ULINZI MKALI KILA KONA, TANZANIA YAKOSOLEWA.
HAYAWI hayawi sasa yamekuwa baada ya Rais wa Marekani, Barack Obama, kuwasili nchini jana kuanza ziara yake ya kiserikali ya siku mbili akitokea Afrika Kusini.
Rais Obama ambaye alipata mapokezi makubwa ya wananchi na viongozi mbalimbali, walioongozwa na Rais Jakaya Kikwete, aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere saa 8:36 akiongozana na mkewe Michelle pamoja na watoto wao wawili, Sasha na Malia.
Mara baada ya kuteremka kwenye ndege yake ya Air Force One, Rais Obama, alikumbatiana na Balozi wa Marekani nchini, Alfonso E. Lenhardt na mkewe, kisha akasalim
iana na mwenyeji wake, Rais Kikwete na Mama Salma.
Rais Obama alikwenda moja kwa moja kwenye jukwaa dogo kisha kupigiwa nyimbo mbili za Tanzania na Marekani zilizoambatana na mizinga 21, kisha akakagua gwaride na vikundi vya ngoma za asili.
Huku akishindwa kujizuia kutokana na burudani hiyo, Rais Obama alijikuta akisakata ngoma na mwenyeji wake, Rais Kikwete na baadaye alisalimiana na viongozi kadhaa wa kiserikali na mabalozi kisha viongozi hao walielekea Ikulu kwa mazungumzo.
Wakati wote ulinzi mkali wa maofisa usalama wa Marekani kwa kushirikiana na wale wa nchini uliimarishwa kila kona, ambako wananchi wengi walifurika mitaani kumlaki kiongozi huyo.
Baada ya mazungumzo mafupi ya faragha, viongozi hao walikuja mbele ya waandishi wa habari kwa ajili ya kuulizwa maswali mbalimbali.
Waandishi na maswali
Kinyume cha matarajio ya wengi, waandishi wa habari wa Tanzania walionekana kutopewa nafasi ya kutosha kufanya kazi zao kwa uhuru kutokana na kupangwa katika eneo moja wakati wote wa matukio.
Hata ilipofika mkutano wao na marais hao, waandishi walipigwa butwaa kuona watu wanne pekee wakitajwa kuuliza maswali ambapo ni swali moja tu liliruhusiwa kwa waandishi wa Tanzania.
Pia maswali yaliyoulizwa hayakuwa na manufaa sana kwa Tanzania, kwani ukiachilia mbali swali la Mtanzania Peter Ambirikile wa gazeti la Jambo Leo, aliyeuliza kama marais hao wanaridhika na misaada ya miradi ya MCC inayotolewa na Marekani, waulizaji wengine walijikita kwenye migogoro ya mataifa ya Afrika.
Katika hotuba yake Rais Obama alisema maendeleo katika nchi za Afrika ikiwamo Tanzania yataletwa na Waafrika wenyewe, kwani Marekani inachofanya ni kuchochea miradi ya maendeleo.
Pamoja na hayo, alipongeza Tanzania kuwa na utawala bora, Bunge bora na hata kuendesha siasa za upinzani kwa amani.
Pia alipongeza Tanzania kuingia katika mchakato wa kupata Katiba mpya pamoja na kumpongeza Rais wa Zanzibar kwa kufanikisha kupata Katiba mpya.
Alisema anafurahi kusikia kuwa misaada wanayotoa imekuwa na matokeo chanya kwa Watanzania kutokana na kupunguza vifo vinavyotokana na ugonjwa wa malaria na maambukizi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kupungua.
Pia alisema mradi wa MCC umefanikiwa kwa Tanzania na kwamba itaingia katika awamu ya pili ya mradi huo.
Kuhusu mradi wa umeme wa Power Africa, alisema nchi nne ndizo zitafaidika na kwamba wametenga dola za Marekani bilioni saba kufanikisha mradi huo.
Aidha, alisema wataongeza fedha katika nchi za Afrika katika kukabiliana na magendo na ujangili.
Alisema ingawa ni mara yake ya kwanza kufika Tanzania, amefurahishwa na mapokezi maalumu aliyopata.
Rais Obama katika kujibu maswali ya migogoro hiyo ya Afrika katika nchi za Congo (DRC) na Misri, aliwaasa watawala kuheshimu wapinzani na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari.
Awali, Rais Kikwete, alisema Tanzania inaendelea kufurahia uhusiano wake na Marekani na kwamba misaada inayopata katika sekta mbalimbali imekuwa na faida kwa Watanzania.
Alitoa mfano kuwa misaada katika sekta ya afya imesaidia kupunguza vifo na misaada katika sekta ya elimu imesaidia kuongeza idadi ya wanafunzi shuleni.
“Misaada mingine tunayopata ni katika usalama wa chakula, umeme na maji,” alisema.
Alisema Marekani imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kulingana na mahitaji ya Tanzania na kutoa mfano katika miradi ya barabara, upatikanaji wa maji katika Jiji la Dar es Salaam na umeme vijijini.
“Tunaridhika na misaada tunayopata kupitia mradi wa MCC…nikisema hatujaridhika rais atakataa maombi mengine,” alisema.
