RAIS JAKAYA KIKWETE.
SHULE
zinazoendeshwa na kumilikiwa na taasisi na watu binafsi, zimetakiwa
kurekebisha ada zao ili Serikali iangalie uwezekano wa kushirikiana nazo
katika kulipia. Ushauri huo umetolewa na Rais Jakaya Kikwete katika
mkutano wa Chama cha Wamiliki wa Vyuo na Shule Binafsi (TAMONGSCO)
uliofanyika hivi karibuni katika ukukbi wa Mkapa mjini Mbeya.
Hatua
hiyo ilitokana na mapendekezo ya Tamongsco yakitaka Serikali ipeleke
wanafunzi kwao na kuwalipia ada, kupitia mfumo wa ushirikiano wa Sekta
Binafsi na ya Umma (PPP).
Katika
mapendekezo yao, walitaka Serikali ipunguze msongamano wa wanafunzi
waliozidi katika shule zake, kwa kuwapeleka katika shule binafsi.
Akijibu hoja hizo, Rais Kikwete, aliyealikwa kuhudhuria, alisema wazo
hilo ni zuri lakini lina changamoto.
“Nimesikiliza
kwa makini sana hoja yenu ya kutaka kushirikiana na Serikali kuondokana
na msongamano wa wanafunzi katika baadhi ya shule zake.
“Natambua
kwamba wakati Serikali inahangaika kupunguza msongamano kwenye shule
zake, baadhi ya shule zenu zina madarasa yaliyo wazi na zingependa
kuletewa wanafunzi na Serikali,” alisema Rais.
Rais
alifafanua kwamba pamoja na uzuri wa wazo hilo, suala hilo lina
changamoto zake kutokana na ukweli kwamba gharama katika shule hizo ni
kubwa, hivyo wazazi au Serikali hawataweza kumudu.
Ombi la JK Kutokana
na hali hiyo, Rais Kikwete katika mkutano huo wenye kaulimbiu ya ‘Changamoto na fursa zilizopo katika ushirikiano baina ya sekta ya umma
na isiyo ya umma katika utoaji wa elimu bora’, alitaka walimu hao
kujadili tatizo hilo la ada kubwa.
“Nina
ombi moja kwenu ambalo napenda mlijadili kwenye mkutano wenu.
Ombi
lenyewe si geni, linahusu ada kubwa zinazotozwa na shule au vyuo vyenu.
Wapo wananchi wengi ambao wangependa sana kunufaika na elimu nzuri
mnayoitoa, lakini wanashindwa kutokana na ada inayotozwa kuwa kubwa.
“Sisemi
ada zenu zifanane na za shule za Serikali, lakini baadhi ya shule na
vyuo vyenu vinalalamikiwa na wananchi kwa kutoza ada kubwa na kwamba
hazitabiriki kwani hupandishwa wakati wowote,” alisema Rais Kikwete.
Tathmini
Pamoja na ombi hilo kwa Tamongsco, Rais Kikwete alisema Serikali kupitia
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imeliona hilo na imeamua
kulifanyia kazi.
Alisema tathmini ya gharama halisi za uendeshaji kwa
mwanafunzi mmoja, itafanywa ili kutoa ushauri stahiki kwa wamiliki wote
wa shule au vyuo kuhusu kiwango cha ada.
Alirejea
kauli yake, kwamba elimu ni huduma muhimu na haki kwa mtoto na si vema
kugeuzwa kuwa biashara ya kuleta faida kubwa.
Alisema hadi sasa uthamini
kwa vyuo vya elimu ya juu umeshafanyika na mapendekezo ya gharama
halisi yameandaliwa.
Rais
alisema tayari hatua za kumpata mtaalamu elekezi zimefanyika, kwa ajili
ya kutathmini gharama za uendeshaji kwa shule za sekondari.
Hata hivyo,
aliwahakikishia Tamongsco kuwa Serikali itaendelea kuwaunga mkono na
kushirikiana nao, ili kuwawezesha vijana wengi zaidi wa kitanzania
kupata elimu.
“Tutaendelea kupokea na kufanyia kazi ushauri wenu ili kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji kwenye sekta ya elimu.”
Sera ya
Elimu Wakati huo huo, Serikali imesema Sera mpya ya Elimu inatarajia
kuanza kutumika mwishoni mwa mwaka huu ambapo pia mitaala ya elimu
itapitiwa upya, ili kwenda sambamba na sera hiyo.
Rais
Kikwete alisema mchakato wa kutunga sera hiyo mpya ya elimu baada ya ile
ya mwaka 1995, umefikia hatua za mwisho na kinachosubiriwa sasa ni
maoni ya wabunge ili sera ikamilishwe.
“Naamini
kabla ya mwisho wa mwaka huu, sera itakuwa tayari kutumika, tunaamini
kuwa sera hiyo mpya italeta mabadiliko katika uendeshaji wa mifumo yetu
ya elimu nchini, na kutoa majibu kwa maswali mengi,” alisema.
Kwa
mujibu wa Rais Kikwete, nafasi ya sekta binafsi katika kuchangia
maendeleo ya elimu nchini itafafanuliwa kwa upana na kina zaidi.
Alifafanua,
kwamba mitaala mipya itakayotokana na sera hiyo, itakwenda sambamba na
hali ya sasa na mahitaji ya maendeleo nchini na duniani, huku
akiwahakikishia kuwepo kwa ushirikishaji wa wadau, wakiwamo wa sekta
binafsi katika suala hilo.
Idara ya Elimu Kuhusu Idara ya Ukaguzi wa
Elimu, Rais alisema itapewa kipaumbele na Serikali inatambua kuwa hali
ilivyo sasa hairidhishi.
“Serikali
imeanza na inaendelea kuchukua hatua thabiti kuimarisha ukaguzi wa
shule na vyuo nchini, miongoni mwa mambo yanayofikiriwa kufanywa ni
kubadili Idara ya Ukaguzi kuwa taasisi inayojitegemea na kuiwezesha kwa
rasilimaliwatu, vitendea kazi na fedha,” alisema.
Alisema
anaamini kwa njia hiyo, wataimarisha utendaji wa ukaguzi na matokeo yake
yataonekana kwa muda mfupi na kuwakumbusha kuwa mkaguzi wa kwanza wa
shule ni Mkuu wa Shule.
0 comments:
Post a Comment