DK JUMA MWAKA AITUNISHIA SERIKALI MAHAKAMANI
JUMA Mwaka maarufu kama Dk. Mwaka na matabibu wenzake wanne wa tiba asili waliofungiwa usajili na kusimamishwa kutoa huduma wamedai mahakamani kwamba Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto hana mamlaka ya kutoa amri hiyo.
Madai hayo yalitolewa jana mbele ya Jaji Ama-Isario Munisi anayesikiliza kesi hiyo katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Mbali na Dk. Mwaka, wengine ni Fadhili Kabujanja wa Fadhaget Sanitarium, Abdallah Mandai wa Mandai Herbal Clinic, Tabibu John Lupimo wa Lupimo Suntarium Herbal Clinic pamoja na Tabibu Simon Rusigwa wa Sigwa Herbal Clinic.
Walalamikaji waliwasilisha maombi yao mawili dhidi ya Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Hata hivyo, upande wa Jamhuri uliwasilisha pingamizi la awali kupinga madai ya matabibu hao.
Upande wa walalamikiwa uliongozwa na mawakili wa serikali waandamizi, Silvester Mwakitalu na Ntuli Mwakahesya na kwamba waliwasilisha pingamizi la awali wakipinga maombi hayo.
Ilidaiwa kuwa matabibu hao hawakufuata taratibu zinazotakiwa kisheria kabla ya kufika mahakamani na hati za viapo vyao zina mapungufu ya kisheria kwa sababu hazina sahihi.
Hata hivyo, wakili wa walalamikaji, Dk. Lucas Kamanija, alidai uamuzi huo ulitolewa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, ambaye hana mamlaka kisheria ya kufanya hivyo.
"Mtukufu jaji tusingeweza kukata rufani Mahakama Kuu au kwa waziri kwa kuwa aliyetoa uamuzi hana mamlaka kisheria ya kufanya hivyo...hakuna uamuzi uliofanywa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala (mjibu maombi namba moja) ambao tungeweza kuukatia rufani,? alidai Dk. Kamanija.
Alidai kilichopo ni uamuzi wa katibu mkuu wa wizara hiyo, ambaye hakuna kifungu chochote cha sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala ambacho kinamruhusu katibu mkuu huyo kufanya uamuzi huo.
Akiwasilisha hoja katika maombi ya matabibu Mandai, Msingwa, Rupimo na Kabujanja ambao kuna waliofutiwa usajili huku wengine wakisimamishwa, wakili huyo alidai matabibu hao hawajakata rufani Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo kwa kuwa aliyeutoa ni katibu mkuu wa wizara hiyo ambaye hana mamlaka ya kufanya hivyo.
Pia alidai hati za viapo za matabibu hao zilizoambatanishwa kuunga mkono maombi hayo, zipo sahihi kisheria, hoja za kisheria na hitimisho kama inavyodaiwa na upande wa Jamhuri.
Kwa upande wa mawakili wa serikali, wakiwasilisha hoja za pingamizi ya awali, waliiomba mahakama kuyatupilia mbali kwa kuwa maombi yapo sahihi mahakamani hapo.
Wakili Mwakahesya na Mwakitalu walidai matabibu hao hawakufuata utaratibu kwa kuwa kutokana na kusikilizwa na hatimaye kuonekana wana hatia kama hawakuridhika na uamuzi huo walipaswa kukata rufani Mahakama Kuu.
Mwakahesya alidai sheria ipo wazi kwamba iwapo mtu aliyesajiliwa hajaridhika na uamuzi atatakiwa kukata rufani
Mahakama Kuu na sio kuwasilisha maombi kama walivyofanya matabibu hao.
Aidha, mawakili wa serikali walidai hati za viapo za matabibu hao ambazo zimeambatanishwa katika maombi hayo, haziko sahihi kwa kubeba vitu ambavyo havitakiwi kisheria yakiwAmo maoni na hitimisho.
Katika maombi ya tabibu Mwaka, mawakili hao wa serikali walidai tabibu huyo amekiuka taratibu na matakwa ya sheria kwa kuwa alitakiwa akate rufani kwa waziri wa wizara hiyo na sio kukimbilia mahakamani.
Pia upande huo ulidai hati ya kiapo cha Mwaka iliyoambatanishwa katika maombi hayo haipo sahihi kwa kubeba maoni, hoja za kisheria na hitimisho, hivyo waliiomba mahakama kuyatupilia mbali kwa gharama.
Kwa upande wa wakili wa tabibu Mwaka, Dk. Kamanija, alidai tabibu huyo asingeweza kukata rufani kwa kuwa hakuna uamuzi uliotolewa na baraza hilo ambao ungepingwa kwani kilichoko ni uamuzi wa katibu mkuu ambaye hana mamlaka ya kufanya hivyo. Baada ya kusikiliza hoja hizo, Jaji Munisi alisema atatoa uamuzi wa maombi hayo Agosti 19, mwaka huu.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment