OPARESHENI Fichua Maovu (OFM) chini ya Global Publishers bado ipo
mzigoni ambapo wiki hii imenasa tukio la hatari baada ya kumbamba
hausigeli akiuza duka la dawa muhimu ‘famasi’.
Kamera za OFM zilitegwa baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa watu
mbalimbali wakidai mhusika mwenyewe akiwa katika kazi nyingine tofauti
na duka hilo.
Tukio hilo linadaiwa kufanyika kwa muda mrefu katika duka hilo lililopo Goroka, Toangoma, Kongowe, Temeke nje kidogo ya Jiji la Dar.
Baada ya OFM kupokea taarifa hizo, ilianza utafiti wake ambapo
iligundua kuwa mmiliki wa duka hilo anatambulika kwa jina la mama Atu.
Ikadaiwa kuwa mmiliki huyo ana tabia ya kumuachia duka hilo hausigeli wake aitwaye Furaha ili auze dawa kwa kubahatisha na mara kadhaa wagonjwa hupewa dozi ndivyo sivyo.
“Kuna mwenzetu alikuwa akiugua ugonjwa mwingine, alipofika pale aliandikiwa dawa za malaria, hali yake ikawa mbaya hadi akakimbizwa hospitalini kulazwa, tulipomuonya mmiliki hakutusikia,” alisema mmoja wa watu wanaoijua ishu hiyo kiundani.
Ili kupata ushahidi kamili, OFM ilijifanya mgonjwa na kwenda kwenye famasi hiyo kuomba ushauri wa matibabu.
Hausigeli huyo alimtajia dawa za typhoid lakini shushushu wetu
alimkwepesha na kumuomba chloroquine ambapo hausigeli huyo alikubali na
kutaka kumpa bila wasiwasi.
Baada ya kushuhudia hayo OFM ilimfuata mwenyekiti wa mtaa huo, Issa Shomari kupitia mjumbe wake na kufika katika famasi hiyo kujionea hali halisi ambapo kama ilivyokuwa mwanzo hausigeli huyo alikuwa tayari kutoa huduma.
Baada ya kikosi kazi kujitambulisha na kumhoji, alikiri kuwa yeye ni mtumishi wa ndani, ana miaka 16, elimu ya darasa la saba, mwenyeji wa Iringa, huwa anaachiwa auze na mwajiri wake huku akifunguka kuwa hutoa dawa za malaria na magonjwa anayoyafahamu.
Akizungumza kwa mshtuko baada ya kujionea hali halisi, mwenyekiti huyo wa mtaa alisema kuwa atahakikisha anawasiliana na kamati ya afya ya Wilaya ya Temeke, Dar ili kuziondoa famasi kama hizo mtaani kwake.
0 comments:
Post a Comment