POLISI saba kutoka wilayani
Kasulu, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, iliyoanza
kikao chake mjini Kigoma leo na kusomewa mashitaka ya kuua kwa kukusudia. Mbele
ya Jaji Sam Rumanyika, askari Polisi hao walidaiwa kuwa Agosti 6, 2011
walimpiga
na kumuua kwa makusudi Festo Stephano, mkulima na mkazi wa Kijiji cha
Rungwe mpya wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Waliopandishwa kizimbani na
kusomewa mashitaka yao ni pamoja na Baraka Hongdi, Koplo Mawazo, Koplo Swahib,
Koplo Charles, Koplo Shamsi, Koplo Jerry na Koplo Amrani ambao kwa pamoja
walikana mashitaka.
Baada ya kukana mashitaka,
kesi hiyo ilianza kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa Jamhuri kuanza kutoa
ushahidi wao, ambapo shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, Masumbuko Stephano,
aliieleza Mahakama kwam
ba askari hao walikusudia kufanya mauaji hayo.
Masumbuko aliieleza Mahakama
kwamba siku ya tukio, alikamatwa pamoja na marehemu na mgambo wa kijiji, na
kuwekwa katika mahabusu ndogo katika Ofisi ya Mtendaji wa Kata.
Alidai baada ya kufika,
askari hao walianza kuwapiga kwa kutumia vitako vya bunduki, fimbo na chupa za
bia, hali iliyosababisha wapatwe na maumivu makali.
Shahidi
huyo alidai kuwa baada ya kupigwa na kukaribia kupoteza fahamu, polisi hao
waliwavua nguo, wakawafunika na turubai ndani ya gari ambapo baadaye walinunua
magunia ya mkaa na kuwakandamiza na magunia hayo.
Shahidi wa pili katika kesi
hiyo, Andrea Sama, alidai kwamba askari hao walikusudia kufanya mauaji siku
hiyo, kwani licha ya kutoa kipigo pia waliwavua nguo na kuwaingiza miti kwenye
sehemu zao za haja kubwa.
“Mheshimiwa Jaji kwa kweli
nilishuhudia vitendo vya askari hao kwa macho yangu, na nilishindwa kuamini
kama jambo hilo linafanyika kwenye ardhi ya Tanzania au tuko nchi nyingine,
maana unyama uliofanywa na askari polisi hao huwezi kudhani kama ni walinzi wa
amani katika nchi hii,” alidai Sama.
Kesi hiyo itaendelea
kusikilizwa mfululizo hadi kutolewa hukumu, ambapo mwanasheria mwandamizi wa
Serikali, Juvelin Rugaihuruza, alidai kuwa upande wa Jamhuri ambao ndiyo
mlalamikaji, unatarajia kuwa na mashahidi 12 na vielelezo viwili.
Washitakiwa hao wanatetewa
na Mwanasheria, Method Kabuguzi, kutoka Kampuni ya Uwakili ya Kigoma Law
Chamber and Advocate ya mjini Kigoma.
0 comments:
Post a Comment