WAHUSISHWA NA MAUWAJI, BIASHARA YA MIHADARATI NA ULAJI WA RUSHWA
http://www.mtanzania.co.tz
IGP SAID MWEMA.SASA ni jambo lililo dhahiri kuwa ndani ya Jeshi la Polisi kuna mtandao wa uhalifu unaoratibiwa na kutekelezwa na Askari Polisi wenyewe.
Mlolongo wa tuhuma za mauaji, ulaji rushwa, kubambikia raia kesi na hata ushiriki wa biashara ya kulevya ambao umekuwa ukiliandama jeshi hilo kwa muda mrefu, huku likikosa majibu ya kujinasua na kashfa hizo, unadhihirisha pasipo shaka kuwepo kwa mtandao huo.
Takwimu zilizotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), hivi karibuni zinaliweka jeshi hilo katika sura mbaya kuliko wakati mwingine wowote, tangu kuundwa kwake na baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wam
ekuwa wakieleza kuwa hata kuchafuka kwa sifa ya Serikali kwa wananchi, kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na mwenendo mbaya wa Jeshi la Polisi.
Kwa mujibu wa takwimu za LHRC za Septemba mwaka 2012, jumla ya raia 24 waliuawa na polisi kwa kupigwa risasi katika mikoa mbalimbali nchini, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.
Mfululizo wa matukio hayo yameifanya Tanzania ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikisifika kuwa kisiwa cha amani, kuingia katika orodha ya nchi zenye sifa mbaya ya vyombo vyake vya usalama wa raia, kuhusika na utesaji na uporaji wa mali walio na dhamana ya kuwalinda.
Aidha, mwenendo huo wa polisi umelifanya litizamwe kwa sura ya kuogopwa na wananchi ambao kimsingi wanapaswa kulitazama kama kimbilio lao dhidi ya wahalifu.
Utesaji na uuaji.
Kwa mujibu wa rekodi zilizopo, zinaonyesha kuwa Jeshi la Polisi hapa nchini limekuwa likinyooshewa vidole na raia kwa kuhusika na mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi.
Mwangosi aliuawa mwaka jana mkoani Iringa akiwa mikononi mwa polisi, ambao walimshambulia kwa silaha mbalimbali kabla ya mmoja wao kumlipua kwa bomu na kuutawanya kabisa mwili wake.
Tukio jingine la mauaji ambalo polisi wanadaiwa kuhusika ni la mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, ambaye alipigwa risasi kadhaa mwilini usiku wa manane wakati akimsindikiza mmoja wa jamaa zake aliyekuwa naye kwenye kikao cha harusi.
Kamanda Barlow aliuawa usiku wa kuamkia Oktoba 13, mwaka jana, eneo la Kitangiri jijini Mwanza na uchunguzi wa kikosi maalumu cha makachero wa polisi unaeleza kuwa upo uwezekano mauaji hayo yalifanywa na vikundi vya kihalifu vya ndani ya Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na mitandao ya kihalifu ya nje na ndani ya nchi.
Sababu iliyotajwa awali kwa makundi hayo kushiriki mauaji ya Kamanda Barlow, ni wadhifa aliokuwa amefikia kabla ya kuuawa kumpa nafasi kubwa ya kuteuliwa kuwa mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, lakini hivi karibuni yameibuka madai kuwa kamanda huyo aliuawa na askari wenzake aliowadhulumu mgao wa fedha haramu.
Tukio jingine la mauaji lililotikisa jamii ambalo polisi wanadai kulitekeleza ni la mauaji ya kinyama ya mwandishi wa habari aliyekuwa na makazi yake mkoani Mwanza, Richard Masatu.
Masatu alitekwa na kushambuliwa vibaya na watu wasiojulikana ambao walimpeleka hospitali na kumtekeleza lakini zipo taarifa zinazoeleza kuwa muda mfupi kabla ya kuteswa kwake, alikuwa akinywa pombe na baadhi ya wanausalama wa mkoani Mwanza.
