Golikipa Juma Kaseja wa Simba, akiokoa mpira wa kono ulioelekezwa golini kwake wakati wa mchezo na dhidi ya JKT RUVU ambapo Simba ilishinda bao 3-0 uliofanyika siku ya jumatano April 18, 2012.
Kipa aliyefunguliwa mlango kuondoka Mtaa wa Msimbazi,
Juma Kaseja amesema taarifa za kutemwa kwake anazisikia kwenye vyombo
vya habari tu, na kwamba hata kama ni kweli hazijamshtua kwa vile
anaamini kiwango chake bado kimesimama kwenye mstari.
Kwa zaidi ya wiki sasa, vyombo vya habari vimekuwa
vikiandika taarifa zilizokosa maelezo ya kina kuhusu kutemwa kipa huyo
namba moja wa Simba na nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa
Stars.
Kaseja ambaye kwa sasa yuko Kigoma kwa ajili ya
mapumziko, alisema anafahamu kuwa mkataba wake na Simba ulishakwisha
tangu baada ya kumalizika kwa msimu uliopita, hivyo yeye ni mchezaji
huru.
“Nasikia tu nimetemwa Simba, lakini kweli sijapata
barua na hata kama ningejulisha, nisingeshangaa kwa sababu mkataba
wangu na Simba ulishamalizika,” alisema Kaseja.
Mlinda mlango hiyo mwenye rekodi ya pekee nchini,
alisema hana ugomvi na uongozi wa Simba pamoja na kutomjulisha kama
hawatamwongezea mkataba.
“Sijawahi hata siku moja kujulishwa kuwa
sitaongezewa mkataba mpya baada ya kumalizika uliotangulia. Hakuna
kiongozi aliyeniambia lolote zaidi ya kusikia kwenye vyombo vya habari
kwamba sitakiwi,” alisema Kaseja.
“Kwa sasa siwezi kuzungumza mengi kwa vile sina
haki hiyo kwa sasa, muda utafika nitaongea. Napumzika huku pia
nikiendelea kufanya mazoezi kwa sababu soka ndiyo ajira yangu,”
aliongeza Kaseja.
Kaseja aliyeidakia Simba kwa miaka tisa mfulilizo
tangu mwaka 2003, hakuwa tayari kuweka bayana mwelekeo wake kama uamuzi
wa kutemwa Simba utabaki palepale.
Alisema: “Siwezi kusema lolote kwa sasa, ila muda
ukifika nitaweka wazi mambo yangu. Naamini bado nina uwezo na kamwe
sitakata tamaa hata kama nitaondoka Simba.”
Tangu kutangaza kutemwa kwa Kaseja zaidi ya wiki
moja iliyopita, taarifa za ndani kutoka Simba zinadai kuwa uamuzi huo
umezaa mgogoro chinichini baina ya viongozi.
Ingawa Mwenyekiti wa Simba Aden Rage, aliwahi
kukaririwa akisema kipa huyo hatavaa jezi za Msimbazi msimu ujao,
viongozi wenzake wanapinga uamuzi huo.
Kaseja aliwahi kulalamikiwa na mashabiki wa Simba
mwishoni mwa msimu uliopita wakimtuhumu kucheza chini ya kiwango hali
iliyosababisha kufungwa mabao ya kizembe.
0 comments:
Post a Comment