Waziri Mkuu, Mh. Peter Mizengo Pinda.IGP SAIDI MWEMA.FREEMAN MBOWE MWENYEKITI WA CHADEMA.
WAKATI
ikibainika kwamba bomu lililorushwa na kulipuka Arusha limetengenezwa
China, Polisi imewataka viongozi wa Chadema kuwasilisha ushahidi
walionao wa mtu aliyelirusha.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema jana kwamba wataalamu wamebaini
kwamba bomu hilo limetengenezwa katika nchi hiyo ya Mashariki ya Mbali,
baada ya kutembelea majeruhi waliolazwa katika hospitali za Selian, St
Elizabeth na Mount Meru jijini hapa.
Wakati Polisi ikisema watu watatu wamekam
atwa wakituhumiwa kuhusika
na tukio hilo, Pinda alisema Jeshi hilo kwa kushirikiana na timu ya
wataalamu wa mabomu inafanya uchunguzi kujua ni nani anayeingiza mabomu
hayo nchini na kwa sababu ipi.
Aidha, Kamanda wa Operesheni Maalumu, Kamishna Paul Chagonja alisema
polisi wako tayari kupokea ushahidi wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
Lema na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wasipouwasilisha,
wataangaliwa kisheria.
Juzi Mbowe aliwambia waandishi wa habari kuwa ana ushahidi wa picha
za video zinazoonesha aliyerusha bomu hilo na atauweka hadharani.
Akiwa Hospitali ya Selian, Pinda alisema Serikali inafanya uchunguzi
juu ya tukio hilo kubaini mabomu hayo yanapita mipaka gani ikizingatiwa
Arusha ni mpakani na nchi jirani.
“Tunafanya uchunguzi wa tukio hili ili kujua ni akina nani
wanapitisha mabomu haya kutoka China maana Arusha iko karibu na mipaka …
natoa pole kwa wana Arusha, wana Chadema na viongozi wao kwa tukio
hili, lakini nasema Serikali haitamwonea haya mtu yeyote aliyehusika na
tukio hilo, kwani ni la kinyama,” alisema Pinda.
Alisema tukio hilo ni la pili jijini hapa likitanguliwa na la kwanza
lilitokea eneo la Olasiti katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph
Mfanyakazi na kuua watu watatu na kujeruhi wengine kadhaa.
Kwa mujibu wa Pinda, upelelezi wa tukio hilo unaendelea na baada ya
taarifa kupatikana, timu ya uchunguzi ilikwenda nchi za nje na kurudisha
nchini baadhi ya watuhumiwa wanaodhaniwa kufanya tukio lile.
Alisema Serikali ilipoamua kutangaza Sh milioni 10 kwa mtu
atakayetaja mhusika inaonesha dhamira ya makusudi ya kukerwa na tukio
hilo.
Aliomba wote wanaofahamu mhusika wa tukio hilo atoe taarifa Polisi na
kumwomba Mbowe kama ana ushahidi autoe ili ukweli ujulikane.
Alisisitiza, kwamba Arusha ni mji wa kitalii na pia wananchi wanaishi
na kufanya shughuli zao, hivyo haupaswi kuonekana kama usio na amani na
kusababisha watalii na mikutano kushindwa kufanyika na kuathiri watu
hususan katika sekta ya utalii.
Waathirika CCM
Watoto ndugu Fatma na Farida Jumanne waliopelekwa Hospitali ya Aga
Khan, Nairobi, wamedaiwa kuwa ni watoto wa baba ambaye ni kada wa CCM.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, baba wa watoto hao, Jumanne
Ali mkazi wa Soweto, alisema hakuwa nyumbani wakati watoto hao
walipokwenda kwenye mkutano huo Jumamosi.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, Magesa Mulongo, taarifa zilizopatikana zilidai kuwa watoto hao wanaendelea vizuri .
Aidha, timu ya madaktari kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI) na
wa Jeshi kutoka Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam waliwasili
juzi jijini hapa kufanya uchunguzi wa kitaalamu kwa mtoto Fahad Jamal
(7) ambaye yuko chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu ( ICU)
na wagonjwa wengine waliolazwa hospitali hizo tatu za hapa.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa CCM) Abdulrahman Kinana ambaye
alitembelea majeruhi waliolazwa, aliiomba Serikali kushirikiana na
Polisi kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo ili lisijirudie
baadaye.
Mbowe, Lema wabanwa Baadhi ya wanasheria waliozungumza na gazeti
hili, wakiwemo ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini, walisema
kitendo cha mtu kuwa na taarifa kuhusu mtuhumiwa na akashindwa kuzitoa
ni kosa kisheria.
“Unaweza kushitakiwa kwa kosa la kuzuia askari kufanya kazi yake.
Kama una taarifa kuhusu mtuhumiwa fulani lakini ukashindwa kuzitoa, ni
sawa na kuzuia mshitakiwa kukamatwa,” alisema mmoja wa wanasheria hao.
Mwanasheria wa Kujitegemea, Martin Geofrey alisema Sheria ya Makosa
ya Jinai kifungu namba 7 kinampa jukumu mwananchi kutoa taarifa Polisi
kuhusu utendaji wa kosa kama limetendeka au linataka kutendeka. Pia
polisi ana jukumu la kuzifanyia kazi taarifa hizo na endapo mwananchi
atatoa taarifa na polisi asifanyie kazi, ni kosa kisheria pia.
Watatu mbaroni
Chagonja alisema tangu tukio hilo litokee Polisi, inashikilia watu
watatu ambao hata hivyo hakutaja majina yao kwa sababu za kiusalama.
Alisema wanaendelea kuwahoji na ikithibitika maelezo ya ushahidi wao
yanajitosheleza, watafikishwa kwenye vyombo vya sheria na kama polisi
wakiona maelezo hayajitoshelezi kisheria, wataachiwa.
Vurugu hospitalini
Polisi jana ilizuia ibada ya mazishi kwenye uwanja wa AICC eneo la
Soweto kutokana na uongozi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (AICC)
kutokuwa tayari uwanja wao kutumika kwa shughuli hiyo.
Baada ya Polisi kuzuia taratibu za maombolezo hayo na wananchi
kuamriwa kuondoka eneo hilo, wafuasi wa Chadema walikwenda kujikusanya
nje ya geti la Hospitali ya Selian alikokuwa Waziri Mkuu, Pinda na
viongozi wengine.
Bila kujali hali za wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo, wafuasi hao
walipaza sauti ya ‘Peoples, Power (Sauti ya Umma)’. Baada ya muda,
Waziri Mkuu aliingia ndani ya gari lake huku ulinzi ukiimarishwa na
kuondoka.
Wana Chadema hao waliokuwa wameshika matawi ya miti mikononi,
waliendelea kuzunguka katika viunga vya Jiji la Arusha wakidai wanamtaka
Mbunge wa Arumeru Mashariki Joshua Nassari huku wakiimba kuwa polisi ni
wauaji.
Mabomu yarindima
Mabomu ya machozi yalifyatuliwa jana na polisi katika uwanja wa
Soweto ili kutawanya wafuasi wa Chadema baada ya kukaidi amri ya
kutofanya maombolezo katika uwanja huo.
Polisi waliamua kufyatua mabomu saa 9.45 alasiri na kufanya wafuasi
wa chama hicho kutawanyika baadhi yao wakiacha pikipiki na magari na
wengine wakilala chini na watoto waliokuwa na wazazi wao. Katika viwanja
hivyo yaliko makazi ya wapangaji wa AICC , moshi ulifuka na kuingia
kwenye nyumba.
Hali ilikuwa mbaya kwa watoto waliokuwa wakitoka shuleni. Kabla ya
kurushwa, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alipanda kwenye gari la
matangazo la chama hicho na kusema Mbowe na Lema hawawezi kwenda Polisi
kutoa ushahidi kwa sababu hawana imani na Polisi kwani ndio watuhumiwa
namba moja, vinginevyo watakutana mahakamani.
Alisema Chagonja hawezi kufanya uchunguzi wa tukio hilo bali ushahidi wa Chadema watautoa kwenye Tume Huru ya Majaji.
Nassari lawamani
Wakati huo huo, Chagonja alisema walipokea malalamiko kutoka kwa
mwananchi wa Wilaya ya Monduli akidai Nassari ndiye aliyemfanyia fujo
kabla ya mbunge huyo kudai amepigwa na kuumizwa.
Hata hivyo, alisema wanafuatilia tukio hilo na ikithibitika Nassari
ndiye aliyeanzisha fujo hizo eneo la Makuyuni, atachukuliwa hatua za
kisheria. Maziko ya watu waliokufa kwenye tukio hilo yatafanyika baada
ya uchunguzi wa kitalamu wa madaktari kukamilika.
Walitarajiwa kuagwa kwenye viwanja hivyo, kabla ya kusafirishwa
kwenda Kilimanjaro (Judith Moshi) , Lushoto (Amir Ally) na Tabora
(Ramadhan Juma) kwa maziko. Mlipuko huo ulitokea Jumamosi iliyopita
wakati Chadema ikihitimisha kampeni zake za udiwani.
Kama kusingetokea mlipuko huo, uchaguzi mdogo wa madiwani ungefanyika
Jumapili kwenye kata nne za Themi, Kaloleni, Elerai na Kimandolu.
Tendwa aonya
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa ameonya vyama vya
siasa kuacha kuchanganya wananchi kwa kunyoosheana vidole, na badala
yake CCM na Chadema wapeleke ushahidi wao kwa vyombo husika.
Aidha amesema ofisi yake haijafikia mahali pa kutaka kufuta vyama
hivyo, kama inavyopendekezwa, kwa kuwa hatua hiyo itakuwa ni sawa na
kufanya mapinduzi ya nchi kwa kalamu.
Mbali na hilo, ameahidi kukutana na Polisi, Chadema na wadau wengine
kulitafutia ufumbuzi suala hilo kwa kile alichosema hali ambayo nchi
imefikia sasa si nzuri na unahitajika ushirikiano kwa ajili ya kuokoa
mustakabali wa nchi.
Tendwa alisema hayo Dar es Salaam jana, wakati akizungumzia masuala
ya kisiasa yanayotokea nchini na kwamba nchi inakokwenda si kuzuri.
“Hali ya kisiasa imebadilika … lakini ifahamike kuwa wa kuijenga nchi
ni mwananchi na wa kuibomoa ni mwananchi pia…ninasikitishwa sana na
tukio la Arusha na ni wajibu wangu kulaani kama kiongozi wa vyama vya
siasa,” alisema Tendwa na kuongeza kuwa mkutano wa Chadema ulikuwa
muhimu kwa kampeni, hivyo wote wameumizwa; Chadema na yeye, lakini Taifa
limeumizwa zaidi.
Alisema, “zipo sheria na ni lazima zifuatwe, vyama vya siasa
visichanganye wananchi kwa kunyoosheana vidole kuwa anayehusika ni
Chadema au CCM kwani vipo vyombo vya upelelezi, vipeleke ushahidi ili
magaidi waliohusika wakamatwe.
“Wananchi wanababaishwa, hali ya siasa ya Arusha si nzuri ni gharama
kwa Serikali kurudia uchaguzi na pia ni gharama kwa wananchi kwa hofu,
kwani Chadema na CCM ni vyama vikubwa…pelekeni ushahidi msijaze hofu
wananchi na Serikali isaidie kuwakusanya na kuwafikisha mahakamani ili
vyama visilete uchochezi,” alisema Tendwa.
Alisema siasa si kupigana mabomu na suala hilo haliko kabisa katika
sheria za vyama vya siasa, viongozi na wananchi watafute suluhu na Ofisi
ya Msajili itafanya hivyo kwa kukutana na wadau hao ili kuliweka sawa.
“Mwaka ujao kutakuwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwa hali hii
si kutakuwa na mapanga? Tusiruhusu hilo…vyama vieleweshwe kuhusu
ustaarabu…matukio ya Arusha yamesikitisha sana, Tume lazima isimamie
maadili na tusitupie mtu lawama, wasaidiane kwani hapa tulikofikia
hapafai hata kidogo na haijulikani nani anasema kweli na nani mwongo,”
alisema Tendwa.
Wagomea Bunge
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Mkurugenzi wa Habari
na Uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema chama chake kitaendelea
kususia vikao vya Bunge Dodoma hadi maombolezo ya waliopoteza maisha
katika mlipuko wa bomu yatakapomalizika.
Pia Chama hicho, kilimtaka Rais Jakaya Kikwete kuunda Tume ya kijaji
kwa ajili ya kuchunguza mfululizo wa matukio ya mauaji yaliyotokea
nchini ikiwa ni pamoja na kuvunja Tume maalumu iliyoundwa na Mkuu wa
Jeshi la Polisi, Said Mwema, kwa kuwa hawana imani nayo.
“Sisi tumeamua kurudi kwa wananchi, watakaobaki kwenye vikao vya
Bunge sijui wanamhudumia nani, tunaomba wananchi washiriki nasi katika
maombolezo haya kwa kuchangia familia zilizoathiriwa na tukio hili,
lakini pia wamtumie Mwema ujumbe wa kumtaka awajibike,” alisema Mnyika.
Alisema wameamua kuchukua hatua hiyo ya kutohudhuria vikao vya Bunge
kwa madai kuwa wakiingia ni sawa na kusaliti wananchi na kutowatendea
haki walioathirika kwa kujeruhiwa na kufa na mabomu Arusha.
Mnyika aliendelea kusisitiza, kwamba Chadema wana ushahidi wa mkanda
wa video unaomwonesha aliyerusha bomu katika mkutano huo na kwamba
alivaa sare za Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na kwamba
baada ya kurusha bomu hilo, alitaka kushambuliwa na wananchi lakini
polisi walimtetea na kukimbia naye kituo cha Polisi.
“Katika mazingira kama haya si suala la kutupiana mpira sisi Chadema
na CCM, lakini katika hili la Arusha ushahidi wa mkanda jamani tunao,
hata ile Tume ya IGP ilikuja tukawapa ushirikiano lakini matokeo yake
vijana wetu wamekamatwa na kuteswa, ndiyo maana hatuna imani na Tume
hii,” alisisitiza.
Wabunge wanne mbaroni
Wakati tunakwenda mitamboni jana taarifa kutoka mjini Arusha
zilieleza kuwa wabunge wanne wa Chadema wamekamatwa na polisi kwa
kufanya mkusanyiko usio halali kwenye viwanja vya Soweto jijini Arusha.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Operesheni Maalumu Paul Chagonja aliwataja
wabunge hao kuwa ni Tundu Lissu (Singida) Mustafa Akunai (Mbulu), Said
Arfi (Mpanda Mjini) pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu , Joyce Nkya.
Aidha Chagonja alisema sababu iliyopelekea polisi kurusha mabomu hayo
ya machozi ni baada ya vijana wa Chadema kuanza kumshambulia Mkuu wa
Polisi wa Wilaya (OCD) wa Arusha ambaye hakumtaja jina na mara polisi
walipoona OCD huyo anashambuliwa ndipo walipoanza kutumia mabomu ya
machozi kutawanya wabunge hao pamoja na wafuasi wa chama hicho ambao
walikusanyika viwanja hivyo bila ya kuwa na kibali.
Alisema Polisi walishauriana na Mwenyekiti wa Chadema Taifa na Mbunge
wa Hai Freeman Mbowe kwamba wanachama wake waondoke uwanjani hapo kwa
sababu wenye uwanja huo ambao ni Kituo cha Mikutano Cha Kimataifa Arusha
(AICC) walizuia kulitumia eneo hilo kwa kufanyia maombolezo ya watu
waliouawa kutokana na mlipuko wa bomu.
Maombolezo yaliyopangwa kufanyika viwanjani hapo na walitegemea Mbowe
atawatangazia wafuasi hao watawanyike badala yake Mbowe hakuwatangazia
wafuasi kutawanyika bali waliendelea na mkutano.
"Tulimwambia (Mbowe) awatawanye wafuasi wake lakini badala ya
kuwatawanya alifanya mkutano usio rasmi hivyo tumekamata wabunge hawa na
bastola moja aina ya bereta iliyokuwa na risasi kumi na risasi moja
ilitumika na ilikuwa bado ina moto pia tunawatafuta Lema(Godbless Mbunge
wa Arusha Mjini ) na Mbowe ambao walikimbia,’’ alifafanua Chagonja.
Habari hii imeandikwa na Veronica Mheta, Arusha, Halima Mlacha, Lucy Lyatuu na Flora Mwakasala.
CHANZO HABARILEO.
0 comments:
Post a Comment