Ingawa iliundwa tume ya polisi ya kuchunguza kuuawa kwake, taarifa ya tume hiyo ilitofautiana na taarifa ya awali ya madaktari waliochunguza chanzo cha kifo chake.
Rushwa.
Tuhuma nyingine ambazo zimekuwa zikiliandama Jeshi la Polisi, ni askari wake kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Wafuatiliaji wa mambo wamekuwa wakieleza kuwa rushwa mbaya inayodaiwa kulichafua jeshi hilo ni ya askari wa barabarani ambao wanafahamika zaidi hivi sasa kama ombaomba, kwa kukusanya chochote kile kutoka kwa madereva wa magari ya abiria na yale ya mizigo.
Zipo taarifa kuwa askari wa usalama barabarani, huelekezwa na wakuu wao wa kazi kuchukua chochote kwa madereva kutokana na ugumu wa maisha na kuwapelekea mgao.
Mwaka 2008 aliyekuwa Mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Jerry Muro, aliripoti matukio mbalimbali ya namna askari wa polisi wa barabarani wanavyochukua rushwa.
Baada ya kazi hiyo ya Muro, Jeshi la Polisi lilichukua hatua na kuwasimamisha kazi askari wake 11 katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro walionaswa na Muro katika mikanda ya video wakipokea rushwa.
Sambamba na hilo, yapo pia madai kuwa rushwa imeghubika katika usaili wa vijana wanaoomba kujiunga na Chuo Cha Polisi (CCP), mkoani Kilimanjaro.
Magendo
Tuhuma ya kujihusisha na biashara ya mihadarati, nayo imekuwa ikiliandama Jeshi la Polisi.
Katika matukio kadhaa, Askari Polisi wamepata kunaswa wakishiriki biashara ya mihadarati na ama kuiba vidhibiti ambavyo ni mihadarati vilivyohifadhiwa kama vielelezo katika vituo vya polisi.
Polisi pia wanatajwa kushirikiana na wafanyabiashara wa mihadarati kufanya biashara hiyo na kwamba wakati mwingine wamekuwa wakiwasindikiza wauzaji wanapokuwa wakisafirisha unga.
Katika kashfa hii, wiki iliyopita askari 16 walikamatwa kwa tuhuma za kuwasaidia wafanyabiashara wakubwa kupitisha biashara ya magendo wilayani Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
Inaaminika kuwa mtandao wa uhalifu wa polisi umekuwa ukivusha mali za magendo na mihadarati kupitia bandari bubu zisizo rasmi, zilizo katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Kubambikia kesi
Katika mlolongo huu wa tuhuma, ipo pia inayowahusisha polisi na ubambikiaji raia kesi kwa lengo la kuwalazimisha kuwapatia fedha.
Wiki mbili zilizopita, askari watatu mkoani Morogoro walikamatwa kwa tuhuma za kukutwa na fuvu la kichwa cha binadamu, ambalo walikuwa wanalitumia kubambikia raia kesi.
Askari hao wa wilayani Kilosa wanadaiwa kujaribu kukitumia kichwa hicho kutaka kumbambikia kesi mfanyabiashara mmoja mkoani humo, kwa lengo la kutaka awapatie kiasi kikubwa cha fedha.
Fuvu hilo linadaiwa ni la mtu aliyeuawa hivi karibuni kati ya Wilaya za Kilosa na Mvomero mkoani humo, hadi sasa bado haijajulikana kama fuvu la mtu huyo lilitokana na mauaji yaliyopata kutekelezwa na polisi au la.
Desemba mwaka 2011, mkoani Arusha, polisi walidaiwa kuiba dola za Marekani 50,000, sawa na Sh milioni 90, zilizopatikana kwa mmoja wa majambazi watatu waliohusika katika uporaji kwa kutumia usafiri aina ya pikipiki, maarufu jijini Arusha kwa jina la ‘toyo’.
Fedha hizo ziliyeyuka mikononi mwa polisi katika mazingira ya kutatanisha.
0 comments:
Post a Comment