ZIARA ya Rais wa Marekani, Barrack Obama, imeacha nongwa kwa mawaziri wa Rais Jakaya Kikwete, Tanzania Daima Jumapili limebaini.
Nongwa hiyo imetokana na mawaziri wachache walioteuliwa kuhudhuria dhifa maalumu ya chakula cha jioni kwa ajili ya Rais Obama, kunyimwa fursa ya kuingia ndani ya ukumbi wa jengo la Ikulu, ilikoandaliwa dhifa hiyo.
Badala yake mawaziri hao maalumu walibaki nje. Wakishuhudia dhifa hiyo kupitia seti za televisheni zilizowekwa nje ya viunga vya Ikulu tofauti na inavyokuwa kwa viongozi wengine wanaoandaliwa sherehe za aina hiyo.
Kilichowakera zaidi ni hatua ya Rais Jakaya Kikwete kutoa agizo la kumuingiza ndani Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe na kuwaacha mawaziri hao wakibaki nje.
Tukio hilo lilitokea wiki iliyopita katika Ikulu ya Rais Kikwete wakati wa ziara ya Rais Obama aliyefika nchini Julai mosi na kuondoka Julai mbili.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya viunga vya Ikulu vilisema kuwa Mbowe alifika Ikulu akiambatana na wabunge na viongozi kadhaa wa CHADEMA, ambapo awali kulikuwa na taarifa kuwa chama hicho hakikupewa mwaliko.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, alikaririwa kuwa CHADEMA hakikuwa na mwaliko rasmi lakini hata hivyo Mbowe na viongozi wenzake walionekana wakiwa kwenye viwanja hivyo, hali iliyoashiria kulikuwapo na mwaliko rasmi wa chama hicho.
Mara baada ya Mbowe kuwasili, ulitumwa ujumbe kutoka ndani wa kumtaka kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuingia ndani ya ukumbi huo wa Ikulu ambapo Rais Obama alikuwa akiendelea kuzungumza.
Ingawa Mbowe hakupata nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na Rais Obama, lakini alipata fursa ya kuzungumza na ujumbe wa maofisa wa Ikulu ya Marekani walioongozana naye katika ziara hiyo ya kihistoria nchini.
Vyanzo vyetu vya habari kutoka ndani ya viunga hivyo vya Ikulu vilieleza kuwa kuitwa kwa Mbowe ndani ya ukumbi na kuwaacha mawaziri kulitokana na shinikizo la Ubalozi wa Marekani katika kutambua nafasi na mchango wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Kitendo hicho kiliwakera baadhi ya mawaziri waliokuwemo kwenye viunga vya Ikulu, lakini hawakupata fursa ya kuingia ndani na kuwa karibu na Rais Obama.
Baadhi ya mawaziri walioteuliwa kuwapo kwenye dhifa hiyo lakini hawakupata fursa ya kuingia ndani ya ukumbi ni pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), George Mkuchika na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wassira na wengine.
Waziri pekee aliyepata fursa ya kuingia ndani ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, lakini wengine wote waliishia nje ya viunga vya Ikulu.
Baadhi ya mawaziri walisikika wakihoji sababu ya Mbowe kupata fursa hiyo na wao kunyimwa wakati serikali yao ndiyo iliyomwalika kiongozi huyo.
Waziri mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa, alisema kama angejua hatapata fursa ya kuingia, asingekwenda Ikulu, badala yake angebaki nyumbani akiangalia runinga zilizokuwa zikirusha moja kwa moja kilichokuwa kikitokea Ikulu.
Kilio cha mawaziri hao kinafanana na kilio cha wananchi wengi waliojipanga barabarani kumpokea wakitarajia kumuona kwenye gari la wazi, lakini aliishia kwenye gari lake maalumu ambalo hata hivyo lilipita kwa spidi kali kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere kwenda Ikulu.
Rais Obama akiwa hapa nchini alifanya shughuli mbalimbali ikiwamo kutembelea eneo ulipokuwa ubalozi wa Marekani uliolipuliwa kwa bomu mwaka 1998 na kuzindua mitambo ya kufua umeme ya Kampuni ya Symbion.
Katika ziara hiyo Obama alisema serikali yake imetenga dola bilioni saba kwa ajili ya kusaidia miradi ya nishati ya umeme kwa nchi sita za Afrika.
Katika hotuba yake Rais Obama alisema kuwa mradi huo utakaofaidisha Watanzania katika awamu ya kwanza utagharimu kiasi cha dola bilioni saba na nchi nyingine zitakazonufaika nao ni Ethiopia, Kenya, Liberia, Nigeria, Uganda na Msumbiji.
Alisema kuwa sababu kubwa ya kuchagua nchi hizo imechagizwa na kuwa na malengo kabambe ya kufanya mageuzi katika sekta ya nishati kwa ajili ya kuboresha uwekezaji na ukuaji wa uchumi.
Obama alisema mpango huo maalumu wa maendeleo ya nishati unalenga kuhakikisha wakazi wengi hasa wa maeneo yasiyokuwa na umeme ambao ni asilimia kubwa wanapata huduma hiyo.
0 comments:
Post a Comment