yeye (Albino).
“Ghafla
diwani Matheo na kundi lake walinyanyuka huku wakiwa wamebeba shoka, panga na
hengo na kuanza kunifukuza,wakati wakiendelea kunifukuza njiani walikuta kundi
la ng’ombe za John zikichungwa na ndipo walipoanza kuzikata kata wakiongozwa na
diwani wetu”, amesema kwa masikitiko makubwa.
Naye mke
wake John, Mary John amesema aliposikia Albino akipiga yowe, haraka alikimbilia
katika eneo la tukio na kukuta diwani akiendelea kukata kata Ng’ombe wao bila
huruma.
“Huku
nikipiga yowe, nilimwomba diwani Matheo aache kuwakata ng’ombe na badala yake
wamkate yeye hadi afe kwa madai kuwa wanakata Ng’ombe ambao hawana hatia
yoyote. Bahati nzuri waliacha zoezi la kukata Ng’ombe wetu”,amesema kwa uchungu
mkubwa.
Kwa
upande wake mwenye mali hizo shamba la Alizeti na Ng’ombe, John Theodore
Ghumpi amesema siku ya tukio hakuwepo nyumbani alikuwa Singida mjini kikazi.
Amesema
alipigiwa simu na kuelezwa juu ya tukio hilo mbaya na hivyo alirudi haraka
nyumbani kwake katika kijiji cha Minyinga.
John
alisema anahisi diwani Matheo amefanya kitendo hicho kwa makusudi kutokana na
ugomvi wao wa kugombe mbuga yenye ukumbwa wa ekari 50.
“Katika
ugomvi huu wa muda mrefu,mwaka 1997 hadi 2007,tumekuwa tukifanya kesi katika
mahakama mbalimbali na mwaka 2007,tulimshinda katika mahakama kuu Dodoma na
aliamriwa kuondoka katika mbuga hiyo”amesema na kuongeza.
“Cha
kusikitisha ni kwamba pamoja na mahakama kuu kutoa amri hiyo halali mwaka 2007
aondoke katika eneo hilo,hadi sasa bado ameng’ang’ania eno letu hataki
kuondoka.
Tumefanya juhudi kubwa kuomba kuomba mamlaka zinazohusika ikiwa ni
pamoja na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Singida,lakini hadi sasa juhudi hizo
hazijazaa matunda.
Mkulima
huyo na mfugaji,alisema jambo jingine linalomsikitisha zaidi ni kauli ya mbunge
wa jimbo la Singida mashariki,Tundu Lissu kumpigia simu mkuu wa kituo cha
Makiungu akiagiza diwani Matheo Alex aachiwe kwa dhamana na kwamba atamtetea
katika kesi ya kukata kata ng’ombe na kufyeka shamba la alizeti.
“Kama
kweli yeye Tundu Lissu ni mbunge wa wakazi wa jimbo la Singida mashariki ambaye
wajibu wake ni pamoja na kuwaongoza wapiga kura na wananchi, kutenda mambo mema
na yanayozingatia sheria, nasubiri kwa hamu kama atabariki kitendo cha diwani
Matheo kwa kumtetea katika kitendo chake hiki cha kinyama”,alisema huku machozi
yakimtiririka.
Kamanda
wa jeshi la polisi mkoa Singida.ACP Geofrey Kamwela alikiri kupokea taarifa ya
tukio lililofanywa na diwani Matheo la tuhuma ya kukata kata Ng’ombe sita na
kuharibu ekari mbili na nusu za shamba la alizeti.
“Kwa sasa
vijana wangu wapo eneo la tukio.Wakishamaliza uchunguzi nitatoa taarifa kamili
ili wananchi waweze kujua undani wa tukio hilo mbaya”amesema kamanda huyo wa
mkoa.
0 comments:
Post a Comment