
Ndugu zangu,
Katika
saa 20 na zaidi Rais Obama alipokuwa katika ardhi ya Tanzania,
sikusikia mahali popote akitamka jina la chama chake cha Democrat. Obama
ametamka ‘ AMERICA!’ mara zisizohesabika.
Kwa
kweli ujio wa Obama umetusaidia Watanzania kupumzika na kelele za
vyama, maana, kwa siku kadhaa, kabla na wakati wa ujio wa Obama,
Watanzania tumepata kupumzika na kusikia habari za vyama vya siasa na
malumbano yasio na hoja za msingi, mara nyingi yasio na tija kwa nchi na
maendeleo yake.
Hakika,
siasa ni kitu kizuri sana kwa nchi. Lakini siasa za ‘ ovyo ovyo’ ni
kitu kibaya kwa nchi. Na mara nyingi, siasa za ‘ ovyo ovyo’ ni kitu cha
hatari kwa nchi na mustakabali wake.
Picha
hiyo hapo juu ina mengi ya kutufundisha; kuwa siasa si uhasama.
Uchaguzi ukiisha watu mnarudi kwenye kufanya kazi. Kupigania maslahi ya
taifa. Si kuendeleza migogoro ya kisiasa na hata kuwepo kwa vurugu. Hayo
hayana tija kwa nchi.
Unapomwangalia
Obama na Bush kwenye picha ya pamoja wakiwa Dar na kwenye kutoa heshima
kwa wahanga wa ugaidi kwenye mlipuko ulitokea kwenye Ubalozi wao mwaka
1998, inadhihirisha ukomavu wa kisiasa.
Unachotumainia
hapa, kuwa ifike siku, hata hapa kwetu Tanzania, kwa Rais aliye
madarakani na Rais Mstaafu kutoka vyama viwili tofauti, tuone picha yao
wakiwa wamesimama pamoja kwenye makaburi ya kumbukumbu ya mashujaa wetu
wa Vita Vya Kagera kule Uganda.
Ndio,
picha hiyo hapo juu ni somo kwetu. Hawa wawili; Bush na Obama, ndio
tuliowaona kwenye kampeni zao wakipambana kiasi huwezi kufikiri wanaweza
kusimama pamoja kama ndugu wa taifa moja.
Lakini,
kwa wenzetu Marekani, siasa si uhasama wala mambo ya kuwindana.
Wanachogombania kwenye siasa ni kupewa heshima ya kuitumikia Marekani.
Na
heshima hiyo akipata mpinzani wako, basi, kwa wenzetu wanachofanya ni
kuungana mkono kwenye kazi ya maslahi ya Marekani bila kujali tofauti
zao za kiitikadi. Na ndicho tunachofundishwa kwenye picha hiyo.
Swali linabaki, Watanzania tuko tayari kubadilika kifikra kwa maslahi ya taifa letu?
About mtanda blog
Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari

0 comments:
Post a Comment