HABARILEO.Naibu Katibu Mkuu CCM, Vuai Ali Vuai
Katibu Mkuu wa Chama cha
Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad.
CHAMA Cha Mapinduzi Zanzibar kimemtaka Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad kuacha kufanya usaliti wa kisiasa na kuwasemea Wazan
zibari katika suala zima la mchakato wa Katiba, ikiwemo mambo ya Muungano.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za CCM mjini hapa, Naibu Katibu Mkuu CCM, Vuai Ali Vuai alisema hakuna kikao rasmi kilichofanyika na kufikia makubaliano ya kuwasemea Wazanzibari katika suala la Muungano.
Alisema CCM inajua kwamba upo mchakato wa katiba ambao unakwenda kwa mujibu wa utaratibu uliopo, ambapo kwa sasa rasimu ya mabadiliko hayo ipo katika hatua za mwisho kuzinduliwa, hivyo hakuna sababu ya kuanza kufanya mikutano ya hadhara yenye lengo la kuwahamasisha wananchi.
Alisema kinachofanywa na kiongozi huyo kwa sasa ni kutaka kuwachonganisha viongozi wakuu wa serikali pamoja na wananchi ili wajitayarishe kufanya fujo na vurugu wakati matakwa yao yasipofikiwa.
“Chama Cha Mapinduzi kinamshangaa sana Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif kwa kauli zake kwamba asilimia 66 ya Wazanzibari wanataka muungano wa mkataba....amekutana nao lini na katika kikao gani.....kwa mfano sisi CCM tunayo sera yetu na msimamo wetu katika suala hilo,” alisema.
Alimtaka kiongozi huyo kuacha kuitumia kamati ya maridhiano kama ndiyo jukwaa la kuwasemea Wazanzibari na kukihusisha CCM. Vuai alifafanua na kusema kwamba Tume ya Maridhiano haina baraka za chama na haitambuliki na kusisitiza hicho ni kikundi cha watu kwa ajili ya kujitafutia ulaji.
“Chama Cha Mapinduzi hakitambui kamati ya maridhiano ambayo inaonekana kujivika joho la vyama vya siasa....kamati hiyo kwa upande wa CCM ameichagua nani na majukumu yake yapi’?” Alihoji.
Akijibu kauli za katibu mkuu wa CUF, Vuai alisema viongozi wastaafu wa CCM akiwemo rais Amani Abeid Karume pamoja na Dk Salmin Amour ni watiifu kwa chama na kamwe hawawezi kwenda kinyume na sera za chama hicho katika Muungano.
Alisema viongozi hao kwa mujibu wa chama, ni washauri wakuu wa Baraza la Wazee wakipewa heshima zote za kichama.
Akizungumza juzi katika mkutano wa hadhara, Katibu Mkuu wa CUF, Hamad (ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar ) alisema viongozi wote wakuu wastaafu wa Zanzibar wametamka bayana kuwepo kwa dola huru ya Zanzibar wakati walipotoa maoni yao mbele ya Tume ya Jaji Warioba.
Vuai aliendelea kumjibu Hamad kwamba msimamo wa CCM upo wazi kwamba haishawishiki hata siku moja kuvunja Muungano ambao upo kwa ajili ya mustakabali wa wananchi wa pande mbili hizi.
Alisema utafiti unaonesha wazi kwamba Zanzibar ndiyo inayonufaika zaidi na Muungano huo katika maeneo mbali mbali, ikiwemo suala la kufanya biashara.
Vuia alitoa mfano wa Bodi ya Mikopo ya Zanzibar ambapo katika mwaka 2011 ilitoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya vyuo vikuu 1,000, wakati Bodi ya Mikopo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitoa mikopo kwa wanafunzi 800.
0 comments:
Post a Comment