Rais
Jakaya Mrisho Kikwete amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Omar
Bashir wa Sudan kufuatia kuuawa na kujeruhiwa kwa askari wa Tanzania,
walioko katika ulinzi wa kimataifa wa amani katika jimbo la Darfur na
kumtaka Rais huyo kuchukua hatua za haraka kuwasaka na kuwakamata
waliohusika na kitendo hicho kiovu na kuwafikisha mbele ya sheria haraka
iwezekanavyo
Katika
mazungumzo yao, Rais Omar Bashir amekubaliana na Rais Kikwete na
kumuahidi kuwasaka hadi kuwakamata wale wote waliohusika na
kuwachukulia hatua za kisheria.
Rais
Bashir amemueleza Rais Kikwete kuwa binafsi anaamini kuwa waliohusika
ni wahalifu na hivyo kuahidi kuwa lazima watasakwa hadi kukamatwa kwa
ajili ya kuchukuliwa hatua.
Rais
Bashir amempa pole Rais Kikwete kwa tukio hilo la kusikitisha ambapo
wanajeshi wa Tanzania wameenda nchini Sudan kulinda Amani na Usalama wa
wananchi wa Sudan.
Mapema
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa(UN) Bw. Ban Ki Moon alimpigia Rais
Kikwete na kumpa pole kwa mkasa huo mkubwa na wa kusikitisha ambao
umewatokea wa Tanzania hao wakati wakiwa katika kutekeleza jukumu lao la
kulinda amani nchini Sudan.
Hadi
sasa hakuna kikundi chochote ambacho kimekiri kuhusika na shambulio
hilo ingawaje kumekua na kutupiana lawama baina ya vikundi vya
kiserikali na vya waasi katika jimbo la Darfur.
Mapigano
baina ya vikundi vya kikabila na koo mbalimbali yamesababisha uvunjifu
mkubwa wa amani na usalama katika jimbo la Darfur kwa muda wa miaka 10
sasa, na mara nyingi mapigano na tofauti zao hizo zimesababisha vifo na
uvunjifu wa amani kwa wananchi wa Sudan na wageni pia.
Mwishoni
mwa mwaka jana Wanajeshi wanne kutoka Nigeria waliuawa karibu na El
Geneina , Magharibi mwa Darfur ambapo pia inaelezwa na Umoja wa Mataifa
kuwa wanajeshi wapatao 50 wameuawa tangu kikosi cha Umoja wa Afrika
kinachoundwa kwa pamoja chini ya Umoja wa Mataifa (UNAMID) kianze
operesheni yake mwishoni mwa mwaka 2007.
Taarifa
za Umoja wa Mataifa pia zinaeleza kuwa kabla ya mashambulizi
yaliyofanyika dhidi ya kikosi cha Tanzania Jumamosi iliyopita, wanajeshi
6 wanaolinda Amani wameuawa tangu Oktoba mwaka huu ambapo pia
inasadikiwa kuwa watu wapatao 300,000 wameyakimbia makazi yao.
Hata hivyo kiini cha mgogoro huo unaosadikiwa kuwa ni ugomvi wa ardhi na rasilimali zilizoko katika jimbo hilo nchini Sudan.
Miili ya maaskari hao saba wa Tanzania inatarajiwa kuwasili nchiniIijumaa tarehe 19, Julai kwa ajili ya maziko.
About mtanda blog
Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
0 comments:
Post a Comment