Alisema misaada ya Marekani kwa kiasi kikubwa imesaidia kuboresha maisha ya Watanzania na kumuomba ikiwa anaweza kuendelea kuisaidia Tanzania afanye hivyo.
Kuhusu swali la ofisa wa ubalozi, Allan Mzengi, anayetuhumiwa kumdhalilisha kijinsia msichana wa Kitanzania, hatua iliyoilazimu Tanzania kulipa fidia alisema:
“Nalijua suala hilo, lilihusu msichana mdogo wa ofisa wetu wa ubalozi, walimchukua vizuri kwa lengo la kumsaidia kielimu, lakini kulitokea tofauti za kifamilia, yule msichana akashtaki akasema anafanyiwa vitendo vya unyanyasaji.
“Nakubali kulikuwapo na suala hilo ila faini iliyotolewa ilikuwa ni kubwa sana, hata kwa pensheni yangu ambayo nitalipwa baada ya kustaafu urais isingetosha kumlipa huyo, hata hivyo sehemu ya malipo hayo imekwisha kufanywa,” alisema Kikwete.
Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC One) ambacho pekee ndicho kilikuwa kikirusha matangazo hayo, mawasiliano yake yalikuwa yakikatika mara kwa mara, hivyo kuleta usumbufu kwa wananchi waliokuwa wakifuatilia ziara hiyo kupitia runinga hiyo au nyingine zilizokuwa zimejiunga na kituo hicho.
Tanzania yakosolewa
Katika hatua nyingine, wakati Rais Obama akipokewa kwa bashasha, gazeti maarufu nchini Marekani la The New York Times, limechapisha habari za kuonesha matukio ya ukatili yanayofanyika Tanzania.
Habari hiyo iliyochapishwa katika toleo lake ya Juni 30, imeleza tukio la kuteswa na kuumiza kwa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka.
Mwandishi wa habari hiyo amejaribu kunukuu kauli ya Dk. Ulimboka akieleza jinsi alivyotekwa na kuteswa kinyama kisha kutupwa kwenye Msitu wa Mabwepande.
Anasema kuwa Tanzania inaheshimika nje ya nchi kama kisiwa cha amani ndani ya ukanda wenye machafuko wa Afrika Mashariki.
Kwamba kutokana na sifa hizo, Tanzania imejizolea sifa na ufadhili wa fedha kutoka kwa mataifa mbalimbali yaliyoendelea, ikiwamo Marekani, ambayo mwaka jana iliipatia zaidi ya dola milioni 480.
Alisema kuwa wakati Rais Obama akiwasili Tanzania makundi ya kutetea haki za binadamu na chama kikuu cha upinzani wanasema matukio ya vitisho na ukandamizaji wa wapinzani wa kisiasa yanashika kasi. “Kuna woga, si amani”.
Ananukuu kuwa waandishi wamekuwa wakishambuliwa na mmoja aliuawa akiwa anatekeleza kazi yake ya uandishi wa habari.
Aliongeza kuwa Julai mwaka jana, serikali ililifungia gazeti huru la uchunguzi la kila wiki la Mwanahalisi, ambalo lilikuwa likiandika kwa undani kuhusu tukio la kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka, ambalo lilihusisha uhalifu huo na serikali ya Rais Kikwete.
Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari yenye makao makuu yake New York nchini Marekani, wiki jana ilimtaka Rais Obama kuliibua suala la uhuru wa vyombo vya habari atakapokutana na Rais Kikwete jijini Dar es Salaam.
Gazeti hilo pia limetaja vurugu za kisiasa kuwa zilichukua sura mpya na ambayo haikutegemewa wakati bomu la kurushwa kwa mkono lilipolipuliwa katika mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi wa madiwani wa CHADEMA na kusababisha vifo vya watu wanne mkoani Arusha.
“Hivi ni vitisho” ananukuliwa Dk. Willibrod Slaa, Katibu Mkuu wa CHADEMA. “Watu wataogopa kwenda kwenye vituo vya kupigia kura na wale jasiri watakuwa wameuliwa”.
Kwamba viongozi wa CHADEMA wamesema wazi wazi kwamba mtu aliyerusha bomu ni polisi au analindwa na polisi. Wamesema chama chao kipo tayari kuutoa mkanda wa video kuthibitisha tuhuma hizo, lakini lazima iwe mbele ya tume huru ya uchunguzi.
Lakini pia ananukuliwa kamishna wa Polisi anayehusika na operesheni, Paul Chagonja akipuuza tuhuma hizo na kuziita kuwa hazina msingi wowote, na alisema kuwa chama hicho kinapaswa kufikisha mikononi mwa polisi ili ufanyiwe kazi.
“Kazi ya msingi ya polisi ni kulinda usalama wa watu, hatufungamani na chama chochote cha siasa,” alisema Chagonja.
Pia ziara hiyo ya Rais Obama imekosolewa na wakazi wengi jijini Dar es Salaam, walidai kuwa imewaathiri katika shughuli zao za kiuchumi kutokana na kuhamishwa kwa muda katika maeneo yao ya biashara.
CHANZO TANZANIA DAIMA.
0 comments:
Post a Comment