Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali nchini imesema karibu nusu ya watu
waliojitokeza kupima vinasaba (DNA) ili kubaini uhalali wa watoto wao,
vipimo vimeonesha si wazazi halisi wa watoto waliopimwa.
Takwimu
hizo ni kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2010, ikionesha
kuwa, asilimia 48.32 ya wazazi 'wanalea' watoto wasio wa kwao wakati
asilimia 51.68 ndio wazazi halali.
Hayo
yameelezwa jana na Mkuu wa Kitengo cha Makosa ya Jinai, Vinasaba na
Baiolojia wa ofisi hiyo, Gloria Machuve katika mkutano na wanahabari
kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Dar es Salaam.
Ingawa
hakutaja idadi kamili ya waliojitokeza kupima DNA, alisema idadi
hutofautiana mwaka hadi mwaka. Ili kufanya vipimo vya DNA, wazazi
hulazimika kulipia Sh 100,000.
Machuve alisema kazi ya DNA si kutambua watoto halali na wasio halali pekee, bali vipimo hivyo vina umuhimu mkubwa kwa jamii.
Alitoa
mfano kuwa, matumizi ya Teknolojia ya vinasaba vya binadamu yamewezesha
kesi mbili za mauaji ya vikongwe na albino kutolewa hukumu katika mikoa
ya Shinyanga, Kagera na Sumbawanga baada ya kufanyika kwa uchunguzi
katika matukio manane.
Aidha,
alisema katika majanga mbalimbali yaliyokumba nchi ikiwa pamoja na
milipuko ya mabomu yaliyotokea Mbagala, Dar es Salaam mwaka 2010
walitambua mabaki ya askari sita ambao baadaye walichukuliwa na ndugu
zao na kuzikwa.
Alitolea
pia mfano wa tukio la moto katika Shule ya wasichana ya Idodi mkoani
Iringa ambako licha ya kuungua vibaya, miili ya wanafunzi 12
ilitambuliwa hivyo makaburi yao kutambuliwa. Katika Jengo la ghorofa
lililoporomoka mtaa wa Kisutu mwaka huu, marehemu 23 walitambulika.
Aidha,
katika ajali ya Ndege ya Comoro mwaka 2010 mabaki ya miili ya marehemu
25 ilitambuliwa huku katika masuala ya uhamiaji teknolojia hiyo
ilitumika kudhihirisha hawana uhusiano na wananchi wa Tanzania.
Machuve
alisema katika masuala ya ubakaji na mimba za utotoni teknolojia hiyo
imesaidia kuwa fikisha wahusika mahakamani pamoja na katika wizi wa
kutumia silaha.
About mtanda blog
Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
0 comments:
Post a Comment