
WANACHAMA wa CCM wanaofanya kampeni za chini kwa chini kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, wataanza kudhibitiwa kuanzia ngazi za chini kich
ama, imeelezwa.
Katika kuhakikisha udhibiti huo unafanikiwa, chama hicho kitafungua majalada maalumu ambamo taarifa za kila mmoja atakayekaidi amri hiyo taarifa zake zitahifadhiwa.
Utaratibu huo unalenga kukusanya ushahidi wa wakaidi wa agizo la chama hicho la kuwataka kutofanya kampeni za aina yoyote hadi muda mwafaka utakapofika.
Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula alipotoa ufafanuzi wa masuala yanayoendelea katika chama hicho na kueleza kuwa wanachofuata ni kanuni na si uamuzi wa mtu.
Alisema wanafuatilia wanachama wao kwa kuweka kumbukumbu kuanzia kata ili kuangalia wanaoanza kampeni mapema za udiwani, ubunge na urais.
“Katika majalada hayo tutaweka kumbukumbu ya aliyofanya ikiwamo sehemu ya kurasa kwenye magazeti na ikiwa alifanya kampeni au mkutano watakuwa na ushahidi kwa kuhoji waliohudhuria na kuweka kumbukumbu,” alisema.
Mangula alisema wanafanya hivyo ili kupata ushahidi watakapokuwa wakifanya uamuzi kwa mujibu wa kanuni, ikiwa ni pamoja na kutokubaliwa kugombea nafasi yoyote ndani ya chama kwa kipindi ambacho Kamati Kuu itaona kinafaa.

0 comments:
Post a Comment