RAIS wa Sudan, Omar Bashir, amesema atachukua hatua zote za kuwasaka kwa
kila hali watu waliohusika na tukio la kuwaua askari saba wa Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), katika Jimbo la Darfur Jumamosi iliyopita.
Mbali ya mauaji hayo, askari wengine 14 walijeruhiwa vibaya, huku mmoja wapo hali yake inaelezwa kuwa mbaya.
Taarifa
iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu mjini Dar es Salaam jana,
ilisema Rais Bashir alitoa kauli hiyo, baada ya kufan
ya mazungumzo na
Rais Jakaya Kikwete kwa simu.
“Rais amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais Bashir, kufuatia
kuuawa na kujeruhiwa kwa askari wa Tanzania, walioko katika ulinzi wa
kimataifa wa amani katika Jimbo la Darfur na kumtaka Rais Bashir
kuchukua hatua za haraka kuwasaka na kuwakamata waliohusika na kitendo
hicho kiovu na kuwafikisha mbele ya sheria haraka iwezekanavyo,
“Katika
mazungumzo ya viongozi hao, Rais Omar Bashir amekubaliana na Rais
Kikwete na kumuahidi kuwasaka hadi kuwakamata wale wote waliohusika na
kuwachukulia hatua za kisheria,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa
hiyo ilisema, Rais Bashir amemhakikishia Rais Kikwete kuwa binafsi
anaamini waliohusika ni wahalifu ambao lazima wasakwe na kuchukuliwa
hatua.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
(UN), Ban Ki Moon naye alimpigia Rais Kikwete simu na kumpa pole
kutokana na tukio hilo.
Taarifa hiyo, ilisema hadi sasa hakuna
kikundi chochote ambacho kimekiri kuhusika na shambulio hilo, ingawa
kumekua na kutupiana lawama baina ya vikosi vya kiserikali na vikundi
vya waasi katika Jimbo la Darfur.
Mwishoni mwa mwaka jana,
wanajeshi wanne kutoka Nigeria, waliuawa karibu na El Geneina magharibi
mwa Darfur, ambapo pia inaelezwa na Umoja wa Mataifa kuwa wanajeshi
wapatao 50 wameuawa tangu kikosi kianze kazi ya kulinda amani mwishoni
mwa mwaka 2007.
SILAHA
Katika hatua nyingine, Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, imesema kuna uwezekano mkubwa Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa (UN), likafanya mabadiliko katika baadhi ya
vipengele vyake.
Kwa mujibu wa sura namba sita ya mkataba wa UN,
majeshi yanayolinda amani katika Jimbo la Darfur hayaruhusiwi kubeba
silaha za kivita.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Idara ya
Mawasiliano wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Mkumbwa Ali, alisema kutokana na shambulio hilo ni wazi kuwa UN
itachukua hatua kuhakikisha kuwa wanajeshi waliopo Darfur wanajihami.
“Bila
shaka, tukio hili litatoa tahadhari nyingine ikiwamo ya kujihami na
hatari kwa kutumia sura namba saba, wataweza kujibu mapigo,” alisema
Ali.
Naye, Ofisa Habari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi la
Tanzania (JWTZ), Meja Joseph Masanja alisema lengo la majeshi ya kulinda
amani ya UN, ni kutafuta suluhu ya amani na si kupigana vita kwenye
Jimbo la Darfur.
MIILI KUWASILI
Kuhusu miili ya wanajeshi saba waliouawa
kuletwa nchini, Ali alisema wanawasiliana na UN, kupata taarifa za
uhakika za kuwasili miili hiyo.
“Ikumbukwe kuwa kikosi cha Tanzania kipo chini ya mwamvuli wa UN, hivyo shughuli zote zipo chini ya UN.
“Hatuna
sababu ya kuficha, tunasubiri taarifa sahihi kutoka UN ndipo
tuufahamishe umma, hadi sasa hatujaletewa taarifa inayoeleza siku ambayo
miili hiyo itawasili,” alisema Masanja.
MAKAIDI
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha National League for
Democracy (NLD), Dk. Emmanuel Makaidi ameishauri Serikali kuwarejesha
askari wa JWTZ, wanaolinda amani katika nchi za Sudan na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Akizungumza na MTANZANIA juzi, Dk.
Makaidi alisema Serikali inapaswa kufanya hivyo, ili kuepusha uwezekano
wa askari wa Tanzania kukumbwa na vifo vingine kutokana na mashambulizi
yanayofanywa na vikundi vya waasi wa nchi hizo.
Alisema kazi
wanayoifanya askari hao nchini Sudan, haina maslahi ya moja kwa moja kwa
Tanzania na kwamba sababu zilizotolewa na JWTZ kuhusu vifo hivyo
hazijitoshelezi.
“Sababu za vifo vya askari wetu zilizotolewa na
jeshi ni za kitoto, hivi unawezaje kulinda bila silaha tena ugenini, eti
umekwenda kulinda amani, hii ni sababu ya maana kweli?” Alihoji.
Alisema
nchi isiburuzwe kwa kisingizio cha kulinda amani barani Afrika na
kwamba ushinikizwaji wa aina hiyo ni matokeo ya nchi kuwa na sera mbaya
ya mambo ya nje.
Sarah Mossi, Rachel Mrisho na Esther Mbusi (Dar es Salaam).
CHANZO MTANZAANIA
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment