HABARILEO.SPIKA WA BUNGE ANNA MAKINDA.Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
WAZIRI wa Wizara ya Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Samuel Sitta ameeleza kukerwa na kibonzo (katuni)
kilichochapishwa na gazeti la Sunday Nation la nchini Kenya hivi
karibuni kikilibeza na kulidhalilisha Bunge la Tanzania.
Kabla ya kuwasilisha hotuba yake ya
bajeti kwa mwaka ujao wa fedha bungeni mjini hapa jana, Waziri Sitta
alisema kibonzo hicho kilililenga katika kulichafua Bunge na kulishushia
hadhi mbele ya jamii jambo ambalo halikubaliki.
Waziri Sitta alisema kibonzo hicho
kilionesha wabunge wa Bunge la Tanzania wakiwa wamelewa, wan
avuta bangi,
wamevaa nguo za nusu uchi na matendo mengine ya ovyo ovyo.
“Kitendo hiki kilichofanywa na gazeti hili ni kitendo kibaya na kinachoweza kuleta mfarakano baina ya nchi hizi mbili jirani.
Hatuwezi kukubali kitendo chochote cha kulidhalilisha Bunge letu tukufu kama ilivyofanywa na gazeti hili,” alionya Sitta.
Wakati huo huo sakata la Rais wa Uganda,
Yoweri Museveni kuamuru kufungiwa kwa gazeti la kila siku la The Daily
Monitor kwa kufichua njama za Rais huyo za kumuandaa mtoto wake Muhoozi
Kainerugaba kuwa Rais wa nchi hiyo jana lilizua vuta nikuvute bungeni.
Vuta nikuvute hiyo ilianza pale Msemaji
Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu Mapitio ya Utekelezaji wa
Bajeti kwa mwaka ujao wa fedha kwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Raya Ibrahim Khamis (Viti Maalum- Chadema), alipotoa kauli ya
kulaani kitendo hicho cha Rais Museveni ndani ya Bunge.
Akisoma maoni hayo ya kambi ya upinzani,
Raya alisema sasa hivi kumezuka wimbi la kukandamiza uhuru wa vyombo
vya habari katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Alisema matukio ya kuvifungia vyombo vya
habari na kuwadhuru waandishi wa habari kwa sababu za kulinda maslahi
ya watawala yanazidi kuongezeka kwa kasi kubwa katika nchi wanachama wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Hata hivyo Raya alipomaliza kusoma
hotuba yake hiyo, alisimama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Maafa na Bunge, William Lukuvi, akitumia kanuni ya 68 ya Bunge akiomba
mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama kuhusiana na hotuba
hiyo.
Kutokana na kanuni hiyo, Lukuvi alimtaka
Mhagama akemee kauli hiyo dhidi ya Rais Museveni akisema kitendo hicho
kinaweza kuharibu uhusiano baina ya Tanzania na Uganda kutokana na
Museveni kukifahamu vizuri Kiswahili.
Hata hivyo kabla ya Mwenyekiti wa Bunge
kutoa mwongozo wake kwa jambo hilo alisimama Mbunge wa Ubungo, John
Mnyika (Chadema) akinukuu kanuni namba 63 kifungu kidogo cha 2, ambapo
alisema amesimama ili kumuelekeza Mnadhimu Mkuu wa Serikali bungeni
(Lukuvi) kuhusiana na mwongozo aliouomba.
“Mheshimiwa Mwenyekiti (Mhagama) kanuni
hii inatamka wazi kwamba Mbunge atasimama bungeni na kuzungumzia habari
ambayo imeandikwa au kutangazwa na vyombo vya habari.
Msemaji wa Kambi ya Upinzani
amezungumzia jambo ambalo lilitangazwa na BBC (Shirika la Utangazaji la
Uingereza), “ alisema Mnyika.
Hatua hiyo ilimfanya Mhagama kuahidi
kutoa ufafanuzi wa suala hilo katika kikao cha jioni jana, ingawa
alisema kitendo cha Mnyika kumjibu Waziri Lukuvi kwa mwongozo aliotaka
Kiti cha Spika kumjibu kilikuwa ni kukiuka kanuni za Bunge.
0 comments:
Post a Comment