HABARILEO.
BAADHI ya watu wanaopinga juhudi za uongozi wa Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC) kukabiliana na ubadhirifu, wamepanga kumwua Mkurugenzi Mkuu
wa Shirik
a hilo, Nehemia Mchechu, imeelezwa.
Akichangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi mjini hapa jana, Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya
(CUF), alifichua njama hizo akiwanyooshea vidole mafisadi waliokuwa
wakitumia nyumba za NHC kujinufaisha kifedha.
Kutokana na kuwapo njama hizo, Mbunge huyo aliiomba Serikali kuchukua
hatua za haraka za kumpa ulinzi mkurugenzi huyo ili asidhuriwe na watu
hao.
Sakaya alisema vitisho hivyo pia vimeelekezwa kwa watendaji wengine
wa shirika hilo wanaopambana na ufisadi huo.
“Mafisadi hawa walikuwa wamezoea kugeuza nyumba za NHC kama miradi
yao kwa kupangisha wananchi wa kawaida na kuwanyonya na wakati mwingine
kuzitumia kwa biashara.
“Kelele hizi ambazo zinasikika hata humu ndani ya Bunge zinatokana na
hasira za mafisadi hawa walioshughulikiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NHC na
watendaji wake. Wanawapelekea watendaji hawa ujumbe wa kila aina wa
vitisho, ikiwamo kumtishia Mkurugenzi kifo,” alisema Sakaya.
Akizungumzia gharama katika nyumba hizo, alisema hatua hiyo inatokana
na Serikali kuondoa mkono wake katika ujenzi wa nyumba na kulifanya
shirika hilo kutumia fedha zake lenyewe kujiendesha.
“Kwa vile hakuna fedha za Serikali pale, ni lazima NHC wajiendeshe
kibiashara, vinginevyo watakufa. Ni lazima nyumba zao ziuzwe kulingana
na bei ya soko, ili kuleta ushindani sokoni,” alisema.
Alisema miongoni mwa vitu vinavyoongeza gharama za nyumba hizo ni
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo kama itaondolewa na Serikali,
itapunguza bei ya nyumba hizo.
Makilagi alia
Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Makilagi ambaye pia ni Katibu wa Umoja
wa Wanawake Tanzania (UWT-CCM), aliiomba Serikali kufanya uamuzi mgumu
wa kufukuza kazi watumishi wa Idara ya Ardhi wanaojihusisha na rushwa na
kujilimbikizia mali, vikiwamo viwanja.
Akichangia hotuba hiyo, Makilagi alisema ingawa Serikali ya CCM
imeamini viongozi na kuwapa madaraka katika sekta ya ardhi, kuna
walioamua kuichafua Serikali kwa kujihusisha na rushwa na ufisadi.
“Naiomba Serikali iwafukuze kazi mara moja maofisa hawa.
Kitendo cha
kuwahamisha maeneo ya kazi hakimalizi tatizo, bali kinazidi kuliongeza,
maana watendaji hao wanapohamishiwa kwenye maeneo mengine huendelea na
ubadhirifu,” alisema Makilagi.
Aliitaka pia Serikali kufanya juu chini ipate fedha za kupima ardhi
nchi nzima akisema hatua hiyo itapunguza migogoro ya ardhi na kupanga
mipango mizuri ya matumizi ya ardhi kuliko sasa.
Mbunge wa Kibaha Vijijini, Jumaa Abuu (CCM) aliitaja Kampuni ya
Mohamed Enterprises (METL), akisema imepora maeneo ya wananchi katika
kata ya Soga Kipengele jimboni mwake na kuzusha mgogoro mkubwa huku
Serikali ikishindwa kuchukua hatua stahiki.
Mbunge wa Igunga, Dalali Kafumu (CCM) alisema ni lazima Serikali
itenge fedha ili kuipata Idara ya Upimaji na Ramani ili iboreshe ramani
badala ya kutenga fedha kwa upimaji wa ardhi peke yake.
Alichachamalia viongozi wa Idara ya Ardhi, Igunga akisema wanapora
maeneo ya wananchi na kujimilikisha au kuyauza kwa watu wenye fedha na
kuwaacha wananchi wakiteseka.
Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Mary Mwanjelwa (CCM) aliitaka Serikali
kusaka na kuwafikisha mahakamani viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya
Ilala na wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
waliopindisha sheria na kuruhusu ujenzi holela wa jengo la ghorofa
lililodondoka Dar es Salaam hivi karibuni. Bajeti hiyo ilipitishwa jana.
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment