
TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ juzi usiku imepoteza mchezo wake muhimu wa kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil, baada ya kufungwa mabao 2-1 na Morocco. Kila mmoja angependa kuona timu yetu inashinda mchezo huo ndio maana walifanya kila aina ya maarifa angalau kutoka sare.
Licha ya hujuma mbalimbali zilizolalamikiwa na viongozi wetu pamoja na makocha, bado tunayo nafasi ya kujifunza mengi katika soka kwa ujumla.
Sisi MTANZANIA tunaamini licha ya kufungwa na Morocco, bado tunashika nafasi ya pili tukiwa na pointi 6, huku Morocco ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 5 na Gambia ikishika mkia katika kundi C.
Ivory Coast inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi 10, ambazo ni tatu mbele ya Taifa Stars baada ya kuifu
nga Gambia mabao 3-0.
Katika hali yoyote ushindani uliojitokeza, ni wazi wachezaji wetu wameumizwa na pengine kuchanganywa na matokeo hayo.
Lakini tunaungana na Watanzania wote kuwapongeza wachezaji wetu kwa kupata pointi 6 hadi sasa huku tukibakiza mechi mbili muhimu ambazo zinaweza kubadilisha matokeo.
Stars itamenyana na Tembo wa Ivory Coast kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kisha itakwenda kupambana na Gambia nchini humo.
Katika mechi zote mbili Stars ina uwezo wa kufanya mambo makubwa zaidi ya mechi zilizopita. Tunafahamu wachezaji wetu hawakuweza kutulia zaidi hasa baada ya kushuhudia beki wao Aggrey Morris akipewa kadi nyekundu kwenye pambano la juzi nchini Morocco.
Lakini bado wachezaji wetu walituonyesha ujasiri wa hali ya juu wa kupambana na kufanikiwa kufunga bao moja la kufutia machozi.
Kucheza mechi dhidi ya Morocco huku zaidi ya dakika 50 timu ikiwa pungufu, ni jambo linalostahili pongezi kwa vijana wetu.
Sisi MTANZANIA tunapenda kuwahakikishia wachezaji, viongozi, makocha na wadhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro kuwa tutakuwa bega kwa bega kuhakikisha wachezaji wetu wanaendeleza moyo wa kujituma na kufuata maelekezo ya wakufunzi wao.
Mechi na Morocco si mwisho wa mashindano au Stars imetolewa. Tunayo nafasi kubwa ya kuendelea kupambana huku tukikabiliwa na mashindano ya CHAN, pamoja na AFCON kwa miaka ijayo.
Wachezaji wetu wachukulie kufungwa na Morocco ni changamoto ya kufanya vema siku zijazo na tunaunga mkono juhudi na maarifa yao.

0 comments:
Post a Comment